Dar es Salaam. Zikiwa zimepita siku 92 tangu aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole alipotekwa na watu wasiojulikana, familia yake leo Jumanne, Januari 6, 2026, imefika katika nyumba aliyokuwa amepanga eneo la Boko Basihaya jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuhamisha mali zake na kuisafisha.
Mbali ya kukusanya na kufungasha mali za ndugu yao, familia hiyo pia imesali sala maalumu ya kumwombea mpendwa wao kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari.
Polepole ambaye aliwahi kuwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), anadaiwa kuchukuliwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake Jumatatu, Oktoba 6, 2025 na hadi sasa hakuna mamlaka wala kundi lililoeleza kufahamu alipo wala usalama wake.
Tukio hilo lilitokea miezi michache baada ya Polepole kutangaza kujiuzulu wadhifa wa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Julai 13, 2025.
Baadaye Jumanne, Agosti 5, 2025, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kupitia Katibu Mkuu wake, Balozi Samwel Shelukindo ilitangaza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ametengua uteuzi wa Polepole na kumwondolea hadhi ya ubalozi, kufuatia taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka.
Mwananchi ilipofika katika nyumba hiyo leo, imeshuhudia shughuli za ufungaji wa mali za Polepole zikiendelea, huku mama yake mzazi, Annamary Polepole akisimamia shughuli hiyo kwa karibu, huku hisia na masikitiko miongoni mwa wanafamilia vikitawala.
Kwa mara ya kwanza tangu kutoweka kwa Polepole na polisi kuweka utepe wa zuio katika nyumba hiyo, leo familia imeruhusiwa kuingia ndani na kushuhudia hali iliyoacha maswali mengi.
Ndani ya chumba kimojawapo, kumeonekana mabaki ya damu iliyokauka ikiwa imetakaa katika baadhi ya maeneo, huku mlango wa kuingilia kwenye chumba hicho ukiwa umevunjwa.
Ndugu wa Polepole, walianza kufuta damu hiyo katika maeneo mbalimbali ya nyumba hiyo, ili iwe safi kabla ya kukabidhiwa kwa mmiliki kwa matumizi mengine.
Kutokana na kile walichokikuta ndani ya nyumba hiyo, mama mzazi wa Polepole ameshindwa kuficha hisia zake, akieleza masikitiko yake huku akiomba kama kuna watu wanamshikilia, wamrudishe mwanawe.
Annamary amesema anatamani mwanawe aachiwe huru na kama kuna tuhuma au makosa dhidi yake, hatua za kisheria zichukuliwe waziwazi.
“Wanirudishie mwanangu. Kama ana makosa, basi afikishwe mahakamani. Yeye ndiye aliyekuwa akinihudumia kwa chakula na mahitaji mengine ya kila siku,” amesema Annamary kwa masikitiko.Bottom of Form
“Wanasema tusomeshe watoto ili watusaidie lakini leo wanawakamata na tunahangaika, naomba mwanangu arudi na akiwa mzima.
“Tunatoa vyombo kwa sababu, ni nani atakayelipa kodi ni nyumba aliyokuwa amepanga, sina mtu wa kulipa kodi, mimi ni maskini wa kutupwa, mimi ni mkulima tu. Nilipoona Humphrey amefikia hapa nilishukuru tu,” amesema.
“Ndani ya nyumba nimekuta damu si kawaida, naomba wamrudishe mwanangu akiwa mzima, wamrudishe mwanangu akiwa mzima, lolote litakalotokea na mimi nilizaliwa na Mungu kutoka mbinguni, nitajua la kufanya. Kila aliyegusa ule mwili kwa namna yoyote na yeye atakufa,” amesema mama huyo.
Ameyasema hayo wakati vitu vyote ndani ya nyumba hiyo vikiwa vimejaa vumbi la muda mrefu, friji ikiwa na vitu vilivyoharibika na ilitoa harufu kali kila mlango ulipofunguliwa.
Hayo yamefanyika wakati nyumba hiyo ikiwa haina umeme hadi sasa, ikidaiwa rimoti ya kuwekea umeme ni miongoni mwa vitu vilivyokusanywa na Jeshi la Polisi wakati askari walipofika nyumbani hapo kufanya upelelezi.
Akizungumzia suala hilo, Wakili Maduhu William kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) aliyeshuhudia tukio hilo, amesema vyombo hivyo vinatolewa kwa sababu mkataba wa upangishaji wa nyumba unaisha Janauri 11, mwaka huu.
Kufuatia mazingira hayo, kama familia iliitafuta ofisi yake ili kujua utaratubu wa namna wanavyoweza kutoa vitu vya Polepole katika nyumba hiyo.
Hali hiyo waliamua kwenda kuomba kibali polisi waweze kuingia ndani ya nyumba na kutoa mali zao, kwa sababu ilikuwa imepigwa marufuku mtu yeyote kuingia ndani.
“Wanachukua vyombo hivi na wanakwenda kuvihifadhi nyumbani kwao. Mimi kama wakili, hadi leo Polepole hajulikani alipo, tunaiomba Serikali na mamlaka zote kueleza Polepole alipo na ana hali gani kwani Tanzania ni nchi inayoongozwa kwa mujibu wa sheria,” amesema Maduhu.
Amesema kupitia sheria za nchi, mtu mwenye makosa anatakiwa kukamatwa ili apelekwe polisi ambako atahojiwa na upepelezi kufanyika kabla ya kupelekwa kwa Mwendesha Mashataka (DPP) ili mtu apelekwe mahakamani.
“Ukipelekwa huko Serikali inaendesha kesi yake, mtu unapewa nafasi ya kujitetea wakati ambao mahakama inafanya tathmini ya ushahidi na kutoa hukumu huku ikieleza kama tuhuma ni za kweli au uongo,” amesema.
Amesema tofauti na hapo hakuna mtu mwenye mamlaka ya kumchukua mtu mwingine na kumpeleka sehemu yoyote au kumuua.
Amesema mahakama pekee ndiyo yenye mamlaka ya kuua kupitia hukumu ya kesi mbalimbali ambazo unaweza kunyongwa hadi kufa. Mfano wa kesi hizo ni uhaini.
“Nje ya mahakama, hakuna mtu anayeruhusiwa kumkamata mtu na kwenda kumtoa uhai wake. Tanzania ni nchi inayoongozwa kwa mujibu wa sheria,” amesema.
Amesema Jeshi la Polisi linadai kuendelea na upelelezi lakini mara zote wamekuwa wagumu kusema wamefikia hatua gani huku akitaka hilo liwekwe wazi.
“Tunaendelea kusisitiza kuwa kama kuna watu wanamshikilia mahala wamtoe wampeleke polisi ili ahojiwe kama ana makosa apelekwe mahakamani, kama kuna kosa haki itendeke kila upande.
Ameongeza:”Sisi hatusemi kama Polepole ni mtu safi, kama ana makosa ziko mahakama apelekwe ili waseme kama ana kosa au hana, lakini mtu ambaye si mahakama kumchukua mtu na kwenda kumficha mahali halikubaliki,” amesema.
Mdogo wa Polepole, Godfrey Polepole amesema wakati wanahamisha vyombo wamebaini kukosekana kwa baadhi ya vitu ndani ya nyumba na wana uhakika kuwa vilibebwa na Polisi, Oktoba 7, mwaka jana walipofika nyumbani hapo.
“Safe ya kuhifadhia hela hakuna, kompyuta mpakato nane hazipo, simu tano, kitambulisho cha taifa na hati ya kusafiria. Wamevunja pia mlango wa gari na kuchukua safe ya hela iliyokuwa ndani yake, wamechukua nyaraka zote zilizokuwa ndani ya gari, kulikuwa na pikipiki ndogo ambayo nyuma huwa ina toolbox wameondoka nayo, antenna ya intaneti wamebeba,” amesema.
Vingine vilivyokosekana ni funguo za pikipiki, kamera za studio na walivunja baadhi ya kamera na taa zilizokuwapo studio.
“Sikuona ushirikiano wa Jeshi la Polisi kwa familia, ila sisi kama familia tulimpigia mmoja wa askari ambaye yeye ndiye alishiriki kubomoa mlango wa gari, tuna uhakika nalo, sitamtaja kwa jina ila nilimuuliza mwendelezo wa kinachoendelea kwenye uchunguzi na alisema hajui lolote linaloendelea nawatafute mabosi zake,” amesema.
Amesema amaamini Jeshi la Polisi linafanya kazi kwa weledi, sikivu na linasimamia haki za raia na mali zao huku akiamini watafanyia kazi.
Akizungumzia madai hayo na wapi vitu vilivyochukuliwa na polisi vilipo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro aliomba muda kufuatilia suala hilo.
“Hivi ndiyo nakusikia wewe unanipa hadithi nyingine, sijui nyumba ya nani imefanya nini vitu, kwa kukusikia wewe nipe muda nifuatilie,” amesema Muliro alipozungumza simu na Mwananchi.
