Dodoma. Katika hatua inayotajwa kuwa mwanga mpya kwa vijana wanaokabiliwa na changamoto za afya ya akili, Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) kimezindua mradi wa TevuAfya, unaolenga kushughulikia kwa vitendo matatizo ya afya ya akili miongoni mwa vijana, hususan wanaoishi mijini na pembezoni mwa miji.
Akizungumza leo Jumanne, Januari 6, 2026, wakati wa uzinduzi wa mradi huo, Makamu Mkuu wa UDOM, Profesa Lughano Kusiluka, amesema kuimarisha afya ya akili kwa vijana ni jambo la msingi na nguzo muhimu ya kufanikisha maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi katika dunia ya sasa inayobadilika kwa kasi.
Profesa Kusiluka amesema vijana ni rasilimali muhimu kwa taifa, hivyo changamoto za afya ya akili wanazokabiliana nazo zinahitaji kushughulikiwa kwa njia bunifu na shirikishi.
Amebainisha kuwa mradi wa TevuAfya umebuniwa mahsusi kusaidia vijana kupata msaada wa kitaalamu, elimu na mifumo rafiki ya kukabiliana na changamoto za kisaikolojia zinazowakumba katika maisha ya kila siku.
Akizungumza katika tukio lililowakutanisha wadau wa elimu, wataalamu na vijana, Profesa Kusiluka amesema maendeleo ya teknolojia ya kidijitali yameleta fursa nyingi kwa vijana, ikiwemo upatikanaji wa maarifa, mawasiliano ya haraka na ubunifu wa kiuchumi.
Hata hivyo, amesema maendeleo hayo yameambatana pia na ongezeko la changamoto za kijamii na shinikizo la kisaikolojia, hususan katika mazingira ya mijini na taasisi za elimu ya juu.
Baadhi ya washiriki wa mradi mpya TevuAfya, unaolenga kushughulikia kwa vitendo matatizo ya afya ya akili kwa vijana wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi.
Ameeleza kuwa tafiti mbalimbali zinaonesha kuongezeka kwa changamoto za afya ya akili miongoni mwa vijana, zikiwemo msongo wa mawazo, wasiwasi, unyogovu na hali ya kukosa matumaini, hali inayochangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo ukosefu wa ajira, mzigo wa masomo, mabadiliko ya mifumo ya kifamilia pamoja na matumizi yasiyodhibitiwa ya teknolojia ya kidijitali.
Kwa mujibu wa Profesa Kusiluka, mradi wa TevuAfya unatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kuimarisha ustawi wa vijana kwa kutoa elimu, ushauri na mifumo ya msaada inayolenga kujenga jamii yenye afya bora ya akili, akisisitiza kuwa afya ya akili ni msingi wa uzalishaji, ubunifu na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
“Hata hivyo, hili si simulizi la kukata tamaa, ni simulizi la matumaini pale mifumo jumuishi ya msaada inapowekwa; ikihusisha taasisi za elimu, familia, jamii na watunga sera, vijana hujenga ustahimilivu na kuimarisha afya yao ya akili,” amesema Profesa Kusiluka.
Ameongeza kuwa elimu sahihi, mazungumzo ya wazi na upatikanaji wa huduma rafiki za afya ya akili ni miongoni mwa nyenzo muhimu katika kukabiliana na changamoto hizo.
Kwa upande wa wanafunzi, Akley Omary wa UDOM amesema wanafunzi wengi hukumbwa na msongo wa mawazo unaotokana na changamoto za kifedha, matatizo ya kifamilia na mazingira magumu ya masomo, huku kukosa mahitaji muhimu kama chakula, vifaa vya masomo na fedha za matumizi vikizidi kuathiri ustawi wao wa kisaikolojia.
Kwa upande wake, Rebeca Kabanda, mwanafunzi wa Information Security Engineering, amesema ukosefu wa ajira ni moja ya changamoto kubwa zinazowaathiri vijana kisaikolojia, hasa pale matarajio ya maisha baada ya kuhitimu yanapogonga mwamba.
Amesema kuwa matumizi sahihi ya Tehama na mitandao ya kijamii yanaweza kuwa nyenzo muhimu ya kutoa elimu na msaada wa kisaikolojia kwa vijana, akisisitiza umuhimu wa kujiepusha na tabia hatarishi na mahusiano yasiyo rasmi yanayoweza kuathiri afya ya akili na maendeleo ya kielimu.
Mradi wa TevuAfya unatarajiwa kutoa mapendekezo ya kisera pamoja na mbinu za vitendo zitakazosaidia kuboresha afya ya akili kwa vijana na kuimarisha ustawi wa jamii kwa ujumla, hatua inayotajwa kuwa muhimu katika kujenga taifa lenye vijana wenye afya njema ya mwili na akili.