Bodaboda aliyehukumiwa miaka 30 jela aruka kihunzi

Arusha. Mahakama ya Rufaa imefuta adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela iliyokuwa imetolewa dhidi ya dereva bodaboda, Mohamed Nyema maarufu Mudi wa Kusizi.

Nyema aliyehukumiwa kwa kosa la wizi wa kutumia silaha, ameachiwa huru baada ya kubaini upande wa mashtaka haukuthibitisha mashitaka yake bila kuacha shaka.

Uamuzi huo umetolewa na jopo la majaji watatu ukiongozwa na Ferdinand Wambali, Lucia Kairo na Deo Nangela, walioketi Dar es Salaam Desemba 29, 2025 na nakala ya hukumu hiyo ikiwekwa kwenye tovuti ya Mahakama.

Katika rufaa ya jinai namba 37 ya mwaka 2024, Mahakama imebaini kuwepo kwa dosari za kisheria, ikiwamo udhaifu katika ushahidi wa utambuzi wa mrufani eneo la tukio.

Hii ilikuwa rufaa ya pili kwa Nyema, baada ya awali kuhukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Mkuranga, hukumu iliyothibitishwa baadaye na Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam.

Katika mahakama ya chini, Nyema alishtakiwa pamoja na washtakiwa wenzake wawili ambao baadaye waliachiwa huru katika rufaa ya kwanza iliyosikilizwa na Mahakama Kuu.

Ilidaiwa kuwa Aprili 14, 2020, katika Kijiji cha Vikindu wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani, Nyema akiwa na wenzake wanne walivamia nyumba ya Shabani Ally na mkewe, Elizabeth George na kuiba mali mbalimbali zikiwamo fedha taslimu Sh4 milioni, televisheni, simu za mkononi na vitu vingine vyenye thamani ya Sh5.75 milioni.

Upande wa mashtaka ulidai kabla na baada ya tukio hilo, Nyema na wenzake walimjeruhi Shabani kwa kutumia panga ili kupata mali hizo.

Baada ya kukamatwa, Nyema na wenzake walifikishwa mahakamani, upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi sita kuthibitisha shtaka hilo.

Mahakama hiyo ilimkuta Nyema na wenzake wawili na hatia, ikieleza kuwa ushahidi wa mashahidi wa kwanza na wa pili wa Jamhuri uliwathibitisha kwa utambuzi wa macho.

Hata hivyo, Nyema alikata rufaa Mahakama ya Rufaa huku akiwasilisha sababu nne, akidai kuwa hakuwa na hatia na hukumu yake ilitokana na ushahidi dhaifu na usioaminika wa utambuzi wa eneo la tukio.

Pia alidai Mahakama Kuu ilikosea kuunga mkono hatia na hukumu dhidi yake huku ikiwaachia huru wenzake wawili waliokuwa wamehukumiwa kwa msingi wa ushahidi unaofanana.

Sababu nyingine ilikuwa kwamba ushahidi wa upande wa mashtaka ulikuwa unapingana, usiotosha na wa ajabu, hivyo kushindwa kuthibitisha kesi bila shaka yoyote.

Wakati wa kusikilizwa kwa rufaa hiyo, Nyema hakuwa na wakili, huku upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na wakili ambaye alipinga rufaa hiyo.

Wakili huyo alidai kuwa mashahidi waliweza kumtambua mrufani kwa sababu kulikuwa na mwanga wa kutosha wa umeme wakati wa tukio na kwamba, walimtaja kwa jina lake la utani, Mudi wa Kusizi, akidaiwa kuwa dereva bodaboda anayejulikana eneo hilo.

Hata hivyo, Jaji Deo Nangela akisoma uamuzi wa Mahakama, alisema jopo hilo limepitia kwa kina rekodi ya rufaa na kubaini kuwa ushahidi wa utambuzi wa mrufani haukuwa salama.

Alisema mashahidi hawakutoa maelezo ya kutosha kuhusu mazingira ya mwanga, aina ya taa zilizokuwepo wala kiwango cha mwanga wakati wa tukio.

Mahakama pia ilieleza kuwa madai ya kumtambua Nyema kwa jina la utani hayakuungwa mkono na taarifa za awali zilizotolewa Polisi, kwani jina hilo lilitajwa baada ya mashahidi kurejea kutoka hospitali bila kubainishwa muda uliopita.

Aidha, Mahakama ilionyesha wasiwasi kuhusu kuchelewa kwa kukamatwa kwa Nyema kwa takribani miezi minne baada ya tukio, licha ya kudaiwa kuwa alikuwa dereva bodaboda anayefahamika katika eneo hilo.

Kuhusu kuthibitisha kosa, Jaji Nangela alisisitiza ni wajibu wa upande wa mashtaka kuthibitisha kesi ya jinai bila kuacha shaka yoyote.

Alisema mapitio ya rekodi ya rufaa yalionyesha kuwepo kwa tofauti kubwa katika ushahidi wa mashahidi, ikiwamo idadi ya watu waliodaiwa kuhusika katika tukio hilo.

Mashahidi wa kwanza na wa pili walidai majambazi walikuwa watano, huku shahidi wa pili baadaye akidai walikuwa 11 na mpelelezi wa kesi akieleza kuwa shahidi wa kwanza alimwambia walikuwa 10.

Jaji alisema tofauti hizo haziwezi kupuuzwa kwa sababu zinaashiria uwezekano wa makosa katika utambuzi wa wahusika wa tukio la wizi wa kutumia silaha.

Kutokana na dosari hizo, Mahakama ya Rufaa ilihitimisha kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha kesi kwa kiwango kinachotakiwa kisheria.

“Kwa kuzingatia hoja zote kwa ujumla, tunaruhusu rufaa, tunafuta hatia dhidi ya mrufani na kuamuru aachiliwe huru,” ilisema hukumu hiyo.