Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga, amesema Serikali imejidhatiti kuhakikisha inafufua viwanda vilivyopo mkoani Tanga, kufuatia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alilolitoa wakati wa ziara yake mkoani humo likiwa na Lengo ni kurejesha hadhi ya Tanga kuwa mkoa wa viwanda kama ilivyokuwa awali.
Akizungumza kuhusu utekelezaji wa agizo hilo Januari 6, 2026, Waziri Kapinga amesema wizara yake kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa wa Tanga imeanza majadiliano ya kina ya kufufua viwanda 18 vya awali, vikiwemo vilivyobinafsishwa na Serikali na vile vya binafsi, majadiliano hayo yamezingatia changamoto za jumla na za binafsi zinazokikabili kila kiwanda ili kuweka mikakati madhubuti ya urejeshwaji.
Waziri Kapinga pia amesema jitihada hizo tayari zinaanza kuzaa matunda, akitolea mfano Kiwanda cha African Hamon ambacho kilikuwa hakifanyi kazi kabisa lakini sasa kimeanza kufanya kazi, kiwanda hicho tayari kimeajiri zaidi ya vijana 200 kwa ajira za kudumu, jambo linalosaidia kuongeza ajira miongoni mwa vijana wa Tanga.
Amesisitiza kuwa lengo la wizara ni kuhakikisha viwanda vyote vilivyolengwa vinaanza kufanya kazi kikamilifu, ili kuimarisha soko la ndani na nje ya nchi kupitia bidhaa zinazozalishwa hapa Tanzania.
Serikali pia itaweka mwakilishi katika kila kiwanda ili kusaidia kurahisisha utatuzi wa changamoto za wawekezaji na kuhakikisha kipaumbele kinatolewa kwa haraka.
Aidha, Waziri Kapinga amesema juhudi hizi zinaendana na maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda, huku viwanda hivyo vikichangia moja kwa moja kuboresha maisha ya wananchi kupitia ajira za uhakika, Mpango huo umeelezwa wazi katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025–2030 na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050, inayolenga kukuza uchumi wa viwanda na maendeleo endelevu.
Akizungumza Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Dkt. Batilda Burian, amesema kwamba kilio cha muda mrefu cha mkoa huo kilikuwa ni viwanda, kwani awali vilibaki kama magofu, Sasa wanafurahi kuona viwanda vikifufuliwa na ameahidi kuendelea kufuatilia ili kufungua viwanda vipya kila wilaya.
Aidha, amesema Serikali itasisitiza kuhakikisha Tanga inakuwa mkoa wa viwanda, Pia ameitaka serikali kuongeza gati ya pili bandarini ili kurahisisha huduma za meli nyingi kutua bandarini, huku wakitarajia kufanya mkutano mkubwa wa kunadi fursa zilizopo mkoani humo.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Tanga Mjini Kassimu Mbaraka, amesema sasa wananchi wa Tanga wanakwenda kunufaika na uwepo wa fursa kutokana na uwepo wa viwanda hivyo, amewahimiza wananchi kuchangamkia fursa hizo na wamiliki wa viwanda ambavyo havijafufuliwa kushirikiana na mamlaka husika kuhakikisha viwanda vyote vinaweza kufanya kazi.









