MEYA DKT. NICAS ASISITIZA KUKAMILIKA UJENZI WA MATUNDU YA VYOO SHULE YA MSINGI TANDAU

Na Khadija Kalili, Kibaha

MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Mawazo Nicas, leo tarehe 5 Januari 2026 ameendelea na ziara yake kwa kufanya ukaguzi wa ujenzi wa matundu sita ya vyoo katika Shule ya Msingi Tandau iliyopo Kongowe, Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani.

Akiwa katika ziara hiyo amesema kuwa ameridhishwa na hali ya ujenzi na kusisitiza Afisa Utumishi kutoa fedha kiasi cha Mil. 50 ili ujenzi huo ukamilike kabla ya shule kufunguliwa kwa sababu watoto zaidi ya 800 wanahitaji kutumia matundu ya vyoo hivyo.

“Nimeona hali ya ujenzi inaridhisha hivyo naamuru Afisa Utumishi aidhinishe kiasi cha fedha zilizobaki zije kutumika kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa vyoo hivi pamoja na kununua madawati na sitaki kuona mwanafunzi anakaa chini,” amesema Dkt. Nicas.

“Kamilisheni ujenzi wa matundu haya haraka iwezekanavyo ili pindi shule zitakapofunguliwa wanafunzi waweze kutumia kwa sababu uhitaji ni mkubwa,” amesema Dkt. Nicas.

Aidha, Afisa Utumishi wa Manispaa ya Kibaha, Mrisho Mlela, amesema kuwa amepokea maelekezo na fedha hizo zitatoka kesho, tarehe 6 Januari 2026.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Afisa Elimu Kata, Julius Samson, amesema kuwa shule hiyo inakabiliwa na uhaba wa matundu ya vyoo na madawati.

“Natoa shukrani zangu za dhati kwa ziara ya Mheshimiwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha na namna alivyotoa maelekezo kwamba fedha zitoke ili ziweze kutatua changamoto inayotukabili, nasema asante sana,” amesema Kaimu Afisa Elimu Kata, Julius.

Wakati huohuo, Dkt. Nicas amepokea malalamiko ya kuomba kurejeshwa kwa gari la wagonjwa lililochukuliwa na Kituo cha Afya Mkoani huku akiongea kwa simu moja kwa moja na Mganga wa Kituo hicho ambaye amekiri kurudisha gari hilo mara moja.

Pia, Dkt. Nicas amekagua ujenzi wa Kituo cha Afya Kongowe ambapo amekagua upanuzi wa majengo ya upasuaji, wodi ya kuzalisha kina mama na wodi ya watoto njiti, zote zikiwa katika hatua ya kukaribia kukamilika, pia amesisitiza Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Mlela, kutoa fedha kiasi cha Mil. 50 ambazo zitasogeza ujenzi katika hatua fulani kwenye majengo hayo mapya.

Dkt. Bertha Makidika wa Kituo cha Afya Kongowe amesema kuwa makadirio ya ujenzi huo ni Mil. 331 ambapo hivi sasa wanahitaji Mil. 50 ambayo pindi itakapotoka itatumika kukamilisha miundombinu ya maji katika majengo hayo.

Ambapo Meya Dkt. Nicas amesema kuwa amemuelekeza Afisa Utumishi, Mrisho Mlela, kutoa fedha kiasi cha Mil. 50, ambapo Mlela amesema fedha hizo atazitoa jioni tarehe 5 Januari 2026.

Dkt. Makidika amesema kuwa katika kituo hicho wamekuwa wakitoa huduma ya uzalishaji kwa dharura tu na hadi sasa hawajawahi kupata rekodi ya vifo vya wazazi.

“Hivi sasa wajawazito hulazimika kutembea umbali wa kilomita 15 kufuata huduma ya uzazi ambapo hulazimika kwenda Mkoani Kibaha au Mlandizi, hivyo endapo pesa itatoka kwa wakati itasaidia kukamilisha majengo hayo na kupunguza usumbufu kwa kina mama wanaojifungua.”

Dkt. Nicas ameahidi kuwa Manispaa itajitahidi kumalizia majengo hayo.

“Nadhani tukamilishe haraka, tuone tunavyokwenda kwenye bajeti tuipitishe haraka ili majengo yakamilike tupeleke kicheko kwa wananchi,” amesisitiza Dkt. Nicas.

Kadhalika, wakazi wa Kongowe wameomba Manispaa iwajengee soko kwa sababu hivi sasa wanakwenda kuhemea soko la Mlandizi, hoja hiyo imechukuliwa na utekelezaji utafanyika.