ALICHOKIFANYA kinda wa Azam FC anayecheza nafasi ya beki wa kati, Twalibu Nuru, kimemfanya kocha wa kikosi hicho, Florent Ibenge kumtabiria siku si nyingi ataitumikia Taifa Stars.
Kinda huyo ameonyesha kiwango kizuri katika michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 inayoendelea kuchezwa Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Unguja, huku Azam ikifuzu nusu fainali ikienda kucheza dhidi ya Simba.
Katika michuano hiyo, kinda huyo amecheza mechi zote tatu hatua ya makundi kwa dakika 225, huku ile ya kwanza dhidi ya Singida Black Stars akitokea benchi na kuingia mwanzoni mwa kipindi cha pili akichukua nafasi ya Mtunisia, Taieb Ben Zitoun, akacheza sambamba na Edward Manyama.
Baada ya hapo, mechi zilizofuata dhidi ya Mlandege na URA, alicheza mwanzo mwisho akiwa pacha na Lameck Lawi.
Ibenge amemzungumzia kinda huyo akisema: “Ana ubora mzuri, akiendelea hivi muda si mrefu nitamuona akicheza timu ya taifa kwani ana ubora huo wa kuitumikia Tanzania.
“Kwa sasa anatakiwa kuongeza juhudi na ndio maana nampa nafasi kuonyesha uwezo na kupata uzoefu zaidi. Nampongeza kwa kuonyesha juhudi kubwa ya kupambana, anahitaji kucheza mechi zaidi ili kuongeza ubora wake na uzoefu kwani bado kijana mdogo,” amesema Ibenge.
