KVZ Yaondoka na somo Yanga Mapinduzi Cup

POINTI moja waliyokusanya KVZ walipocheza dhidi ya TRA United, kisha wakafungwa 3-0 na Yanga, kuna funzo kubwa wamelipata makamanda hao wa Kikosi Cha Valantia Zanzibar.

KVZ iliyokuwa kundi C, imeaga mashindano ikiwa na pointi moja, huku leo Jumanne ikifahamika timu gani itafuzu nusu fainali pale Yanga yenye pointi tatu itakapocheza na TRA United iliyokusanya pointi moja.

Kocha Msaidizi wa KVZ, Khalid Omar, amesema licha ya kupoteza dhidi ya Yanga, lakini kuna kitu wamejifunza kutoka kwa wapinzani wao hao.

Amesema kutokana na ukubwa wa Yanga, wao kama KVZ ambao wanataka nao kuwa wakubwa, kuna vitu wanaendelea kujifunza ili kufikia malengo na kupitia mechi yao dhidi ya Yanga, kuna kitu wameongeza.

“Itaendelea kubaki kwamba Yanga ni timu kubwa kwetu na licha ya kupoteza dhidi yao lakini tumejifunza kitu kutoka kwao. Tuna mambo mengi ya kuangalia kutoka kwa Yanga katika kujifunza kwetu sisi KVZ kwani tuna malengo ya kufika mbali.

“Safari yetu imeishia hapa, lakini kwa ujumla mashindano yametupa somo ambalo tunakwenda nalo uwanja wa mazoezi kufanyia kazi pale palipokuwa na mashimo, ili kuwa bora kuelekea mechi zetu za Ligi Kuu Zanzibar,” amesema kocha huyo.

KVZ ilianza Kombe la Mapinduzi 2026 kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya TRA United, kisha ikafungwa mabao 3-0 na Yanga katika mechi ya mwisho kundi C. Matokeo hayo yameiondosha KVZ mashindanoni ikiwa na pointi moja.