Ngowi achaguliwa kuwa diwani Kirua Vunjo Magharibi

Moshi. Msimamizi msaidizi wa uchaguzi wa Kata ya Kirua Vunjo Magharibi, Daniel Maeda amemtangaza Heriel Ngowi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa diwani wa kata hiyo, baada ya kupata kura 3,536 za ‘Ndiyo’ kati ya kura 4,358 zilizopigwa.Uchaguzi huo umefanyika baada ya kusogezwa mbele kufuatia kifo cha aliyekuwa mgombea udiwani kupitia CCM, John Kessy, aliyefariki dunia Oktoba 21, 2025.

Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo hayo Jumatatu, Januari 5, 2026, Maeda amesema jumla ya wapigakura walioandikishwa katika kata hiyo walikuwa 7,790 huku wapigakura 4,358 wakijitokeza kupiga kura.

“Wananchi waliojiandikisha kupiga kura walikuwa 7,790, waliopiga kura ni 4,358, ambapo kura za ‘Ndiyo’ ni 3,536 na kura za ‘Hapana’ ni 699,” amesema Maeda.

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Ngowi amesema ushindi huo ni deni kwa wananchi wa Kirua Vunjo Magharibi, akiahidi kuwatumikia kwa uaminifu na kuhakikisha anapigania maendeleo ya kata hiyo.

“Ninawashukuru wananchi wa Kirua Vunjo Magharibi kwa kuniamini na kunipa nafasi ya kuwatumikia kama diwani.

“Ushindi huu ni deni kwa wananchi na ninaahidi kupigania maendeleo katika sekta za afya, elimu, miundombinu ya barabara pamoja na huduma ya maji,” amesema Ngowi baada ya kutangazwa mshindi.