KITENDO cha Muembe Makumbi City kufunga bao moja katika mechi mbili za Kombe la Mapinduzi, lawama ziende kwa washambuliaji wakiongozwa na Abdallah Idd Pina.
Muembe Makumbi iliyokuwa kundi B, imeondoshwa mashindanoni ikiwa na pointi moja iliyoipata mechi ya kwanza dhidi ya Fufuni katika sare ya 1-1, kabla ya kuchapwa 1-0 na Simba.
Kocha wa Muembe Makumbi, Sheha Khamis Rashid, amesema safu yake ya ushambuliaji imemuangusha kutokana na nafasi nyingi zimetengenezwa, lakini wameshindwa kuzitumia.
“Katika ulinzi wamefanya vizuri kidogo angalau, kuruhusu mabao mawili katika mechi mbili ikiwamo moja dhidi ya Simba, sio mbaya.
“Lakini mbele tumetengeneza nafasi nyingi tumeshindwa kuzitumia vizuri. Hili linatufanya tuone kuna sababu ya kuimarisha eneo hilo.
“Hata hivyo, maboresho yameanza na ndio maana tumemsajili Pina ambaye tunaamini atatusaidia katika mechi zijazo za ligi,” amesema Rashid.
Pina aliyetua Muembe Makumbi dirisha dogo akitokea Pamba Jiji ni mzoefu wa ligi ya Zenji kwani msimu uliopita alikuwa mfungaji bora akiichezea Mlandege alipofunga mabao 21.
