Madereva Watanzania waliokwama DRC waiangukia Serikali, yenyewe yajibu

Dar es Salaam. Zaidi ya madereva 100 wa malori kutoka Tanzania wamekwama Jamhuri ya  Demokrasia ya Congo (DRC) kufuatia tishio la kiusalama.

Madereva hao ambao kwa mujibu wa waliozungumza na Mwananchi wamezuiwa kuendelea na safari kutokana na vurugu za wananchi dhidi ya Serikali ya nchi hiyo.

Wamesema vurugu hizo zimeripotiwa leo Jumanne Januari 6, 2026 zikiwahusisha wachimbaji wadogo wa madini kufuatia tamko la Serikali kuwazuia kufanya shughuli zao.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, mmoja wa madereva hao, Frank Egina amesema madereva waliokwama katika Mgodi wa Kisamu wamejikuta katika hali hiyo kutokana na kutoweka kwa hali ya amani iliyosababisha shughuli zao kusimama na kuwalazimu kubaki bila uhakika wa usalama wao.

“Wachimbaji wadogo kwa kugomea tamko la Serikali wameamua kufanya fujo, mimi nilifika huku Jumapili na kufanikiwa kushusha mzigo vizuri, lakini leo nipo hapa Kisamu tumezuiwa kutoka mpaka hali itakaporejea,” amesema Egina.

Hassan Maganga, dereva mwingine anayefanya safari zake kutoka Dar es Salaam kwenda DRC amesema hali ni mbaya katika mitaa ya eneo hilo huku usalama ukibaki sehemu ya mgodini walipokaa wakiwa katika ulinzi mkali wa vyombo vya ulinzi na usalama vya Taifa hilo.

“Hapa tulipo usalama ni mdogo sana maana tupo salama hapa tu tunapolindwa, lakini huko nje hali ni mbaya sana,” amesema.

Ameongeza kuwa, hali ya usalama kwa madereva wa Kitanzania wanapoingia nchini humo si ya kuridhisha, kwa kuwa  wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi, ikiwamo vitisho vya usalama, vikwazo vya usafiri na mazingira yasiyotabirika, hali inayowatia hofu na kuhatarisha utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Dereva mwingine, Lukman Rashid, ambaye ni miongoni mwa madereva waliokwama nchini humo, ameiomba Serikali ya Tanzania kuingilia kati  kuwasaidia, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu ili kuhakikisha usalama wao.

Amesema madereva wanapofika eneo la Kisamu,  wengi wanapitia dhoruba nyingi zikiwamo kupigwa, kuuawa na magari kuchomwa moto akiomba Serikali iwasaidie washushe mizigo kabla ya kufika huko.

“Ninaomba Serikali iingilie kati na waajiri wetu pia, badala ya kufika hadi huku tuwe tunashushia mizigo Kasumbalesa huko ni eneo salama,” amesema.

Ameongeza kuwa ukatili dhidi ya madereva wa Tanzania kutoka kwa vyombo vya ulinzi na usalama wa nchi hiyo ni mkubwa akisema wakishushia mizigo Kasambalesa itawasaidia kuepuka athari hizo.

“Tanzania inaongoza kuleta madereva wengi hapa Congo, hapa tulipozuiliwa sisi tupo zaidi ya madereva 50 na kuna migodi mingi sana huko nako wapo wengi tu wamezuiwa,” amesema.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne, Januari 6, 2026, kwa njia ya simu kuhusu changamoto zinazokabili madereva, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo

 amesema kuwa, hatua mbalimbali tayari zimeshachukuliwa ili kuhakikisha usalama na ustawi wa madereva hao, huku akisisitiza umuhimu wa kushirikiana na mamlaka husika ili kuondoa vikwazo vinavyokwamisha shughuli zao.

 “Kuhusu hali ya kiusalama tumeshapata taarifa na tayari hatua zimeshachukuliwa kuhakikisha wanaendelea na shughuli zao kwa usalama,” amesema.

Balozi wa Tanzania nchini DRC, Juma Mshana amesema maofisa wa ubalozi wa Tanzania nchini humo wamekuwa mstari wa mbele katika kusikiliza na kutatua changamoto wanazokutana nazo madereva, akitoa wito kutumia ofisi yake kwa msaada wa haraka.

“Tumekuwa tukifuatilia kila kinachotokea na  tumetoa namba zetu za simu kwa viongozi wote wa madereva ili wapatapo shida waweze kutufikia na kuwasaidia.

“Niwaombe madereva wote wanapopata changamoto watoe taarifa za haraka kuhusu tatizo lililopo na mahali walipo ili tuweze kuwafikia na kutatua changamoto hizo kwa haraka,” amesema.