Na: OWM (KAM) – Mwanza
Waziri wa Nchi, ofisi ya Waziri Mkuu – Kaz, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Clement Sangu amekagua maendeleo ya ujezi wa Mradi wa hoteli ya Nyota tano unaotekelezwa na NSSF ambao ujenzi wake umefikia asilimia 83.
Aidha, Mhe. Sangu amefanya ziara hiyo leo tarehe 5 Januari, 2025, Jijini Mwanza na mara tu alipowasili katika mradi huo alipokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba pamoja na Watumishi wa NSSF Mkoani wa Mwanza.
Akizungumza baada ya kukagua na kupata maelezo ya wataalam na wasimamizi wa mradi huo, Waziri Sangu amepongeza Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa hatua iliyofikiwa katika ujezi wa hoteli hiyo na kuagiza mkandarasi kukabidhi majengo hayo ndani ya muda uliopangwa kwa mujibu wa makubaliano ya mkataba.
‘’Nitoe maagizo kwa Mkurugenzi Mkuu na Watendaji wake, wasimamie mradi huu ukamilike ndani ya muda uliopangwa kwani utakuwa kivutio kwa wananchi na wageni wa mataifa mengine hivyo kupata fedha za kigeni zitakazo saidia katika ukuaji wa uchumi” amesema
Vilevile, Waziri Sangu amemshukuru Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mradi huo ambao umewekezwa katika eneo la kimkakati ndani ya Mkoa wa Mwanza na ambalo kiuchumi litaongeza thamani ya Jiji hilo na nchi kwa ujumla.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba ameahidi kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na Mhe. Waziri na amebainisha kuwa kazi zilizobaki katika ukamilishaji wa ujenzi huo zitaendelea kufanyika kwa ufanisi na kwa wakati ili mradi huo ukamilike kwa muda uliopangwa.


