Watoto wetu wako salama mabwenini?

Mabweni. ambayo awali yalichukuliwa kama sehemu salama za kulea nidhamu, kuimarisha malezi ya pamoja na kuwezesha mtoto kupata muda wa kujisomea bila usumbufu wa majukumu ya nyumbani, sasa yanatazamwa kwa jicho tofauti. 

Swali tunalojiuliza katika makala haya ni kama mabweni bado ni sehemu salama kwa watoto wetu.

 Swali hili linazidi kuwa na uzito kila uchao kutokana na kuongezeka kwa taarifa na matukio ya vitendo vya ulawiti, usagaji na mienendo isiyofaa inayoripotiwa ndani ya mabweni.

Katika shule mbalimbali za msingi na sekondari, kuna taarifa nyingi za watoto wa kiume kudhalilishwa kingono na wenzao wakubwa au hata wale wa umri mmoja, huku wengine wakilazimishwa kushiriki vitendo vya ushoga.

 Vilevile, mabweni ya wasichana nayo hayako salama, kuna taarifa za watoto wanaolazimishwa kuingia katika uhusiano wa kimapenzi wa jinsia moja (usagaji), wakihofishwa au kushawishiwa kwa njia mbalimbali. 

Mara nyingi vitendo hivi hutokea usiku, bila walimu au walezi wa mabweni kufahamu, au kwa baadhi ya matukio, hata kwa uhusika wa baadhi ya wale wanaopaswa kuwalinda watoto.

Jamii nyingi bado zina kigugumizi katika kujadili masuala ya ukatili wa kingono dhidi ya watoto, hasa yanapohusiana na masuala ya ushoga au usagaji. 

Lakini ukweli mchungu ni kuwa vitendo hivi vipo, vinaendelea, na vinaathiri maisha ya watoto wetu kwa kiwango kikubwa.

 Wengi hubeba maumivu ya kiakili na kihisia kwa miaka mingi, huku wakiwa hawana ujasiri wa kuzungumza walichopitia. 

Baadhi hujikuta wakibadili mienendo yao ya kijinsia, wengine hupoteza kabisa kujiamini, na kwa wachache hali hiyo huwasukuma kuachana na masomo.

Kwa nini hali hii inazidi kushamiri katika mabweni? Sababu ni nyingi, lakini kubwa kati ya zote ni udhaifu katika mifumo ya uangalizi wa watoto. 

Walezi wengi wa mabweni hawana mafunzo ya kutosha ya saikolojia ya mtoto na mbinu za kutambua tabia hatarishi kwa haraka.

 Muda mwingi wa usiku watoto huachwa wenyewe bila uangalizi wa karibu, na wale wanaopaswa kuangalia mienendo yao, ama wamejikita kwenye kazi nyingine au hawana motisha ya kutekeleza wajibu wao ipasavyo.

Vilevile, shule nyingi hazina sera madhubuti au mifumo ya wazi ya kutoa taarifa pale panapotokea vitendo vya ukatili. 

Watoto hawaelekezwi namna ya kutoa taarifa kwa usiri na bila kuogopa adhabu au kubezwa. Wengine huambiwa “msingizie” au “mtajiletea matatizo” wanapojaribu kueleza wanachopitia. 

Hali hii huwafanya waathirika kuwa waoga, huku wahalifu wakiendelea na vitendo vyao bila woga wowote.

Ni wakati sasa wa shule zote za mabweni  za serikali na binafsi,  kuweka mifumo madhubuti ya kulinda watoto dhidi ya vitendo hivi. 

Kwanza, ni muhimu kuwa na sera ya ulinzi wa mtoto  inayojulikana na kueleweka na walimu, wafanyakazi wote wa shule na wanafunzi. 

Sera hiyo itoe miongozo ya wazi kuhusu nini kinachokubalika na kisichokubalika, hatua za kuchukua iwapo kuna tukio la ukiukwaji wa maadili, na namna ya kutoa taarifa kwa usiri.

Pili, shule ziweke mfumo salama wa kutoa taarifa ambapo mwanafunzi anaweza kueleza anachopitia bila hofu ya kudhalilishwa, kutengwa au kuadhibiwa.

 Mfumo huu unaweza kuwa ni sanduku la maoni la siri, namba maalumu ya simu ya msimamizi wa watoto au hata mtandao maalum wa malalamiko. Mfumo huu uwekwe wazi kwa wanafunzi na wapewe elimu ya mara kwa mara namna ya kuutumia.

Tatu, walezi wa mabweni wapate mafunzo ya mara kwa mara ya malezi, ushauri nasaha na mbinu za kufuatilia mienendo ya watoto. 

Walezi hawa wasiwe watu walioteuliwa tu kwa sababu ya upungufu wa wafanyakazi, bali wawe watu wenye weledi, maadili, na wito wa kweli wa kazi ya kulea na kuwalinda watoto.

Nne, shule zifanye tathmini ya kisaikolojia na kitabia ya wanafunzi mara kwa mara kwa kushirikiana na wataalamu wa saikolojia. 

Hii itasaidia kubaini mapema tabia hatarishi, ushawishi wa makundi mabaya au mabadiliko ya kitabia yanayoweza kuwa ishara ya mtoto kupitia changamoto zisizoeleweka.

Tano, wazazi nao wanapaswa kuwa sehemu ya ulinzi wa mtoto. Shule zibuni utaratibu wa kuhusisha wazazi kwa karibu kupitia vikao, mafunzo ya malezi na midahalo kuhusu usalama wa watoto wao.

 Wazazi wengi huamini mabweni ni suluhisho la matatizo yao ya kifamilia au kazi, lakini bila kushirikishwa katika malezi ya kila siku, watoto huweza kupotea mwelekeo na kuangukia mikononi mwa waharibifu.

Kama taifa, hatuwezi kuendelea kupuuza hali hii. Tunapowapeleka watoto wetu shule za bweni, tunaamini tumewaweka katika mikono salama.

Tunatarajia watalelewa katika maadili mema, watasoma kwa bidii, na hatimaye kuwa watu wa maana kwa familia na taifa.

 Lakini pale tunaposhindwa kuweka mifumo ya kuwalinda, tunageuza mabweni kuwa maeneo ya mateso ya kimya, mahali ambapo ndoto zao zinavunjika bila sauti kusikika.

Ni lazima sasa tufungue mjadala mpana, usio na aibu wala woga, kuhusu mienendo ya wanafunzi mabwenini. Tuache kufumbia macho, na badala yake, tuamue kwa dhati kujenga mazingira salama, yenye staha na maadili kwa watoto wetu. 0754990083