YANGA imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya TRA United katika mechi ya kuhitimisha hatua ya makundi ya Kombe la Mapinduzi 2026.
Mechi hiyo iliyochezwa leo Januari 6, 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja, bao la ushindi lilifungwa na Celestine Ecua dakika ya 31 akiitumia vizuri pasi ya Maxi Nzengeli.
Katika mechi ya leo, Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves aliamua kumuanzisha Abubakar Othuman ‘Ninju’ katika beki wa kati sambamba na Frank Asinki, kisha eneo la kiungo wa kati, Duke Abuya na Mohamed Damaro wakicheza pamoja.
Mbali na hilo, Yao Kouassi Attohoula alirejea rasmi uwanjani akiingia dakika ya 82 kuchukua nafasi ya Kibwana Shomari.
Kwa upande wa TRA United, Denis Nkane aliyetua hapo hivi karibuni akitokea Yanga, alianza akicheza kwa dakika 73 na kumpisha Ramadhan Salum Chobwedo. Katika muda huo, Nkane alikuwa akipambana zaidi na Kibwana Shomari.
Matokeo hayo yameifanya Yanga kufuzu nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi 2026 ikiwa na pointi sita na kuongoza kundi C baada ya kushinda mechi zote mbili dhidi ya KVZ 3-0 na TRA United 1-0.
Yanga sasa inakwenda kucheza dhidi ya Singida Black Stars hatua ya nusu fainali, mechi ikipangwa kuchezwa Januari 9, 2026, saa 2:15 usiku.
Katika hatua ya makundi, Yanga imeweka rekodi ya kuwa ndio timu pekee iliyocheza bila ya kuruhusu bao, ikifunga manne.
