Njombe. Wanafunzi wenye ulemavu katika shule ya Mundindi, iliyopo katika Wilaya ya Ludewa, mkoani Njombe, wamepatiwa mashine ya kufulia na kukaushia nguo, yenye thamani ya Sh1.7 milioni, na wanachama wa kundi la WhatsApp wilayani humo, ikiwa ni jitihada zao kuwafikia watu wenye uhitaji.
Aidha, kundi hilo limekabidhi mabuti ya mvua 160, yenye thamani ya Sh1.6 milioni, kwa wafungwa wa gereza la Ibihi lililopo wilayani Ludewa.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, kwa niaba ya kikundi hicho leo, Januari 6, 2026, kiongozi wa msafara huo, Vasco Mgimba, amesema huo ni utaratibu wa kawaida kwa kikundi hicho kuwafikia wenye uhitaji katika wilaya hiyo na kutoa misaada mbalimbali.
Amesema katika kusherehekea Mwaka mpya wa 2026, kikundi hicho kimeona ni vema kuwafikia watoto wenye ulemavu na wafungwa, ili kutoa faraja kwa makundi hayo muhimu katika jamii.
“Tumekuwa na utaratibu wa sisi kama kikundi kuyafikia makundi mbalimbali, na kwa mwaka huu tumeona tuanze na hawa watoto wenye ulemavu na wafungwa kwenye gereza letu,” amesema Mgimba.
Amesema kupitia michango ya wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya wilaya hiyo, kikundi hicho husaidia kwa kiasi kikubwa kutoa sadaka hiyo kila mwaka kwa watu wenye uhitaji.
Ametoa wito kwa wadau wengine na makundi katika jamii kuiga mfano huo kwa kutoa msaada kwa makundi yenye mahitaji, ili kuendelea kuleta faraja na kuunga mkono maendeleo ya jamii.
Mmoja wa wanakikundi hicho, Christa Nyenza, kwa niaba ya wenzake ambao ni Damian Kunambi, Ally Ponda Shaura na Wise Mgina, amemshukuru mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Sunday Deogratias, kwa ushirikiano na mchango wake chanya katika kikundi hicho.
Amesema ushirikiano huo umekuwa kichocheo cha umoja, mshikamano na utekelezaji wa shughuli za kijamii zenye manufaa kwa wananchi.
“Tunamshukuru sana mkurugenzi wetu wa Wilaya ya Ludewa kwani amekuwa chachu ya kufanikisha jambo hili muhimu lenye kusaidia jamii ndani ya wilaya yetu,” amesema Kunambi.
Mkuu wa Idara ya Elimu Msingi Wilaya ya Ludewa, Daniel John, amekishukuru kikundi hicho kwa kutoa msaada huo wa mashine ya kufulia na kukaushia, akisema utaongeza ufanisi katika mazingira ya huduma na maisha ya walengwa.
“Msaada huu umekuja wakati muafaka, hivyo tunawashukuru wanakikundi, na msaada huu utaongeza ufanisi katika mazingira ya huduma na maisha ya walengwa,” amesema John.
Naye Mkuu wa Gereza la Ibihi, Eden Lwamnana Biralo, amesema msaada huo wa mabuti kwa wafungwa wa gereza hilo, utaongeza ufanisi wa kufanya kazi na kuleta maendeleo kwa wafungwa hao na jamii inayowazunguka.
“Tuwashukuru wanakikundi kwa kutuona na kuona umuhimu wa kuwakumbuka wafungwa na kutoa msaada huu wa mabuti, tunawaombea kesho watuone kivingine,” amesema Biralo.