Mlandege tatizo wachezaji sio kocha

KOCHA msaidizi wa Mlandege, Sabri Ramadhan China amesema wachezaji wa kikosi hicho wameshindwa kuifanya kazi ipasavyo ndiyo sababu ya kuwa timu ya kwanza kuaga mashindano.

Mlandege ambayo ni bingwa mtetezi wa Kombe la Mapinduzi, imeondoshwa kwa aibu kutokana na kupoteza mechi zote tatu za kundi A, ikifunga bao moja na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara sita.

Akizungumza na Mwanaspoti, China amesema wao kama benchi la ufundi walifanya kila kitu katika uwanja wa mazoezi, lakini wachezaji wakashindwa kukiwasilisha siku ya mechi vile inavyotakiwa.

Amesema hiyo pia imechangiwa na aina ya wachezaji waliopo kikosini kwao kwani asilimia kubwa hawana uzoefu wa mashindano mbalimbali.

“Mwaka huu bahati sio ya kwetu, kiukweli niseme inauma sana kwa sababu bingwa mtetezi kutoka awali kama hivi sio kitu kizuri, hatuna cha kufanya, mpira ndio ulivyo. Tutajipanga kwa wakati ujao,” amesema.

“Tatizo sio mbinu kama ingekuwa mbinu tunapokuwa uwanja wa mazoezi tunafanya vya kutosha na kueleweka tatizo ni wachezaji kwa sababu mazoezini wanafanya vizuri, katika mechi inakuwa tofauti.

“Nina wasiwasi kwamba uzoefu pia umetuangusha kwa sababu wapinzani tuliokutana nao wana wachezaji wazoefu sana, sisi hatuna.

“Mlandege iliyobeba Kombe la Mapinduzi 2023 na 2024, msimu huu ilianza kufungwa 3-1 na Singida Black Stars, ikachapwa 1-0 na URA, kisha ikamaliza na kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Azam.