Rais Samia kuzindua jengo la utawala Taasisi ya Sayansi za Bahari

Unguja. Katika utekelezaji wa ajenda ya kuimarisha miundombinu ya elimu ya juu, Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua jengo la taaluma, utawala na bweni katika Taasisi ya Sayansi za Bahari (IMS), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Zanzibar.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Januari 6, 2026, Unguja, Zanzibar, Makamu Mkuu  wa chuo hicho, Profesa William Anangisye amesema jengo hilo litakalozinduliwa na Rais Samia Januari 8, 2025, ni hatua ya kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

“Ujenzi wa majengo haya ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) ambazo ni jitihada za Serikali katika kuleta mageuzi ya uchumi hususani katika maeneo ya sayansi za bahari na uchumi wa Buluu,” amesema Profesa Nangisye.

Amesema majengo yanayozinduliwa yapo kwenye eneo lenye ukubwa wa hekta 50.24.

Profesa  Anangisye amesema katika mradi huo uliogharimu Sh11 bilioni, mkataba wa ujenzi wake ulisainiwa Februari 22, 2024, ambapo ujenzi huo unatekelezwa na Kampuni ya Till Construction Ltd akisimamiwa na Geometry  Consulting Ltd.

Kwa upande wa mikataba ya ungaji wa samani katika majengo hayo, ulisainiwa Novemba 2025 na Kampuni ya Jaffery Ind Sain Ltd inaendelea na kazi za ufungaji wa thamani kwa gharama ya Sh746.785 milioni.

Amesema jengo la taaluma na utawala lina miundombinu ya kisasa inayojumuisha vyumba 41 vya ofisi, vyenye uwezo wa kuhudumia zaidi ya wafanyakazi 80, madarasa 10 yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 300 kwa wakati mmoja.

“Maabara tano za kisasa za kufundisha na utafiti zenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 114 kwa wakati mmoja, chumba cha kompyuta chenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 35, ukumbi wa mikutano wenye uwezo wa kuhudumia watu 150  na bweni la wanafunzi lenye vitanda 40 litakaloboresha upatikanaji wa huduma za makazi,” amesema.

Amesema maabara hizo zinajumuisha kemia ya bahari, bailojia ya bahari, fizikia ya bahari, microbiology na biotechnology  pamoja na maabara ya vifaa maalumu, zitakazowezesha tafiti za hali ya juu zinazohusiana na rasimali za baharini, mazingira ya pwani, mabadiliko ya tabianchi na ubunifu wa bidhaa zitokanazo na mazao ya baharini.

Profesa Anangisye amesema kupitia mradi wa HEET taasisi ya Sayansi za Bahari itaongeza na kuboresha utoaji wa programu za cheti.

Amesema pia itachochea tafiti bunifu na matumizi ya matokeo ya utafiti katika maendeleo ya Taifa, kukuza ujasiriamali unaotokana na rasimali za bahari ikiwamo kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao ya bahari kama mwani na kuimarisha utalii.

Profesa William Anangisye amesema wakati wa utekelezaji wa mradi huo, jamii inayozunguka eneo la Buyu imenufaika kwa kupata ajira 1,457 pamoja na fursa za kiuchumi kupitia biashara ndogondogo na usambazaji wa chakula na malighafi.

Mkurugenzi wa IMS, Dk Mwita Mangora amesema baada ya miundombinu hii kukamilika, wanatarajia kuona mabadililo makubwa katika taaluma nyanja za bahari.

“Tunataka kiwe chuo jumuishi, tunaenda kuanzisha shahada ya uvuvi wa bahari, shahada ya sayansi za bahari na utalii wa kimazingira,” amesema.