Mzazi fanya haya kila siku kuimarisha elimu ya Mtoto

Januari inapokaribia, wazazi wengi wanaamini kuwa kazi kubwa imeshamalizika baada ya kulipa ada na kununua sare mpya za shule

Hata hivyo, siri ya mafanikio ya mtoto shuleni haipo kwenye ukuta wa madarasa pekee, bali kwenye mazingira yanayotengenezwa nyumbani kila siku.

Ili mwanao afanye vizuri na “anyooke” kimasomo na kitabia, hapa kuna orodha ya mambo muhimu unayopaswa kuyafanya kama mzazi, yatakayorahisisha kazi ya mwalimu na kumpandisha mtoto wako chati.

Kagua madaftari kila siku

Hili ni jambo la dakika 15 tu lakini lina umuhimu wa miaka 100. Unapokagua madaftari, unajua mwanao amefundishwa nini na ameelewa kiasi gani.

Hii inamtuma ujumbe mtoto kuwa “baba na mama wanafuatilia ninachofanya,” hali inayomfanya awe makini zaidi darasani.

Usimfanyie mtoto kazi zake, lakini hakikisha anazifanya. Tenga muda maalum na eneo tulivu la yeye kukaa na kufanya homework.

Hii inajenga nidhamu ya kazi na kumfanya mtoto awe na utaratibu usiobadilika.

Zungumza na mtoto kuhusu siku yake

Badala ya kuuliza “Shule ilikuwaje?” uliza maswali mahususi kama “Leo umejifunza nini kipya?” au “Ni kitu gani kimekuchekesha leo shuleni?”. Hii inajenga uwezo wake wa kuelezea mambo na kukuweka karibu na hisia zake.

Himiza utamaduni wa kusoma

Mtoto anayekuona unasoma gazeti, kitabu, au hata Quran au Biblia, atavutiwa kusoma pia. Tenga muda wa kusoma hadithi pamoja kabla ya kulala. Hii huongeza msamiati wake na uwezo wa kuelewa masomo ya lugha.

Punguza muda wa televisheni na simu

Teknolojia ni nzuri lakini ni adui wa umakini  kama haitadhibitiwa. Hakikisha kuna muda maalum wa kuangalia TV na siyo saa zote. Ubongo wa mtoto unahitaji kupumzika ili uweze kuchakata maarifa mapya.

Weka ratiba ya kulala mapema

Mtoto aliyepata usingizi wa kutosha (saa 8-10) huwa na utulivu na uwezo mkubwa wa kufikiri darasani. Mzazi anayemruhusu mtoto kukesha anaandaa mwanafunzi atakayelala darasani kesho yake.

Fundisha maadili na heshima

Mwalimu asilazimike kutumia nusu saa kufundisha mtoto wako kusema “shikamoo”, “samahani”, au “asante”. Maadili haya yakianzia nyumbani, mwalimu atatumia muda mwingi kufundisha hisabati na sayansi, na siyo kupambana na utovu wa nidhamu.

Chai ya asubuhi ni muhimu sana. Mtoto mwenye njaa hawezi kuelewa masomo. Hakikisha anakula mlo kamili unaompa nguvu na kinga dhidi ya magonjwa yatakayomfanya akose vipindi.

Wasiliana na mwalimu mara kwa mara

Usiwe mzazi wa “kushtukiza” unapoitwa kwa matatizo pekee. Piga simu au tuma ujumbe mfupi kwa mwalimu wa darasa kuuliza maendeleo ya mtoto. Ushirikiano huu unamfanya mwalimu ajisikie anathaminiwa.

Usitamani tu alama za “A”. Mpongeze mtoto anapoonyesha juhudi, anapoboresha mwandiko, au anapopata alama nzuri kuliko mara iliyopita. Hii inamjengea hali ya kujiamini.

Kumbuka, mwalimu ana watoto wengi wa kuwahudumia, lakini wewe unaye mmoja au wachache wa kipekee. Ukitekeleza orodha hii, utakuwa umetoa mchango mkubwa zaidi kuliko ada uliyolipa. Januari hii, anza na mtindo huu mpya, na utaona mabadiliko makubwa kwa mwanao ndani ya muda mfupi.