Wabunge waapa kuisimamia Serikali, vikao vya kamati za Bunge vikiitishwa

Dodoma. Wakati vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge vikitarajiwa kuanza Januari 13 hadi 23, 2026, baadhi ya wabunge wamesema wamejiandaa kufanya kazi kwenye kamati watakazopangiwa ili kuisimamia vema Serikali.

Vikao hivyo ni maandalizi ya mkutano wa pili wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, unaotarajiwa kuanza shughuli zake baada ya vikao vya kamati kumalizika katika wiki mbili za mwanzo.

Shauku ya wananchi ni kuona wabunge watakaoongoza kamati nyeti, kama vile Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Serikali za Mitaa (LAAC) na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), ambazo huongozwa na wapinzani.

Taarifa iliyotolewa leo Januari 6, 2026, na Ofisi ya Bunge inaeleza kwamba wabunge wanatakiwa kufika Dodoma kuanzia Januari 12, 2026, kwa ajili ya kuanza vikao hivyo siku inayofuata, Januari 13. Moja ya shughuli kwenye vikao hivyo ni uchaguzi wa wenyeviti na makamu wenyeviti wa Kamati za Bunge kwa mujibu wa kanuni ya 138(1) ya kanuni za Bunge za mwaka 2025.

“Vikao vya Kamati za kudumu za Bunge vitaanza kufanyika siku ya Jumanne, Januari 13, hadi Januari 23, 2026, katika Ofisi ya Bunge jijini Dodoma,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.

 Aidha, wabunge watapata nafasi ya kuzifahamu wizara na taasisi zake pamoja na baadhi ya sera na sheria kulingana na majukumu ya kila kamati, kama ilivyofafanuliwa kwenye nyongeza ya nane ya kanuni ya 140 ya kanuni za Bunge.

Wabunge kwenye kamati hizo pia watapitishwa kwenye majukumu yao ya msingi, na Kamati ya Uongozi itafanya maandalizi ya hoja zitakazojadiliwa kwenye kikao cha Bunge.

Akizungumzia vikao hivyo, mbunge wa Tunduru Kaskazini (ACT Wazalendo), Ado Shaibu, amesema wao kama wabunge wa upinzani wamejipanga kutumia vizuri kila fursa watakayoipata ili wapaze sauti zao, hasa katika kuiwajibisha Serikali.

Amesema wabunge wa upinzani ni wachache kuliko kipindi kingine chochote tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi, hivyo ni muhimu kuwa na mikakati maalumu ya uwakilishi wa wananchi.

Mbunge huyo anasema wataanza kutoa mchango ndani ya kamati na mijadala ya Bunge, huku akikiri kwamba mkutano wa pili wa Bunge utajikita zaidi katika mjadala wa hotuba ya Rais, lakini kila nafasi itakayopatikana lazima waitumie vyema kwa masilahi ya wananchi.

“Naomba wananchi watambue kuwa tunakwenda kufanya kazi ya kushirikiana na sisi tulio wachache. Hata ndani ya CCM kuna wabunge huwakilisha wananchi, na hao tutakuwa nao kwani wataonesha nia njema,” amesema Ado.

Kwa upande wake, mmoja wa mawaziri katika Bunge lililomaliza muda wake, ambaye ameomba asitajwe jina, amesema Spika Zungu ni mzoefu katika Bunge, hivyo hana mashaka kuhusu usukwaji wa kamati.

Waziri huyo amesema hofu yake ndogo ni namna ya kumpata Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, lakini kwa kamati zilizobakia haoni kama kutakuwa na shida.

Akizungumzia maandalizi ya mkutano wa pili wa Bunge la 13, mbunge wa viti maalumu (CCM), Cecilia Paresso, amesema hili halitakuwa Bunge la kulala, bali litakuwa la kasi katika kuisimamia na kuishauri Serikali.

Amesema wananchi watarajie makubwa kwenye mipango na ahadi za Serikali, ikiwemo maji, umeme, elimu, barabara, kilimo na ufugaji, ambazo moja kwa moja zinawagusa wananchi.

Paresso amesema moto aliokuwa nao akiwa chama pinzani hautazima hata anapokuwa ndani ya chama kinachotawala.

“Kikubwa ni kusimama katika hoja zenye kuleta maslahi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla, sitaweza kunyamaza pale nitakapoona mambo mengi hayaendi sawa lazima nipaze sauti, hatutaki Bunge na ndiyo mzee,” amesema Paresso.

Paresso anasema msingi wa mambo yote ni kuangalia ndani ya nchi kuwa na utulivu na amani kwani ndiyo msingi wa maendeleo huku akizungumzia hotuba ya Rais, amesema lazima waijadili na kuichambua vizuri ili kufikia malengo makuu yenye matamanio ya kuacha tabasamu kwa Watanzania.