Mido ya Kagera yaibukia Mbeya City

MBEYA City inaendelea na maboresho katika dirisha dogo lililofunguliwa kuanzia Januari 1, 2026, ambapo kwa sasa kikosi hicho cha jijini Mbeya kiko kwenye hatua za mwisho za kumsajili kiungo Said Naushad.

Naushad anayeichezea Kagera Sugar inayoshiriki Ligi ya Championship kwa msimu huu, tayari yupo jijini Mbeya kwa ajili ya kukamilisha usajili huo, ambapo mazungumzo ya kutua katika kikosi hicho yamefikia sehemu nzuri kati ya pande hizo mbili.

Mwanaspoti linatambua, baada ya mechi ya juzi ya Championship kati ya KenGold dhidi ya Kagera Sugar iliyopigwa jijini Mbeya, uongozi wa Mbeya City ulikutana na nyota huyo ambapo mazungumzo hayo yameenda vizuri ili kukichezea kikosi hicho.

“Kila kitu kinaenda vizuri kwa ajili ya mchezaji huyo kujiunga na Mbeya City na makubaliano binafsi yamefikiwa tayari, tunaendelea kukamilisha baadhi ya sajili ili kupunguza presha ya kugombania dakika za mwishoni,” kilisema chanzo hicho.

Naushad anaungana na nyota wengine waliowahi kucheza Kagera Sugar katika timu hiyo ya Mbeya City, baada ya Hijjah Shamte aliyekamilisha uhamisho wake wa kujiunga na kikosi hicho akitoka MFK Karvina B ya Jamhuri ya Czech na Omary Chibada.

Nyota wengine wapya katika kikosi hicho kinachonolewa na Kocha, Mecky Maxime ni Abalkassim Suleiman aliyeachana na Pamba Jiji tangu msimu uliopita na aliyekuwa kiungo wa Fountain Gate, Abdallah Kulandana aliyevunja mkataba wake na timu hiyo. 

Mwingine ni aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Yacouba Songne raia wa Burkina Faso, ambaye anakaribia kujiunga na kikosi hicho pia, baada ya msimu wa 2024-2025 kuachana na TRA United zamani Tabora United aliyoifungia mabao manne ya Ligi Kuu.