Wananchi Arusha watoa dukuduku kwa tume Jaji Chande

Arusha. Wananchi wa Mkoa wa Arusha wameitaka Tume ya kuchunguza matukio yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 kuhakikisha mapendekezo itakayowasilisha yanagusa kwa kina suala la mabadiliko ya Katiba.

Wamesema mabadiliko ya Katiba ndio chanzo kikuu cha malalamiko na machungu yaliyoibuka na kusababisha vurugu za Oktoba 29, 2025 baada ya kukosekana haki ya kusikilizwa na kutekelezwa.

Tume hiyo inayoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman, imeanza kupokea maoni ya wananchi wa Arusha Januari 6, 2026, kupitia mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Mkuu wa Wilaya ya Arusha.

Oktoba 29, 2025 zilitokea vurugu katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Songwe, Geita, Arusha, Mara na Ruvuma, zilizosababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali.

Kufuatia matukio hayo, Rais Samia Suluhu Hassan aliunda Tume ya Uchunguzi, ambayo ripoti yake inatarajiwa kuwa mwongozo wa kuanzisha mchakato wa maridhiano kupitia Tume ya Maridhiano na Upatanishi itakayoundwa baadaye.

Akifungua mkutano huo, Jaji Chande amesema shughuli hiyo ni ukurasa maalumu wa kusikiliza maoni, uzoefu na mapendekezo ya wananchi, kwa lengo la kuiwezesha Tume kufanya uchunguzi wa kina, wa haki na jumuishi.

Amesema Tume inalenga kubaini chanzo cha matukio hayo, kutathmini hatua zilizochukuliwa na kuainisha mapendekezo ya kurejesha na kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa.

“Kwa heshima kubwa, tunawakaribisha wadau wote wakiwemo wananchi, asasi za kiraia, taasisi za Serikali na kidini, viongozi wa jamii na vyama vya kitaaluma kushiriki na Tume inathamini maoni yote yatakayopokelewa, kwani yatakuwa msingi wa kujenga maridhiano ya kitaifa,” amesema Jaji Chande.

Akizungumza katika mkutano huo, Samweli Mungure, mkazi wa Arusha aliyepoteza ndugu katika vurugu hizo, amesema mabadiliko ya Katiba ni suluhisho la msingi la kuzuia migogoro kama hiyo kujirudia.

“Wengi wanaona maandamano yalikuwa na sababu nyingi, lakini kiini chake ni Katiba mpya, hivyo Serikali ione umuhimu wa kufanya mabadiliko ya kina, kwani hiyo ndiyo njia kubwa ya kuponya majeraha, na kuleta suluhusho,” amesema.

Kwa upande wake, Seth Venase amesema changamoto ya ajira, hususan kwa vijana imekuwa chanzo kikubwa cha hasira dhidi ya Serikali na kuzua maandamano.

Ameeleza kuwa kodi na ushuru nyingi vinawakatisha tamaa vijana kujiajiri au kuanzisha biashara.

“Vijana wengi wanajitahidi kuuza au kuanzisha biashara, lakini vikwazo ni vingi, ajira za kuajiriwa ni chache, hali inayoongeza chuki na kukata tamaa,” amesema.

Ameongeza kuwa Serikali inapaswa kuwaunga mkono vijana wenye mawazo ya uwekezaji kwa mitaji nafuu na kupunguza vikwazo vya kikodi vinavyokwamisha maendeleo yao.

Naye Samweli Kilwa, amesema umuhimu wa haki ya kujieleza na kusikilizwa ni mdogo licha ya kufundishwa katika somo la uraia, lakini utekelezaji wake bado ni changamoto.

“Wengi walichokuwa wanapambania ni haki ya kujieleza. Serikali ilipaswa kusikiliza na kuchukua hatua, badala ya kutumia nguvu zilizoongeza madhara hata kwa wasiohusika,” amesema.

Amesema kuwa tume hiyo itaweza kuacha alama na kumbukumbu njema katika kizazi kijacho endapo itahakikisha ripoti yao itazalisha malengo ya maandamano hasa mabadiliko ya katiba mpya.

Katika ushuhuda wa yaliyokea Rebeka Kasarani amesema familia yake ilipoteza kijana wa miaka 17, Allen Joram, aliyepigwa risasi alipokuwa akienda dukani na bado hawajapata mwili wake, hivyo kuiomba Serikali kusaidia upatikanaji wa mwili.

“Mtoto wetu hakuwa mwandamanaji lakini aliuawa, tulizunguka hospitali na vyumba vya kuhifadhia maiti bila mafanikio.

“Baada ya siku tatu tuliambulia kiatu chake pekee bila mwili,” amesema huku akiitaka Tume kuhakikisha haki inatendeka kwa waathirika na familia zao ikiwemo kupata mwili wa mtoto wao.

Maiko Baraka, naye amesema tukio la kupoteza mkewe, Neema, aliyepigwa risasi mlangoni akiwa anaendelea na shughuli zake za kila siku, ameumia na kuomba Serikali kulichukulia jambo kwa uzito katika hatua ya usuluhishi.

“Picha zilisambaa mitandaoni watoto wakimlilia mama yao katika tukio hilo lilitokea Sakina, Kibanda cha Maziwa. Naomba Serikali iache kudai walioathirika wote walikuwa waandamanaji, kwani hilo linaongeza machungu, bali wafanye usuluhishi wenye kusaidia familia kupata faraja,” amesema.

Kwa upande wa wazee, Godluck Kaaya (70), mstaafu wa Serikali, alionya kuhusu wimbi la vijana wasiokuwa na ajira wanaohamia mijini, akisema hali hiyo ni bomu la kijamii.

“Kama hatua hazitachukuliwa kuwaunganisha vijana katika fursa za ajira, maandamano ya Oktoba 29 yatakuwa madogo ukilinganisha na yatakayokuja,” amesema.

Akihitimisha mkutano huo, Jaji Chande amesema Tume imepokea maoni na malalamiko yote na itaendelea kuyafanyia kazi ndani ya muda wa siku 90 iliopewa.

“Lengo si kulundika lawama, bali kubaini ukweli wa nani alifanya nini, kwa nini, na nani aliathirika na taarifa itakayopatikana itaiongoza Serikali katika mazungumzo ya maridhiano na amani,” amesema.