Mamia wajitokeza kujiandikisha Nida Tabata, vyeti vya kuzaliwa kikwazo

Dar es Salaam. Licha ya idadi kubwa ya wananchi kujitokeza kujisajili ili kupatiwa kitambulisho cha uraia (Nida), Jimbo la Segerea, Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, kigezo cha kuwa na cheti cha kuzaliwa imeonekana kuwa kikwazo kwa wengi kuweza kupata huduma hiyo.

Mwananchi ambayo imefika Jumatatu Desemba 5, 2026 katika ofisi ya mtendaji kata ya Tabata ambapo shughuli hiyo inafanyika ilishuhudia mamia ya wananchi wakiwa katika foleni wakisubiri kupata huduma hiyo.

Hata hivyo, wengi walionekana kuondoka mara maofisa Nida walipofika na kuwaeleza kuwa cheti cha kuzaliwa kuwa nacho ni lazima hasa kwa waliozaliwa kuanzia miaka ya 1980 kwenda mbele.

Ofisa usajili wa Nida akiwa anamuhudumia mwananchi aliyefika kujiandikisha.

Waliozaliwa miaka ya 1970 kurudi nyuma walitakiwa kuwa na kiapo kutoka mahakamani.

Baadhi ya wananchi wakizungumza na Mwananchi Digital, akiwamo Frida Abdallah, amesema tangazo lililotolewa na walichokikukuta ni tofauti.

“Katika tangazo lililotolewa kuhusu shughuli hii ambalo wengi tuliliona kwenye makundi ya WhatsApp lilieleza kuwa unaweza kuja na kitambulisho cha kupiga kura, leseni au kitambulisho cha shule.

“Pamoja na kujihimu kufika hapa saa 11:00 asubuhi, muda huu wa saa 6 tunakuja kuambiwa kuwa lazima cheti cha kuzaliwa au kiapo kwa wale waliozaliwa miaka ya kuanzia 1970 kurudi nyuma, nakipata wapi saa hizi wakati mchakato wake wa kukipata sio rahisi,” amesema Frida.

Katika wito wake, Frida ameshauri kunapokuwa na shughuli kama hizo ni vema mamlaka zote zinazohusika ziwepo, wakiwamo wanaotoa vyeti vya kuzaliwa ili wananchi kupata urahisi wa huduma.

Joyce Maiko, mkazi wa Buguruni Mnyamani, amesema nyaraka zote anazo ikiwamo cheti cha kuzaliwa isipokuwa amekwama hana namba za Nida za baba wala mama yake ambao walishafariki miaka ya 2000, hivyo kutakiwa kwenda kuapa mahakamani.

Msajili wa Nida Mkoa, John Itimba akiwa anamihudumia mmoja wananchi waliofika kujiandikisha kupata vitambulisho vya Taifa.

“Mimi nadhani ifike mahali Serikali ipunguze michakato katika kupata Nida kwani mimi pamoja na kuwa na nyaraka zote, Nida za wazazi tu ndio zimenikwamisha, nazipata wapi, wakati baba alifariki mwaka 1990 na mama alifariki mwaka 2000,” amesema Joyce.

Kwa upande wake, Baraka Kichere aliyekuwa akikamilisha nyaraka zote, amepongeza ofisi ya Nida kushuka kwa wananchi kwa kile alichoeleza imekuwa ngumu kwenda ofisini kwao kutokana na kuwepo kwa foleni kubwa inayokinzana na muda wake wa kujitafutia riziki.

“Ukitaka kufuatilia Nida inamaana uache kazi zako siku nzima na hii Januari tunakimbizana na mahitaji ya shule ya watoto, hivyo kitendo cha wao kuja huku mtaani kwetu ni cha kupongeza, maana unafika unahudumiwa unaenda kuendelea na shughuli zako nyingine.

Wakati wananchi wakiwa na maoni hayo, Msajili wa Nida Mkoa, John Itimba, amesema katika usajili huo cheti cha kuzaliwa hakiepukiki.

Kutokana na hilo, ametoa wito kwa wanaohitaji kujisajili kuhakikisha wanakuwa na nyaraka hiyo pamoja na nyingine zilizorodheshwa na kubainisha kuwa huduma inayotolewa ni kwa wale wanaojiandikisha kwa mara ya kwanza (yaani wapya).

“Nyaraka zingine zinazohitajika ni pamoja vyeti vya kuzaliwa vya wazazi, vyeti vya Nida vya wazazi, vyeti vya shule na barua ya utambulisho kutoka kwa ofisi ya Serikali ya mtaa wake,” amesema Itimba.

Akizungumzia sababu ya kufanya shughuli hiyo ya usajili, amesema ni moja ya mpango wao ulipo kwa mwaka huu na malengo ni kufanya katika majimbo yote yaliyopo Wilaya ya Ilala wameanza na la Segerea.

Sababu nyingine iliyowasukuma, amesema kumekuwa na idadi ndogo ya watu wanaofika ofisini kwao kwenda kujiandikisha, hivyo wameona wawafuate mtaani.

“Tumegundua wananchi wengi bado wana uhitaji wa vitambulisho, hivyo ni wachache wanaofika ofisini kwetu, hivyo hii ni kama fursa kwao wanapaswa kuitumia kwa kuwa kwa siku 30 katika shughuli hii tunatarajia kuwafikia watu 30,000.

Awali, mratibu shughuli hiyo ambaye pia ni mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Tabata Mtambani, Heri Vuoni amesema hii ni mara ya pili kufanyika kwa shughuli hiyo ambapo mara ya kwanza waliifanya mwaka 2024 na kuweza kuwafikia watu 8,000.

Hata hivyo, Vuoni amesema katika shughuli ya leo hadi kufika saa 7:00 mchana, zaidi ya watu 500 walikuwa wamejiandikisha kuhitaji huduma hiyo.

Naye mwenyekiti wa Serikali ya mtaa huo, Abdallah Shomari amesema waliomba huduma hiyo muda mrefu katika mtaa wake na anashukuru hilo limefanikiwa.