Askari wa JWTZ, raia watatu kortini kwa uhujumu uchumi

Moshi. Askari wawili wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na raia watatu wamefikishwa kortini mjini Moshi, wakikabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi ya kukutwa na nyara za Serikali zenye thamani ya Sh591.3 milioni.

Washtakiwa hao ni Sajenti Andrew Ndaga mwenye namba MT.76601 na Stesheni Sajenti Chumu Rajabu mwenye namba 76764 na raia ni Mzee Ally Mzee, Juma Cheupe na Ally Ayubu maarufu kwa jina la ‘Hakimu’,

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi mkoani Kilimanjaro, Ally Mkama ilidaiwa kuwa katika shtaka la kwanza linalowakabili askari wawili wa JWTZ ambao ni Sajenti Ndaga, Stesheni Sajenti Rajabu na Mzee.

Makosa yao yanaangukia katika kifungu namba 86(1) na (2)(b) cha Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori iliyofanyiwa marejeo mwaka 2023, ikisomwa pamoja na kifungu namba 57(1) na 61(2) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi.

Katika kosa la kwanza, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa Oktoba 21, 2025, huko eneo la Sango katika wilaya ya Moshi, walipatikana na meno ya tembo 16 na vipande 15 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh591.3 milioni.

Meno hayo, ambayo ni mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni sawa na tembo 12 waliouawa wenye thamani ya Dola 240,000 za Marekani (Sh591.3 milioni), kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.

Katika kosa la pili, linalowakabili Sajenti Ndaga na raia wawili ambao ni Cheupe na Ayubu maarufu kwa jina la ‘Hakimu’, wanakabiliwa na makosa ya kujihusisha na kufanya biashara ya nyara za Serikali kinyume cha sheria.

Inadaiwa katika tarehe mbalimbali katika miezi ya Julai na Oktoba 2025, katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, walijihusisha na biashara ya nyara za Serikali kinyume cha sheria.

Inaidaiwa katika tarehe hizo na maeneo hayo, waliuza, kununua, kuhamisha, kusafirisha na kupokea meno ya tembo 16 na vipande 15 vya meno ya tembo, sawa na tembo 12 waliouawa. Meno hayo, ambayo ni mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yalikuwa na thamani ya dola 240,000, sawa na Sh591.3 milioni za Tanzania.

Kulingana na sheria, kesi za aina hiyo husikilizwa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi. Hata hivyo, inaelezwa kuna mazingira yanayoruhusu zisikilizwe na mahakama za chini kwa kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Kifungu 86(1)(b) cha Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori kinasema mtu akitiwa hatiani, na kama thamani ya nyara ni Sh100,000, atatozwa faini ya jumla isiyopungua mara kumi ya thamani ya nyara au kifungo kisichozidi miaka 30 au vyote viwili.

Lakini kifungu hicho, pamoja na kifungu 61(2) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi, kinatoa adhabu ya kifungo cha jela kwa muda usiopungua miaka 20 lakini usiozidi miaka 30 au adhabu ya kifungo hicho na hatua nyingine yoyote ya adhabu.

Pia kinaeleza kuwa isipokuwa pale sheria inapoweka hatua za adhabu kubwa zaidi kuliko zile zilizotolewa na sheria hiyo, Mahakama itaweka adhabu hiyo kubwa.

Kesi hiyo ya jinai namba 000027119 ya mwaka 2025, iliyopo, imepangwa kutajwa Januari 9, 2026 katika hatua za awali.