Hai. Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir amesema Serikali imewekeza kwenye Chuo cha Ufundi Arusha kupitia mradi wa umahiri wa Kikuletwa (EASTRIP) kuwa kitovu cha mafunzo ya nishati jadidifu kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Akizungumza leo, Jumanne Januari 6, 2026 katika kituo hicho kilichopo Kata ya Rundugai, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, amesema kituo hicho cha umahiri ni cha kimkakati kwa lengo la kutoa mafunzo ya vitendo katika uzalishaji wa nishati jadidifu.
Pia, kituo hicho kitawaandaa na kuwapa ujuzi vijana watakaofanya kazi katika miradi mikubwa ya kitaifa na kimataifa ikiwamo Bwawa la Uzalishaji Umeme la Mwalimu Nyerere na kitachochea ushirikiano wa kikanda kwa kupokea wanafunzi na watalaamu kutoka nchi mbalimbali kwa ajili ya mafunzo na tafiti.
“Nimetembelea mradi na kusikia mawasilisho mbalimbali ya utekelezaji wa mradi huu, napenda kutumia fursa hii kuupongeza uongozi na watumishi wa Chuo cha Ufundi Arusha pamoja na uongozi wa Wilaya ya Hai kwa utekelezaji mzuri wa mradi huu utakaoleta tija kwa Taifa letu,” amesema Wanu.
Amesema utaratibu wa chuo hicho kuwahusisha wakufunzi katika ujenzi wa mtambo wa kufua umeme, unajenga uwezo na kuboresha mafunzo kwa wanafunzi.
“Nimefarijika kusikia kuwa chuo kinashiriki katika utekelezaji wa mkakati wa Serikali wa matumizi ya nishati safi kwa kutoa mafunzo kwenye kituo cha Kikuletwa, nahimiza wanafunzi wanaosoma mkondo wa amali kuchagua masomo yanayohusiana na nishati jadidifu kutokana na fursa kubwa zikizopo,” amesema Wanu.
Naibu Waziri huyo ameongeza kuwa ushirikiano uliopo kati ya chuo hicho na viwanda pamoja na taasisi za elimu, sayansi na teknolojia ndani na nje ya nchi utasaidia watumishi na wanafunzi kufanya tafiti zenye kutatua changamoto katika jamii.
Ameongeza kuwa ongezeko la udahili wa wanafunzi uliotokana na ongezeko la mitalaa mipya na mazingira mazuri ya kujifunzia na kufundishia, pia, limechochea ongezeko la wanafunzi wa jinsia ya kike kwenye kozi za ufundi.
Awali, Mkuu wa Chuo cha Ufundi Arusha, Profesa Musa Chacha, akitoa taarifa ya mradi wa kujenga ujuzi na ushirikiano wa kikanda wa Afrika Mashariki (EASTRIP), amesema Kampasi ya Kikuletwa ina ukubwa wa eka 354 ni eneo lililojengwa mitambo ya kufua umeme na wakoloni wa kijerumani mwaka 1930 ikiwa na mitambo miwili na mwaka 1970 Shirika la Umeme (Tanesco) walikabidhiwa kuuendesha mtambo huo.
Amesema mwaka 2013 walikabidhiwa kituo hicho kwa ajili ya kukitumia kwa mafunzo ya nishati jadidifu kwa wanafunzi wao na mtambo huo utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 1.65 katika eneo hilo la Kikuletwa.
“Mradi wa Kujenga Ujuzi na Ushirikiano wa Kikanda wa Afrika Mashariki (EASTRIP) ni wa kimkakati unaotekelezwa katika nchi za Tanzania, Kenya, Ethiopia kupitia mkopo wa masharti nafuu wa Benki ya Dunia (WB) uliidhinishwa Oktoba 2018 na unatarajiwa kukamilika Desemba 2026,” amesema Profesa Chacha.
Amesema chuo hicho kilipatiwa jumla ya Sh46.7 bilioni kujenga kituo hicho ikiwa ni pamoja ujenzi wa madarasa, mabweni na kafteria na utekelezaji wake unakaribia kukamilika.
Profesa Chacha ameongeza mafanikio ya mradi huo ni kuongeza udahili hadi Desemba 2025 jumla ya wanafunzi 3,519 wamepatiwa mafunzo ya nishati jadidifu,pia ununuzi wa vifaa vya kisasa vya kujifunzia na kufundishia.
“Uwepo wa Kituo cha Umahiri wa Kikanda cha mafunzo ya nishati jadidifu utafungua fursa nyingi kwa chuo, kwa jamii ya Kikuletwa na Taifa kwa jumla,” amesema Profesa Chacha
Mkuu wa Wilaya ya Hai, Hassan Bomboko amesema uongozi wa Serikali ya wilaya utaendelea kushirikiana na chuo hicho kufikia malengo yaliyokusudiwa na kuahidi kushirikiana na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) kuboresha barabara inayofika katika kituo hicho.
