Pacha mpya inasukwa Singida Black Stars

USAJILI wa mabeki wawili wa kati Singida Black Stars, Abdallah Salum Kheri ‘Sebo’ na Abdulmalik Zakaria umetajwa kuwa unakwenda kuimarisha zaidi eneo hilo baada ya kuonekana kuna shida.

Katika kuimarisha eneo hilo, benchi la ufundi la Singida Black Stars, linaloongozwa kwa sasa na kocha David Ouma katika michuano ya Kombe la Mapinduzi, kuna kitu linafanya.

Ouma amesema wanalazimika kuimarisha eneo hilo kwani ni muhimu katika mpango wa kusaka ushindi kwani huwezi kupata matokeo mazuri kama huna safu nzuri ya ulinzi.

“Tunaimarisha kila eneo kwa sababu kuna wachezaji hatutakuwa nao baada ya dirisha dogo la usajili.

“Tumesajili mabeki wawili wa kati na tunawatumia katika Mapinduzi Cup kuhakikisha wanaelewana kabla ya mashindano mengine yaliyo mbele yetu,” amesema Ouma.

Mabeki hao walipata nafasi ya kucheza pamoja mechi dhidi ya URA iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1. Kabla ya hapo, Sebo alianza na Kennedy Juma walipocheza dhidi ya Mlandege na Singida kushinda 3-1, kisha dhidi ya Azam katika sare ya 1-1, walicheza Kennedy na Abdulmalik.

Mbali na mabeki hao, ndani ya Singida kuna Mukrim Issa ambaye hajaanza mechi yoyote ya Mapinduzi, alitokea benchi mara moja dhidi ya Mlandege.

Inaelezwa kwamba, uamuzi wa Singida kuwasajili Abdulmalick kutoka Mashujaa na Sebo aliyetokea Pamba Jiji, ni sehemu ya kuimarisha eneo la beki wa kati huku Anthony Tra Bi akitajwa kuondoka kipindi hiki na sasa hayupo na timu Zanzibar.