Dar es Salaam.Uhaba wa samaki katika Soko la Kimataifa la Samaki la Feri jijini Dar es Salaam, umejitokeza kufuatia hali ya hewa ya upepo mkali baharini uliosababisha hata bei ya kitoweo hicho hususan dagaa mchele, kupanda bei.
Jana, Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac) ilitoa tahadhari kwa wavuvi na wasafirishaji wa majini kuchukua hatua za tahadhari kutokana na upepo mkali na mawimbi makubwa katika Bahari ya Hindi kuanzia Januari 5 hadi 8, 2026.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi leo Jumanne Januari 6, 2026 katika soko hilo, umebaini samaki ni adimu na kusababisha wachuuzi wengi wa rejareja kukaa kwa muda mrefu bila kupata bidhaa.
Baadhi yao wameonekana wakisubiri bila mafanikio, huku samaki wachache waliopatikana wakigombewa kwa bei ya juu.
Kwa mujibu wa wavuvi, ndoo moja ya dagaa mchele yenye ujazo wa lita 20 iliyokuwa ikiuzwa kati ya Sh40,000 hadi Sh50,000 awali, sasa inauzwa kati ya Sh200,000 hadi Sh250,000 kutokana na ugumu wa kuvua samaki baharini.
Baadhi ya wafanyabiashara wakiwa wamepumzika katika Soko la Feri wakisubiria samaki leo Jumanne Januari 6, 2026.
Mmoja wa wavuvi sokoni hapo, Hamis Mjanga amesema hali ya hewa imewaathiri moja kwa moja kwa sababu wengi wao wamelazimika kusitisha shughuli za uvuvi.
“Januari ni mwezi wenye mahitaji mengi kama ada za shule, kodi za nyumba na tozo mbalimbali. Inakuwa ngumu kupata kipato wakati samaki hawapatikani au wanapatikana kwa gharama kubwa,” amesema Mjanga.
Ametoa wito kwa Serikali kujenga viwanda vingi vya kuchakata na kuhifadhi samaki ili kuwezesha upatikanaji wa bidhaa hiyo hata nyakati za hali mbaya ya hewa.
Naye Mwenyekiti wa Wavuvi wa ‘Zone One’, Seif Abdulrahman, amesema wamewashauri wavuvi kupumzika kwa kipindi hiki kwa kuzingatia tahadhari zilizotolewa na mamlaka husika.
Amesema samaki wanaouzwa kwa sasa wengi ni wale waliokuwa wamehifadhiwa kwenye friji, hali inayochangia kupanda kwa bei.
Kwa upande wake, mfanyabiashara wa dagaa kwa bei ya rejareja kutoka Mwananyamala, Mwanahawa Yusufu amesema hali hiyo imewaathiri wafanyabiashara wadogo.
“Kawaida nikifika sokoni asubuhi haipiti saa moja napata ninachohitaji, lakini leo hadi saa sita sijapata chochote. Tunajikuta tukinunua samamki au dagaa mchele kwa mafungu madogo madogo ilimradi urudi nyumbani na kitu,” amesema.
Mkazi wa Mmbande, Zuhura Abdallah amesema wameanza kupunguza mafungu ya dagaa mchele wanayowauzia wateja wao kutokana na bei kupanda, hali inayosababisha malalamiko, lakini hana budi kufafanua sababu kwa wateja wake.
Akizungumzia hali hiyo, Ofisa Uvuvi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam katika Soko la Samaki Feri, Livinus Butimbe amesema upungufu wa samaki unatokana na msimu wa upepo wa Kaskazi unaoambatana na mawimbi makali.
“Mawimbi yanapokuwa makali, wavuvi wachache huenda kuvua na hata wanaoenda uwezo wao wa kuvua samaki hupungua,” amesema.
Ameongeza kuwa ingawa kuna vyanzo vingine vya samaki, asilimia kubwa ya mahitaji hutegemea wavuvi wa kila siku, hasa kwa dagaa mchele.
Ameunga mkono wazo la kuanzishwa kwa hifadhi ya samaki, akieleza kuwa wakati mwingine dagaa hufika hadi Sh5,000 kwa ndoo, bei ambayo ingewezesha kununuliwa kwa wingi na kuhifadhiwa kwa matumizi ya baadaye.
Butimbe amesema soko hilo lina mpango wa kuongeza vifaa vya ubaridi kwa ajili ya kuhifadhi samaki. Amesema kwa sasa wanamiliki makontena ya ubaridi yasiyozidi matano.
Usafiri wa majini waendelea
Wakati huo huo, usafiri wa abiria kwa vyombo vya majini unaendelea kama kawaida licha ya tahadhari ya hali ya hewa.
Meneja wa Kampuni ya Flying Horse, Abubakar Daud amesema safari zao kati ya Dar es Salaam na Zanzibar zinaendelea bila athari zozote, huku wakizingatia mawasiliano ya karibu na mamlaka.
Meneja Masoko wa Zan Fast Ferries, Sudi Hamis amesema wamekuwa wakipokea simu nyingi kutoka kwa wateja wakitaka kujua hali ya usafiri, lakini amewahakikishia kuwa huduma zinaendelea kwa kuzingatia usalama na kutokuzidisha idadi ya abiria.
Kwa upande wa Azam Marine, mmoja wa wafanyakazi amesema huduma zao pia zinaendelea kama kawaida.
Vivuko vinavyofanya safari kati ya Kivukoni na Kigamboni, vikiwamo vya Azam na cha Serikali cha MV Kazi, pia vimeendelea kutoa huduma.
Baadhi ya wananchi wameipongeza Serikali na mamlaka kwa kutoa tahadhari mapema.
Mkazi wa Kigamboni, Nusura Haji, amesema hatua hiyo imewasaidia wananchi kufanya uamuzi sahihi kuhusu safari zao kulingana na umuhimu na hali ya usalama.
