HATUA ya makundi katika Kombe la Mapinduzi 2026, inahitimishwa leo kwa kupigwa mechi moja matata sana pale New Amaan Complex kuanzia saa 2:15 usiku ambapo itakuwa Yanga dhidi ya TRA United.
Hii inakumbushia wanavyopeana ushindani wa Ligi Kuu Bara na sasa wanahamishia Kombe la Mapinduzi ikiwa ni mechi ya kundi C.
Ni mechi ambayo imeshikilia uamuzi wa kufuzu nusu fainali ambapo Yanga inahitaji sare imalize kinara wa kundi na pointi nne, wakati TRA United ushindi ndio muhimu zaidi ili kukaa kileleni. Hivi sasa ina pointi moja, sare au kupoteza haina maana kwao.
Msimu huu timu hizo hazijakutana bado na hii itakuwa mara ya kwanza, lakini msimu uliopita kila mmoja alitamba nyumbani kwa mwenzake.
TRA United ambayo wakati huo ilikuwa ikiitwa Tabora United, ilianza kuichapa Yanga 1-3 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, kisha yenyewe ikapigwa 0-3 pale Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora.
Utamu wa mechi hii unakuja kutokea kwa wachezaji wa pande zote ambapo Emmanuel Mwanengo na Offen Chikola wanakutana na chama lao la zamani kwa mara ya kwanza tangu walihame msimu huu. Chikola aliondoka dirisha kubwa, Mwanengo dirisha dogo. Pia Denis Nkane aliyeenda TRA United kutoka Yanga, anakutana na waajiri wake hao.
Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves, anaamini hiki ni kipimo kizuri kwa kikosi chake katika mbio za kuwania taji hilo ambalo Yanga inalisaka kwa mara ya tatu baada ya kulibeba 2007 na 2021.
“Tumetoka kupata ushindi mechi ya kwanza dhidi ya KVZ na sasa tunakabiliwa na mechi nyingine ngumu dhidi ya TRA ambayo imekuwa ikifanya vizuri katika ligi,” amesema.
Kwa upande wa Ettiene Ndayiragije ambaye ni kocha wa TRA United, amesema: “Hiki ni kipindi cha kuangalia wachezaji wapya wanaokuja, lakini pia tunakitumia kuimarisha timu kwa ajili ya mashindano yaliyo mbele yetu.”
