Shahidi aeleza mashine zilivyokutwa yadi kesi ya mafuta TPA

Dar es Salaam. Shahidi wa tano wa upande wa Jamhuri katika kesi ya wizi wa mafuta na uharibifu wa bomba la mafuta, ameieleza mahakama kuwa alikuta mashine mbili za kuchimbia mafuta aina ya Honda ndani ya yadi iliyodaiwa kuhusishwa na gari lililotiliwa shaka na polisi.

Shahidi huyo, Mrakibu wa Polisi Godfrey Lumbage, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo, Jumanne Januari 6, 2026, wakati anatoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Beda Nyaki.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Monica Matwe, Lumbage amedai kuwa mwaka 2021 alikuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kigamboni na kwamba Mei 31, 2021, alipigiwa simu na askari Mgaya aliyemweleza kuhusu gari lililotiliwa shaka, likitokea eneo la Maweni kuelekea barabara ya Kosota na kuishia ndani ya yadi ya Ungindoni.

Ameeleza kuwa dereva alikimbia baada ya kuegesha gari hilo ndani ya yadi isiyo na mtu.

“Nilivyopata taarifa hizo, nilimfahamisha mkuu wangu wa kazi, SSP Thobias Wale, kisha nilienda eneo la Maweni ambapo nilikuta viongozi wengine wa polisi, akiwemo Mkuu wa Upelelezi wa Kanda aitwaye Shila, na niliamriwa kuanza upelelezi,” amedai Lumbage.

Amedai kuwa katika yadi ya Maweni walikuta vifaa mbalimbali, ikiwemo pampu za Honda, pampu ya kuvutia maji, visu vitatu vya kupekechea ardhi, mtambo mkubwa wa kuchimba kisima, mabomba vipande 25 na mipira miwili ya kupitishia mafuta. Shahidi alikukusanya vielelezo hivyo na aliita mashahidi huru.

Ameeleza kuwa uchunguzi wa awali ulibaini mmiliki wa yadi hiyo aliitwa Nuru. Baada ya hapo, alienda yadi ya Ungindoni ambapo alikuta magari makubwa zaidi ya matano aina ya How na vitu vingine vilivyokamatwa.

Amebainisha kuwa uchunguzi ulionesha mmiliki wa yadi ya Ungindoni aliitwa Dida na wamiliki wa yadi hizo mbili walikamatwa ili kueleza kuhusu watu waliowapangisha.

Kesi hiyo inamkabili aliyekuwa dereva wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Tino Ndeketa (45), na wenzake saba, wakiwemo Fikiri Kidevu (33), Amani Yamba (53), Mselem Abdallah (44), Kila Sangiti (30) maarufu kama Mudy Mzeze, Twaha Salumu (47) maarufu Mwarabu, Gaudence Shayo na Hamis Hamis (49), mkazi wa Kigamboni.

Kesi imeahirishwa hadi kesho kwa usikilizwaji zaidi wa ushahidi wa upande wa Jamhuri.

Washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na kukabiliwa na shtaka la kutakatisha fedha, ambalo halina dhamana.

Washtakiwa wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 30189 ya mwaka 2024, yenye mashtaka manne yakiwemo kuharibu miundombinu, kutakatisha fedha na wizi wa mafuta yenye thamani ya Sh33.9 milioni mali ya Mamlaka ya Bandari Tanzania( TPA).

Mashtaka mawili kati ya hayo ni ya uharibifu wa mali, yaliyotenda kati ya Januari 1, 2019, na Desemba 31, 2022, eneo la Tungi, Kigamboni, ambapo waliharibu bomba la kusafirishia mafuta aina ya Petroli na Dizel mali ya TPA.

Pia wanadaiwa kuwa kati ya Januari mosi, 2020, na Desemba 31, 2020, wanadaiwa kuiba lita 16,225 za mafuta ya dizel yenye thamani ya Sh33.9 milioni mali ya TPA. Siku hiyo hiyo, wanadaiwa pia kutakatisha fedha kiasi cha Sh33.9 milioni, wakijua zinatokana na kosa la wizi.

Washtakiwa hao kwa mara ya kwanza walifikishwa mahakamani hapo Oktoba 22, 2024, na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi.