TFF, Gamondi waitana mezani | Mwanaspoti

BAADA ya kuifikisha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars katika hatua ya 16 Bora ya michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) 2025 akiwa kama kocha wa mpito, Miguel Gamondi ameitwa haraka mezani kusaini mkataba wa kuinoa timu hiyo inayotarajiwa kurejea nchini leo na ikiandaliwa mapokezi makubwa ya kitaifa.

Gamondi ameiongoza timu hiyo katika mechi nne za michuano hiyo akiwa kama Kaimu kocha mkuu baada ya kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na kocha Hemed Suleiman ‘Morocco’ aliyeipeleka Morocco,  ambako imetoka sare mbili dhidi ya Uganda na Tunisia na kupoteza mbele ya Nigeria na ile ya juzi ya 16-Bora dhidi ya wenyeji Morocco.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilimpa Gamondi timu hiyo ya taifa akitokea klabu ya Singida Black Stars aliyojiunga nayo msimu huu na kuiwezesha kutwaa ubingwa wa Kombe la Kagame 2025, lakini akiwa na rekodi tamu wakati anaifundisha Yanga kwa misimu miwili kabla ya kutimuliwa mwishoni mwa mwaka juzi.

GAMO 01

Chanzo cha kuaminika kutoka kwa rafiki wa karibu wa kocha huyo raia wa Argentina, kimeliambia Mwanaspoti kuwa kocha ameanza mazungumzo na TFF kwa ajili ya kusaini mkataba wa kuwa kocha mkuu rasmi.

“Ni kweli TFF wameanza mazungumzo na Gamondi ambaye licha ya kuitaka nafasi hiyo ametoa mapendekezo yake kuwa yupo tayari, lakini anatakiwa kupewa ruhusa ya kuendelea kufundisha timu nyingine yoyote,” kilisema chanzo hicho na kuongeza; “Gamondi amesema kufundisha timu ya taifa ni kwa misimu kutokana na kalenda ya FIFA hivyo kwa kuwa ameshazoea kufundisha anaomba kupewa nafasi ya kufanya majukumu yake akiwa na timu nyingine.”

Kocha huyo ambaye bado ana mkataba na Singida Black Stars aliyojiunga nayo mwanzoni mwa msimu huu, tayari amepewa majukumu mengine na waajiri wake hao.

GAMO 02

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Bodi ya Wakurugenzi ya Singida Black Stars, wamefanya mabadiliko ya kiufundi katika benchi lao ambapo aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, yaani Gamondi amekuwa mkurugenzi wa ufundi wa klabu.

Pia imemwajiri Othmen Najjar kuwa meneja mkuu wa timu, imembadilishia majukumu Ramadhani Nsanzurwimo, aliyekuwa mkurugenzi wa ufundi na kumteua kuwa mshauri wa ufundi wa klabu.

Meneja Mkuu wa timu atafanya kazi kwa karibu na kocha mkuu mpya, David Ouma, akishirikiana na makocha wasaidizi Mousa Nd’aw na Muhibu Kanu.

GAMO 03

Aidha, klabu haina pingamizi lolote kwa kocha Gamondi kuteuliwa kuwa kocha mkuu wa kudumu wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, endapo mamlaka husika zitaona inafaa.

Watumishi wengine ambao hawajatajwa katika taarifa hii wanaendelea kutekeleza majukumu yao kama kawaida ndani ya benchi la ufundi.

Mabadiliko hayo yanaanza mara moja na yamefanyika kwa lengo la kuongeza ufanisi wa kiufundi katika kipindi hiki ambacho timu inashiriki mashindano ya kitaifa na kimataifa.