Arusha. Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir ameielekeza Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) kupanua wigo wa uandaaji wa wakufunzi na walimu tarajali wa mafunzo ya amali kwa ajili ya shule za sekondari na vyuo vya ufundi stadi.
Amesema kuna fursa muhimu ya kufundisha mafunzo ya amani kwa wakufunzi tarajali ikiwamo yanayohusu ukarimu na utalii nchini.
Naibu Waziri huyo ametoa maagizo hayo jana Jumatatu Januari 5, 2026 alipokagua Chuo cha Veta cha Mafunzo ya Hoteli na Utalii (VHTTI), kilichopo eneo la Njiro jijini Arusha.
Amesema maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023, yameainisha msisitizo kwenye elimu ya ujuzi, kwenye ngazi zote kuanzia elimu ya msingi kwa maana ya mafunzo ya amali kwa shule za msingi na sekondari.
Amesema chuo hicho kina mchango katika kuandaa rasilimali watu wa kutosha inayokidhi mahitaji ya soko la ajira kwenye sekta hiyo ya muhimu nchini.
“Sambamba na hilo nimeona kuna fursa muhimu ya kufundisha mafunzo ya amali kwa wakufunzi tarajali yanayohusu ukarimu na utalii nchini. Kutokana na umuhimu huo naielekeza Veta ipanue wigo wa uandaaji wa kurufu na walimu tarajali wa mafunzo ya amali kwa ajili ya shule za sekondari pamoja na vyuo vya ufundi stadi,” amesema.
Naibu Waziri huyo amesema suala hilo litafanikiwa zaidi kwa kuweka utaratibu mzuri kwa wahitimu wa chuo hicho kupatiwa mafunzo ya mbinu za ufundishaji na ujifunzaji (Pedagogical Skills) kwa kushirikiana na Chuo cha Veta cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro (MVTTC).
Akizungumzia chuo hicho, Naibu Waziri huyo amesisitiza Veta kutekeleza wajibu wake na kuendeleza ushirikiano na wadau muhimu wakiwamo wa sekta ya binafsi wa ukarimu na utalii ambayo ina mchango mkubwa katika pato na uchumi wa Taifa, kuanzia uandaaji wa mitaala na utoaji wa mafunzo.
Wanu amesema Tanzania inaendelea kupiga hatua kubwa katika maendeleo ya sekta mbalimbali za kiuchumi nchini na kumekuwa na ongezeko la maeneo mapya ya uwekezaji, ujenzi wa viwanda vidogo, vya kati na vikubwa na ukuaji wa sekta za kipaumbele ikiwepo madini, uchumi wa bluu, utalii, ukarimu na kilimo biashara.
“Nimeshuhudia chuo hiki ni cha mfano hapa nchini kinachotoa mafunzo na Huduma ya Ukarimu na Utalii, na hivyo kuwasaidia wananchi kupata ujuzi unaotakiwa kwenye sekta ya utalii yenye mchango mkubwa hapa nchini,” amesema.
Mkurugenzi Mkuu wa Veta, Anthony Kasore amesema hadi sasa wana vyuo 80 katika wilaya na mikoa mbalimbali nchini na vingine vimeendelea kujengwa.
Amesema Veta imeendelea kuongeza wigo wa ushirikiano na wadau wa nje ambao wamekuwa wakileta wanafunzi na kuwalipia moja kwa moja kupitia kampuni zao, kwa Veta Arusha inapokea wanafunzi 80 wa kutoka kwa wadau hao.
Awali, mkuu wa chuo hicho, Magubi Mabelele amesema chuo hicho kilianza mwaka 2010 hoteli iliyoko chuoni hapo imekuwa ikiingiza mapato ambayo yamekuwa yakitumika katika uendeshaji wa gharama za chuo pale ambapo makao makuu inapokuwa imezidiwa.
Amesema chuo hicho kimekuwa kikikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mabweni ya kulala wanafunzi jambo ambalo linawafanya kubuni namna ya kuweza kupokea wanafunzi wote kwa pamoja.
“Chuo kina uwezo wa kudahili wanachuo 1,200 kwa mwaka kupitia fani tano za usafiri wa utalii, mapokezi, uokaji, upishi na usafi, pia, tumekuwa tukitoa udahili kwa wanaotaka mafunzo mafupi pamoja na mafunzo maalumu, hata hivyo tuna changamoto ya mabweni,” amesema.
Mkurugenzi wa Veta Kanda ya Kaskazini, Monica Mbele amesema ofisi yake inaendelea na ujenzi wa vyuo vinane katika maeneo ya wilaya mikoa ya kanda ya kaskazini ambayo hayakuwa na vyuo hivyo.
Amesema baada ya kukamilika kwa ujenzi wa vyuo hivyo, Veta kanda ya kaskazini itakuwa na jumla ya vyuo 22 na kuongeza idadi kubwa ya wahitimu.
