…………..
CHATO
WAZIRI wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally, amempongeza Mbunge wa Jimbo la Chato kusini kufuatia mikakati mizuri ya kuwainua vijana kiuchumi kupitia sekta ya mifugo.
Ni baada ya Mbunge huyo, kuahidi kutoa msaada wa ng’ombe 18 kwa vikundi vya vijana waliopo tayali kufuga kisasa kwaajili ya kuongeza uzalishaji wa maziwa kwenye jimbo hilo.
Dkt. Bashiru akizungumza na wadau wa mifugo na uvuvi katika kikao maalumu cha mkoa wa Geita kilichofanyika kwenye Chuo cha usimamizi wa fedha kampasi ya Geita-Chato, (IFM) amewasisitiza wadau kuacha kufuga kwa mazoea badala yake watumie fursa zilizopo ili kupata tija.
Amewashauri wafugaji kubadilisha mitazamo yao ya kuendelea kufuga ki zamani na kusababisha migogoro mingi ya wakulima na wafugaji badala yake waingie kwenye kilimo bora cha majani ya mifugo, kunenepesha mifugo, kuongeza uzalishaji wa maziwa, kuuza mifugo yao kwa kg na kufuga samaki kwa njia ya vizimba.
“Ninawashauri wafugaji tuanze kufuga kibiashara, tuache kufuga kizamani, sekta ya ufugaji bado inachangia pato dogo sana katika uchumi wa taifa natamani tutoke huko, watu wapate tija katika ufugaji, na hii litawezekana kama tutatengeneza malisho ya kisasa na huduma za ugani kwa ng’ombe wetu” amesema Dkt. Bashiru.
Kutokana na michango mbalimbali yenye kuongeza uelewa kwa wafugaji na wavuvi, Mbunge wa Jimbo la Chato Kusini, Pascal Lukas Lutandula, akaguswa na njia bora za ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na kuahidi kuinua uchumi wa vijana wa jimbo lake kwa kuwagawia ng’ombe wawili kila kata.
Uamuzi huo umeonekana kumfurahisha zaidi Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, kwa kuwa umelenga kuinua uchumi na kuongeza ajira kwa vijana ambao serikali inaendelea kuweka mikakati ya kuwasaidia kujikwamua na lindi la umaskini.
Mbali na hilo, ameahidi kushirikiana na mamlaka zingine ili kuanzisha mashamba darasa ya ufugaji kwenye Jimbo lake ili kubadilisha mitazamo ya wafugaji na wavuvi kwa kuwa sekta hiyo ikiendeshwa kisasa inauwezo wa kuinua uchumi wa mtu, kaya na taifa kwa ujumla.
Ahadi ya Mbunge huyo, imekuja ikiwa ni siku chache baada ya kuwagawia wananchi wa jimbo lake ng’ombe tisa kwaajili ya kusherehekea sikukuu ya mwaka mpya 2026.
Upo msemo usemao “Huwezi kuongeza maziwa ndani ya grasi iliyojaa, ila unaweza kuongeza sukari ndani ya maziwa yaliyojaa na ukaongeza radha ya maziwa hayo” ikimaanisha watu wema wanaweza kupata nafasi hata katika moyo uliojaa.
Pongezi kwa Mheshimiwa Mbunge kuguswa na shida za wananchi wake na kuwa na moyo wa dhati kutatua changamoto za kiuchumi kwa jamii anayoiongoza.
Mwisho.

