Mwanza. Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dk Pius Chaya amewataka wawekezaji wote nchini kuajiri wataalamu wa ndani kutoka vyuo vikuu ili kuvuna ujuzi endelevu.
Amebainisha kwamba kwamba Serikali haitamani kuona uwekezaji uliopo nchini unakufa, kushindwa kuendelea na kusimama pale wawekezaji watakapoiacha.
Dk Chaya ameitaka Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (Tiseza) kusimamia utekelezaji huo kwa kuhakikisha wawekezaji wote waliosajiliwa wanatekeleza agizo hilo, ikiwamo kuajiri Watanzania wenye ujuzi walio na elimu ya darasa la saba na kidato cha nne.
Naibu Waziri huyo amebainisha hayo leo Jumanne Januari 6, 2025 alipokagua maeneo ya uwekezaji mkoani Mwanza ikiwamo kiwanda cha kuzalisha chakula cha kuku, samaki na mafuta ya soya cha Rofi Farming pamoja na kiwanda cha kuzalisha nondo, misumari na nyaya cha Ziwa Steel vilivyopo Magu.
Viwanda hivyo kwa jumla vimetengeneza ajira Watanzania zaidi ya 950 wenye utaalamu na wasio na utaalamu katika fani za utawala, uhasibu, uzalishaji na vibarua.
Amesisitiza kuwa Serikali inatamani kuona uwekezaji wa aina hiyo unaendelea, lakini usipokuwa na wataalamu wenye sifa ambao watapata ufahamu kutoka kwa wawekezaji wa nje, itakuwa vigumu kuiendeleza miradi hiyo.
Amesema wizara yake itasimamia kuhakikisha wawekezaji wote ambao wamesajiliwa kupitia Tiseza wanawafuatiliwa ili waajiri vijana wenye sifa ili waimudu na kuielewa miradi, hata pale inapotokea wawekezaji wameondoka na kuachia mradi, nchi iwe na vijana ambao wataweza kuisimamia vyema.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Dk Pius Chaya akikagua misumari inayozalishwa na mwekezaji Ziwa Steel wilayani Magu Mkoa wa Mwanza. Picha na Damian Masyenene
“Na hii iwe kwa wawekezaji wote Tanzania, nimefika kwenye maeneo haya ya uwekezaji wamejitahidi kutoa ajira kwa vijana wenye shahada katika maeneo ya sheria, utawala na uhasibu, lakini kule kwenye uzalishaji ambako ndiko kwenye injini ya uzalishaji, tunategemea kuwa na watu ambao wamesomea haya mambo,” amesema Dk Chaya.
“Kuna vyuo vyetu vinafundisha vijana katika hizi taaluma za ufugaji wa samaki kama Chuo cha Kilimo Sokoine (Sua), Udsm (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam) na vingine. Naomba Tiseza mlisimamie hili, tunahitaji vijana wa kidato cha nne, darasa la saba na wale ambao wana taaluma.”
Amevipongeza viwanda hivyo viwili hasa Ziwa Steel ambacho mwekezaji wake ni mzawa, amesema vimewekeza jumla ya Sh84 bilioni, huku akivihakikishia kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ikiwemo miundombinu ya barabara, umeme na maji ili iongeze uzalishaji na kutoa ajira kwa Watanzania.
“Serikali imejikita katika kukuza uchumi ili ulete ajira zenye tija, tunapopata wawekezaji kama hawa wenye uwezo wa kuzalisha ajira nyingi kwa Watanzania, lazima tuwaunge mkono. Hivyo, tutaendelea kuwaunga mkono ili uwekezaji wao uwe na tija na endelevu, hatutegemei kuona uwekezaji kama huu unasimama,” amesema Dk Chaya.
Mwakilishi wa Kiwanda cha Rofi Farming, Neziah Mussa amesema licha ya uwekezaji wa Sh19 bilioni uliofanyika, bado hakuna soko la uhakika na kukosa baadhi ya malighafi ikiwemo soya ambayo wanauziwa bei ya juu Sh2,200 hadi 2,500 kwa kilo moja huku uwezo wao ukiwa ni kununua kwa Sh1,500.
“Tunahitaji msaada wa Serikali ikiwamo usaidizi wa kisera tuwe na mtandao wa wafugaji wa samaki Kanda ya Ziwa ili kurahisisha kupata soko la uhakika. Pia, kuondoa mlolongo mrefu katika kupata vibali, kwani umekuwa ukichelewa mwekezaji kuanza uzalishaji,” amesema Neziah.
Naye, Philip Sylivanus kutoka Ziwa Steel ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini na kuvutia wawekezaji wa nje, ambapo kutokana na mazingira rafiki yaliyopo nchini, kampuni yao imeshinda zabuni ya Sh30 bilioni ya kusambaza nondo, misumari na nyaya nchini Rwanda katika ujenzi wa uwanja wa ndege wa Bugesera.
Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Johari Samizi amesema mkoa huo unaendelea kufanya mazungumzo na mikoa ya nyanda za juu kusini inakozalishwa soya kwa wingi ili kupata malighafi ya kutosha kwa ajili ya wawekezaji wa kuzalisha mafuta ya soya.
“Malighafi ya soya imekuwa ni changamoto, tumeona tumesikia na mkoa umeanza kufanya mawasiliano na mikoa inayozalisha zao hili, nitoe rai kwa wazalishaji wa soya nchini waone hii fursa kwa sababu inafika wakati viwanda vyetu vinasimama,” amesema Samizi.