MABINGWA wa Kombe la Mapinduzi mwaka 2016, timu ya URA, imekubali ushindani iliokutana nao msimu huu katika michuano hiyo imewapa funzo na kuahidi wakati ujao itaondoka na kombe.
Hayo yamesemwa na kocha msaidizi wa kikosi hicho kutokea Uganda, Ssemuyaba Bashiru aliposema kundi A walilokuwepo halikuwa rahisi kutokana na kukutana na timu zenye ushindani, hivyo wanakwenda kujipanga zaidi.
URA ilianza mashindano kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mlandege, kisha sare ya 1-1 dhidi ya Singida Black Stars, kisha kichapo cha 2-1 kutoka kwa Azam na kumaliza nafasi ya tatu ikikusanya pointi nne. Azam ni kinara iliyomaliza na pointi saba ikifuatiwa na Singida (5), huku Mlandege ikiburuza mkia haina kitu.
“Ushindani ulikuwa mkubwa sana, ukiangalia kila mechi tuliyocheza ilikuwa ngumu kupata matokeo ya ushindi. Ile ya kwanza tulicheza siku chache baada ya kufika hapa, kisha zikaja mechi mfululizo zinazokunyima muda mwingi wa maandalizi.
“Lakini tunashukuru tumetumia mashindano haya kuwatambulisha wachezaji wetu vijana na tunaamini tunaporejea nyumbani tutafanya vizuri katika Ligi Kuu.
“Safari yetu katika Kombe la Mapinduzi mwaka huu imefika mwisho, lakini Mungu akipenda tutarudi tena mwakani na kuondoka na kombe kama ilivyokuwa mwaka 2016,” amesema kocha huyo.
URA ilipobeba ubingwa huo mwaka 2016, fainali iliichapa Mtibwa Sugar mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Amaan, Unguja.
