Aga Khan yapata ithibati ya JCI kwa mara ya nne

Dar es Salaam. Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam imeendelea kuimarisha hadhi yake kama kinara wa kitaifa na kikanda katika ubora wa huduma za afya na usalama wa wagonjwa, baada ya kutunukiwa kwa mara ya nne mfululizo muhuri wa dhahabu wa ithibati kutoka Joint Commission International (JCI) ya Marekani.

Ithibati ya JCI inatambulika kama kigezo cha juu duniani katika utoaji wa huduma za afya salama, zenye ufanisi na zinazomweka mgonjwa katikati.

Kupitia ithibati hiyo, Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam inaendelea kuwa hospitali pekee nchini iliyopata heshima hiyo kubwa.

Hayo yamesemwa leo, Jumatano, Januari 7, 2026, na Ofisa Mwendeshaji Mkuu wa Taasisi ya Huduma za Afya ya Aga Khan nchini, Sisawo Konteh.

Konteh amesema baada ya kupata ithibati ya kwanza mwaka 2016, hospitali hiyo imefanikiwa kuidhinishwa upya mara mbili, huku ithibati ya nne mfululizo iliyopatikana mwaka 2025 ikidhihirisha dhamira yake ya kudumisha ubora na kuendeleza maboresho endelevu katika utoaji wa huduma za afya.

Kwa mara ya kwanza, Konteh amesema kazi ya tathmini ya ithibati ilifanyika kwa njia ya mtandao, hatua aliyoitaja kuwa na mafanikio makubwa yanayoonesha uwezo wa hospitali katika matumizi ya teknolojia na utayari wake wa kukidhi viwango vya kimataifa hata chini ya tathmini ya mbali.

“Katika tathmini ya mwaka huu, hospitali ilisifiwa kwa uimara wa mifumo yake ya uongozi wa kitabibu, uendeshaji wa shughuli na kuimarika kwa utamaduni wa utoaji wa huduma bora unaozingatia ubora na usalama wa wagonjwa,” amesema na kuongeza;

“Kupata ithibati ya JCI kwa mara ya nne ni ushahidi wa kujitolea kwa madaktari, wauguzi, wasimamizi na wafanyakazi wote wa Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam, kwamba wanafanya kazi kwa bidii kila siku ili kuhakikisha viwango vya kimataifa vinazingatiwa huku wakitoa huduma zenye huruma na zinazomlenga mgonjwa kwa wananchi wa Tanzania,” amesema Konteh.

Amesema mafanikio hayo pia yanaonesha uwekezaji endelevu wa Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN) katika kuimarisha mifumo ya afya na kupanua upatikanaji wa huduma bora za afya katika ukanda huu.

“Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam, inaendelea kujidhatiti katika kuinua ubora wa huduma, kupanua huduma za kibingwa na kukumbatia ubunifu ili kuendelea kutoa huduma za afya za kiwango cha kimataifa na kuweka viwango vipya vya ubora nchini Tanzania na nje ya nchi,” amesema Konteh.

Aga Khan Health Services (AKHS) ni miongoni mwa taasisi tatu chini ya AKDN zinazosaidia shughuli za afya, pamoja na Wakfu wa Aga Khan na Chuo Kikuu cha Aga Khan.

Kwa pamoja, taasisi hizo hutoa huduma bora za afya kwa takribani watu milioni 14 kila mwaka, zikiwa na mkazo mkubwa katika mipango, mafunzo na maendeleo ya rasilimali watu.

AKHS pia hushirikiana na Huduma za Elimu za Aga Khan na Wakala wa Aga Khan wa Makazi ili kuunganisha vipaumbele vya afya katika miradi ya pamoja.