Uganda yatoa kongole utekelezaji bomba la mafuta ghafi

Tanga. Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda, Dk Ruth Nankabirwa ameipongeza Tanzania kwa hatua kubwa iliyofikiwa katika utekelezaji wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP).

Mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda.

Dk Nankabirwa ametoa pongezi hizo leo Jumanne, Januari 6, 2026 jijini Tanga, wakati wa ziara yake ya kikazi akiongozana na ujumbe kutoka Uganda waliotembelea eneo la Chongoleani mkoani Tanga, ambako ujenzi wa mradi huo unaendelea.

Dk Nankabirwa amesema ameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo unaotarajiwa kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi, ajira na maendeleo kwa Tanzania, Uganda na ukanda mzima wa Afrika Mashariki.

Hivyo, ameziagiza Wizara za Nishati za nchi hizo mbili kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika ili shughuli zote za utekelezaji wa mradi ziendelee bila kukwama.

Ameongeza kuwa mradi wa EACOP ni miongoni mwa miradi mikubwa duniani na barani Afrika, hivyo wananchi wa pande zote mbili wana sababu ya kujivunia mafanikio yanayopatikana, yakiongozwa na dhamira ya dhati ya marais wa Tanzania na Uganda.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati wa Tanzania, Salome Makamba amesema dhamira ya dhati ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni imewezesha utekelezaji mzuri wa mradi huo unaotarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika nyanja za kiuchumi, kijamii, ajira pamoja na uboreshaji wa huduma za jamii.

Makamba ameipongeza Kampuni ya EACOP kwa kazi kubwa inayoendelea na kuitaka kuendelea kutoa fursa za ajira na zabuni kwa kampuni na wazawa wa Tanzania na Uganda, kama ilivyoainishwa katika mkataba wa utekelezaji wa mradi huo.

Awali, kabla ya kutembelea eneo la mradi, ujumbe wa Waziri wa Uganda na ujumbe wa Tanzania ulioongozwa na Naibu Waziri wa Nishati walitembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa huo, Balozi Dk Batilda Buriani.

Dk Buriani amesema Mkoa wa Tanga umenufaika kwa kiasi kikubwa na uwepo wa mradi wa EACOP, hususan katika kutoa ajira kwa vijana wa maeneo yanayopitiwa na bomba, pamoja na kuboreshwa kwa huduma za kijamii ikiwemo maji, umeme na miundombinu mingine.

Ameipongeza Kampuni ya EACOP kwa kuzingatia masuala ya utunzaji wa mazingira, bayoanuai na usalama katika kipindi chote cha utekelezaji wa mradi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Mradi huo ulianza kutekelezwa mwaka 2022 na unatarajiwa kukamilika Julai mwaka huu. Mradi huo unahusisha ujenzi wa vituo viwili vya kupunguza msukumo wa mafuta, vituo sita vya kuongeza msukumo wa mafuta, pamoja na ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta kutoka Uganda hadi Bandari ya Tanga.

Katika ziara hiyo, ujumbe wa pande zote mbili ulitembelea pia eneo la gati la kuegesha meli kwa ajili ya upakiaji wa mafuta, matenki ya kuhifadhia mafuta ghafi pamoja na miundombinu yake.