AZAM FC ipo katika mazungumzo na mshambuliaji Ben Malango ambaye kocha Florence Ibenge anatamani uzoefu wake uongeze nguvu ndani ya timu.
Malango ni Mkongomani ambaye amecheza Uarabauni katika timu kama Raja Casablanca na timu ya mwisho ni Qatar FC ambayo aliichezea msimu uliopita akiifungia mabao manne.
Licha ya kwamba hana timu kwa sasa, lakini kumekuwapo na mazungumzo ya pande mbili kati ya timu na mchezaji zinazopambana kukubaliana suala la maslahi.
Mmoja kati ya watu wa karibu wa mchezaji huyo ameliambia Mwanaspoti kwamba, wapo kwenye mazungumzo na Azam, lakini hawajafikia makubaliano ya mwisho.
Amesema Azam inamtaka Malango aiongezee nguvu hasa katika Kombe la Shirikisho Afrika, lakini kwa upande wao wanaiona timu hiyo kuwa ni moja kati ya klabu bora Tanzania.
“Tupo kwenye mazungumzo na Azam FC. Wanamtaka Ben, lakini bado hatujafikia mwisho. Kuna vitu tunataka pande mbili zifikie muafaka,” amesema mtu huyo.
“Haitakuwa vigumu kwa Ben kwenda Azam, ni timu nzuri na kitu muhimu ni kwamba atakwenda kufanya kazi na kocha anayemheshimu sana hapa DR Congo (Florent). Huyu ni baba wa wachezaji wengi hapa.
“Unajua Ben ni mshambuliaji mwenye uzoefu mkubwa hapa Congo, na anajua sana kufunga. Alitaka kupumzika kidogo na sasa tupo tayari kurudi kazini kama Azam watakubali tunayotaka, hakuna shida atakuja.”
Kama Azam itampata mshambuliajia huyo itakuwa na washambuliaji watatu ikiongezea kwa waliopo sasa ambao ni Nassor Saadun na Japhte Kitambala ambaye pia ni Mkongomani.
