::::::::::
Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) umetangaza kurejea kwa huduma za kivuko cha MV KAZI, kinachotoa usafiri wa abiria na magari kati ya Kigamboni na Magogoni jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa TEMESA, kivuko hicho kilisimamisha huduma kuanzia Januari 5 hadi Januari 8, 2026, kuanzia saa mbili usiku, kutokana na sababu za kiusalama.
Hata hivyo, kwa sasa huduma za kivuko hicho zimeanza kutolewa kama kawaida, huku abiria na magari vikiendelea kuvushwa bila changamoto.
TEMESA imesema inaendelea kufuatilia kwa karibu hali ya hewa, ili kuhakikisha usalama wa abiria pamoja na mali zao wakati wote wa safari.
Aidha, uongozi wa wakala huo umeomba radhi kwa abiria wote waliopata usumbufu kutokana na kusimamishwa kwa huduma katika kipindi hicho.
Wananchi wameshauriwa kuendelea kuchukua tahadhari, ikiwemo kufuatilia taarifa rasmi za utabiri wa hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).
Pia, TEMESA imesisitiza umuhimu wa kuzingatia maelekezo ya mabaharia wa vivuko kwa ajili ya usalama wao.
Kwa ujumla, TEMESA imedai itaendelea kuchukua hatua zote muhimu kuhakikisha usalama, ufanisi na uendelevu wa huduma za vivuko kwa wananchi.
