Wananchi wataja kero ya kukatikakatika ka umeme

Mbeya. Wananchi wa Kata ya Iwiji, Wilaya ya Mbeya Vijijini, wamelalamikia kukosekana kwa huduma ya umeme wa uhakika, wakisema hali hiyo inaendelea kuathiri kwa kiasi kikubwa shughuli zao za kiuchumi na kijamii.

Wananchi hao wamedai kuwa kukatikakatika kwa umeme bila taarifa ya awali kumeongeza usumbufu na gharama za maisha, hali inayowalazimu kutembea umbali mrefu kufuata huduma muhimu, ikiwemo kunyoa nywele, kusaga nafaka na shughuli ndogondogo za ujasiriamali zinazotegemea nishati hiyo.

Kilio hicho walikitoa leo Jumanne, Januari 6, 2026, kwa mbunge wa Mbeya Vijijini, Patali Shida baada ya kukagua miradi ya maendeleo katika eneo hilo na kufanya mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero za wananchi wa kata hiyo.

Wananchi walimtaka mbunge huyo kuwasilisha changamoto hiyo kwa mamlaka husika ili hatua za haraka zichukuliwe kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika eneo hilo.

“Mbunge hatuna raha hata kidogo na haturidhishwi na upatikanaji wa huduma za  umeme kumekuwa na changamoto ya muda mrefu kuna wakati hata siku mbili hatupati huduma na hakuna taarifa hivyo tunaathirika kiuchumi katika ngazi za familia na kijamii,” amesema Waziri Mwala.

“Tunaomba Serikali kusikia  kilio chetu kupitia kwa mwakilishi wetu, mbunge Patali Shida tupate umeme wa uhakika kwa kutambua asilimia kubwa vijana tumejiajiri katika shughuli mbalimbali hususani usafirishaji nafaka na kinyozi,” amesema.

Kwa upande wake Diwani wa Iwiji, Tuyonje Mwazembe amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kwamba  kati ya vitongoji  29, vilivyopo katika eneo lake  24 pekee bado havija unganishiwa nishati ya umeme.

“Nashukuru Mungu kilio hicho wananchi wamefikisha kwako mbunge, lakini nami nisisitize ombi hilo kuweza  kuingilia kati ili kuharakisha mchakato na wananchi  warejeshe matumaini kwa Serikali yao kwa lengo la kuwaondoa gizani,” amesema.

Kufuatia kilio hicho, Patali amesema  atahakikisha anasimamia kilio cha kukatika katika kwa umeme kutokana na uwekezaji mkubwa wa Serikali ya awamu ya sita kuona vitongoji vyote na vijiji vinafikiwa na rasilimali hiyo muhimu.

“Serikali imewekeza nguvu kwenye suala la upatikanaji wa uhakika wa nishati ya umeme mijini na vijijini lengo ni kuona vijana wanajiajiri katika nyanja mbalimbali za kiuchumi,” amesema.

Katika hatua ya kuwahakikishia wananchi kuwa changamoto hiyo itapatiwa ufumbuzi, Shida, alilazimika kumpigia simu Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Mbeya ili kupata ufafanuzi kuhusu kero ya kukatikakatika kwa umeme katika Kata ya Iwiji.

Akizungumza kwa njia ya simu, Meneja wa Tanesco Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Seleman Mgwira, amesema shirika hilo tayari limepokea taarifa za changamoto ya kukatika kwa umeme katika eneo hilo na kubaini kuwa hali hiyo ni sehemu ya changamoto zinazohitaji mkakati wa muda mfupi na wa muda mrefu, ambao utekelezaji wake tayari umeanza ili kumaliza tatizo hilo.

Aidha, Mhandisi Mgwira amesema kupitia Mradi wa Nishati  Vijijini (REA) katika Wilaya ya Mbeya Vijijini, jumla ya vitongoji 114 vinatarajiwa kunufaika na upanuzi wa huduma ya umeme, hatua ambayo itachochea shughuli za kiuchumi na kuboresha maisha ya wananchi wa maeneo husika.