Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM), kimepanga kubadili mwelekeo wa utendaji wake, kutoka viongozi wa juu kutoa maelekezo kwa wale wa chini badala yake viongozi wa mashina watapokea shida za wananchi na kuzipeleka juu kwa utekelezaji.
Hatua hiyo kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Asha-Rose Migiro, inalenga kuhuisha utendaji na kukiweka chama hicho karibu na jamii, ili kuendelea kulinda wanachama kilionao.
CCM inakuja na maelekezo hayo, katika kipindi ambacho kumekuwa na malalamiko kupitia mitandao ya kijamii kuwa, hakiwajali wananchi.
Hata hivyo, kwa nyakati na majukwaa tofauti viongozi wa chama hicho, wamekuwa wakisisitiza utendaji wao unalenga kuwanufaisha wananchi.
Hayo yameelezwa leo, Jumatano Januari 7, 2025 na Dk Migiro katika hotuba yake aliyoitoa kwenye kikao kazi na viongozi wa chama hicho wa mashina, matawi na kata za Wilaya za Temeke na Kigamboni, jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa CCM, Dk Asha-Rose Migiro akizungumza leo Januari 7, 2026 wakati wa kikao cha viongozi wa chama hicho wa mashina, matawi na kata za Wilaya za Temeke na Kigamboni, jijini Dar es Salaam.
Amesema viongozi hao wa chini waache utaratibu wa kusubiri amri na maelekezo ya utendaji kutoka juu, badala yake wapokee changamoto za wananchi na kuzipeleka juu kwa ajili ya utekelezaji.
“Sisi tutapenda kufahamu kutoka chini na kujua kwamba hili na lile linafanyika. Sisi amri yetu inatoka chini na sio juu kushusha chini,” amesema.
Amesema yote hayo yanalenga kukiimarisha na kukijenga chama hicho na kuendelea kulinda mtaji wa wanachama kinaojivunia.
Katika ujenzi wa chama, Dk Migiro amesema ni muhimu viongozi wa mashina na wengine wote nchi nzima kujenga uhusiano mwema na lugha nzuri kwa wananchi na jamii kwa ujumla.
“Katika hamasa zetu, kazi zetu na kuwatumikia Watanzania basi tuwe karibu sana na jamii, tujue kwamba matatizo yao ni matatizo yetu,” amesema.
Amesema viongozi wa chama hicho wanapokuwa karibu na jamii, watajenga ushirikiano mwema na hatimaye kutakuwa na mshikamano wa kitaifa.
Amewataka viongozi hao kuwa wepesi kushirikiana na Serikali na kusikiliza yanayotokana na utekelezaji wa ilani ya CCM.
Ili kuisimamia vema Serikali, amesema lazima wakati wote wawe na ilani ya kitaifa na zile za ngazi za chini za mikoa na wilaya husika.
Amesema kuisimamia Serikali ni kuwakumbusha viongozi yaliyoahidiwa kupitia ilani, taarifa ziwe zinatolewa na viongozi wawe wanazungumzia utekelezaji.
Amesema CCM ina bahati ya kuwa na vitega uchumi ambavyo vinalenga kufanya shughuli za kuinufaisha, hivyo viongozi wavilinde na wasijinufaishe navyo.
Sambamba na hilo, amesema ziara yake mashinani imetokana na kutambua kuwa, mshina ndiyo moyo wa chama hicho na humo ndiko uliko uhai na umadhubuti.
Amesema wamekubaliana katika sekretarieti kwamba ziara yake ya kwanza ianzie ngazi ya mashina na wako tayari kusikia ushauri wa namna gani bora ya kushirikiana nao ili kupokea taarifa za kina.
Dk Migiro amesema wanapokwenda kukiimarisha chama hicho ni wajibu wao kurejea baadhi ya mambo mazuri yaliyofanywa na chama hicho.
Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenan Kihongosi akizungumza leo Januari 7, 2026 wakati wa kikao cha viongozi wa chama hicho wa mashina, matawi na kata za Wilaya za Temeke na Kigamboni, jijini Dar es Salaam.
Amesema zamani kulikuwa na madarasa ya itikadi yaliyokuwa yanawaeleza walipotoka na wanapokwenda na hata viongozi wanajua uhalisia wa historia ya chama.
Amesisitiza wazee watumike kutoa madarasa hayo ya itikadi ili kuzalisha viongozi bora.
Awali, akizungumza kumkaribisha Dk Migiro, Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenan Kihongosi amewaelekeza viongozi wa chini wa chama hicho kujibu upotoshaji wowote unaotolewa dhidi ya chama hicho.
Amewasisitiza wasiwe wanyonge, kwa kuwa wapotoshaji wengi hawapo nchini na kwamba viongozi watumie nafasi zao kujibu upotoshaji bila kuogopa.
“Hatuwezi kuwa viongozi wa kuogopa watu wa chama kingine. Siku hizi wanakishambulia chama chetu ili wakichafue. Wapinzani wetu wa kisiasa, tukae tufanye siasa zenye sera, umoja katika nchi si kwenda kuharibu Taifa,” amesema.
Amesema viongozi hao hawana sababu ya kuogopa kukisemea chama hicho kwa kuwa kimefanya kazi kubwa tangu kuasisiwa kwake.
Amesema anaamini ziara hiyo ya Dk Migiro kwa viongozi wa ngazi ya chini wa CCM, itarudisha matumaini kwa viongozi wa mashina na nafasi nyingine.
Ameeleza ni muhimu wanachama wa chama hicho kutumia muda huo kuhubiri utekelezaji wa yale yaliyoahidiwa wakati wa kampeni za uchaguzi.
“Wenzetu wanaleta maneno mengi, chokochoko nyingi, wanafanya upotoshaji, ili watuondoe kwenye reli, lakini hawatatuondoa,” amesema.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema kwa miaka kadhaa wananchi wa mkoa huo wamekuwa na malalamiko ya kufungwa kwa barabara kila mvua inaponyesha.
Amesema maeneo zaidi yanayolalamikiwa ni Jangwani, Kigogo na Mkwajuni na kwamba tayari Serikali imeshatoa fedha za kuhakikisha kote kunajengwa madaraja kuyakabili hayo.
Kwa upande wa Jangwani, amesema daraja hilo linajengwa kwa Sh6.7 bilioni na litakuwa na urefu wa mita 300, huku ujenzi wa madaraja ya Kigogo na Mkwajuni ukiendelea.
Ameeleza eneo la Mbagala nako ulipo Mto Mzinga kumekuwa na shida na baadhi ya watu wamepoteza maisha, lakini sasa zimetolewa Sh54 bilioni kwa ajili ya ujenzi wake.
Chalamila amesema barabara kutoka Kibada hadi Kimbiji yenye urefu wa kilomita 41, zimetolewa zaidi ya Sh95 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami.
Amesema Januari mwaka huu wanafunzi wanatakiwa kuanza kidato cha kwanza kwa Dar es Salaam pekee ni 95,323, huku wa daraja la kwanza wakiwa zaidi ya 100,032
Kwa idadi hiyo ya wanafunzi, amesema Dar es Salaam ilipaswa kuwa na madarasa 1,906 ili kukidhi haja ya wote, na tayari Serikali imejenga madarasa 1,908 hivyo yanatosha na kuna ziada.
Amesema tayari wameshapiga marufuku michango holela shuleni isipokuwa itolewe kwa makubaliano kupitia vikao kati ya shule na wazazi wa wanafunzi.
Ametumia jukwaa hilo, kuahidi kuulinda Mkoa wa Dar es Salaam, huku akiwataka wananchi kukaa jijini humo kwa amani na wafanye siasa za majibizano ya hoja na atakayevunja amani atashughulikiwa.
