Zanzibar yazindua flyover ya kwanza Mwanakwerekwe

Unguja. Zanzibar imeandika historia mpya ya maendeleo baada ya kuzindua rasmi barabara ya juu (flyover) Mwanakwerekwe, mradi ambao ni ishara ya mafanikio ya kimaendeleo katika miaka 62 tangu Mapinduzi Matukufu.

Ujenzi wa flyover ni sehemu ya mfululizo wa miradi ya kisasa inayolenga kuboresha miundombinu ya usafiri, biashara na huduma za kijamii kisiwani humo.

Flyover hiyo ni ya kwanza Zanzibar na imejengwa kwa viwango vya kisasa, huku ikiongeza hadhi ya visiwa hivyo katika historia ya maendeleo, kwa kuwa Zanzibar pia imewahi kuwa miongoni mwa maeneo ya mwanzo barani Afrika kuanzisha huduma kama televisheni ya rangi, treni ya abiria na lifti za kisasa.

Ujenzi wa flyover hiyo ulianza Desemba 1, 2023 na kukamilika Desemba 31, 2025, ukigharimu Sh23.7 bilioni, kwa kuunganisha barabara kuu kutoka Uwanja wa Ndege wa Amani hadi katikati ya mji na kutoka Fuoni, hivyo kupunguza msongamano uliokuwa ukikumba makutano hayo kwa miongo kadhaa.

Akizungumza leo Jumanne Januari 6, 2026 wakati wa uzinduzi, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, amesema: “Katika kipindi cha miaka 62 ya Mapinduzi, Zanzibar imeendelea kushuhudia mafanikio makubwa ya kimaendeleo. Flyover hii ni historia mpya, ikionesha jinsi tunavyoweka miundombinu ya kisasa kwa wananchi wetu, kukuza uchumi na kuvutia wawekezaji.

“Barabara hii ni mradi wa kimkakati unaolenga kupunguza msongamano, kuongeza usalama wa watumiaji wa barabara na kurahisisha usafiri wa watu na mizigo,” amesema Rais.

Rais Mwinyi amesisitiza kwamba, uwekezaji katika miundombinu ni nguzo muhimu ya kukuza uchumi, kuchochea shughuli za kibiashara na kuvutia wawekezaji.

“Slogan yetu ni uongozi unaoacha alama, na leo tumeitekeleza kwa vitendo dhamira hiyo,” amesema.

Rais Mwinyi pia amewataka wananchi kuitunza na kuitumia ipasavyo barabara hiyo ili idumu kwa vizazi vijavyo, huku akiahidi kulipa fidia stahiki kwa yeyote atakayepishana na miradi ya maendeleo.

Barabara hiyo ya juu namba moja, imepewa jina la Hussein Ali Hassan Mwinyi Mwanakwerekwe, ni mradi wa kimkakati unaolenga kupunguza msongamano wa magari, kuongeza usalama wa watumiaji wa barabara na kurahisisha usafiri wa mizigo na abiria.

Katibu Mkuu wa Ujenzi na Uchukuzi, Ali Said Bakar amesema flyover hiyo imejengwa kwa kutumia nguzo 48 zilizozikwa chini ya ardhi kwa kina cha mita 29 hadi 32, miinuko ya mita 230–240, na upana wa barabara ya juu mita 18.

Pia, amesema flyover inaweza kubeba mzigo wa hadi tani 70, ikiwa na mitaro, njia za wapita kwa miguu na taa za barabani, yote yakiwa yamekamilika kwa viwango vya juu.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk Khalid Salum Mohammed amesema flyover hiyo ni matokeo ya maono na busara za kiongozi, akibainisha kuwa mradi huo unapanua mfumo wa barabara mjini na vijijini, ukijumuisha mradi wa flyover mbili zitakazokamilisha mpangilio mzima wa usafiri.

Wakazi na watumiaji wa barabara hiyo wameridhishwa na matokeo yake. Abdull Said Haji, mkazi wa Kwerekwe, amesema: “Flyover hii itapunguza muda wa kusubiri, kuokoa gharama na kurahisisha shughuli za kila siku kwa wananchi.”

Ashura Juma Amour amesema: “Msongamano ulikuwa kero kubwa. Sasa barabara hii itarahisisha usafiri na usafirishaji kwa wote, ikitoa nafuu kwa wakazi na abiria.”