Licha ya ripoti na madai yanayoendelea kusambaa kuhusu juhudi za Marekani kumkamata Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro, mjadala huo umeibua upya kumbukumbu za operesheni za kijeshi zilizowahi kutekelezwa na taifa hilo katika nyakati tofauti za kisiasa na historia ya dunia.
Kinachozitofautisha operesheni hizo si ukubwa wa nguvu za kijeshi zilizotumika pekee, bali pia muda uliotumika kuyafikia malengo husika, mabadiliko ya kisiasa kuanzia operesheni zilizochukua wiki kadhaa hadi zile zilizotekelezwa kwa dakika chache tu.
Kwa mfano, operesheni iliyolenga kumkamata Rais wa Venezuela, Nicolás Maduro, iliripotiwa kuchukua takriban saa mbili na nusu tu, ikitajwa kuwa ya kushtukiza na yenye kasi kubwa.
Hii inatofautiana kwa kiasi kikubwa na operesheni ya kumwondoa madarakani kiongozi wa Panama, Manuel Noriega, iliyochukua siku 15 tangu Desemba 20, 1989 hadi Noriega alipojisalimisha Januari 3, 1990, baada ya kujificha katika ubalozi wa Vatican mjini Panama City.
Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro akiwa chini ya ulinzi jijini New York nchini Marekani. Picha na Mtandao
Kwa upande mwingine, operesheni iliyomuua kiongozi wa mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda, Osama bin Laden, imeendelea kutajwa kama moja ya operesheni za kijeshi zilizotekelezwa kwa muda mfupi zaidi, lakini zenye athari kubwa duniani.
Uvamizi huo uliofanyika Mei 2, 2011 katika mji wa Abbottabad, kaskazini mwa Pakistan, ulichukua takriban dakika 40 pekee, tangu wanajeshi wa Marekani walipotua, kumuua Osama na kubeba mwili wake na kuondoka nao eneo la tukio.
Mifano hii mitatu inaonesha kwa uwazi jinsi mikakati ya kijeshi ya Marekani imekuwa ikibadilika kulingana na mazingira ya kisiasa, kiusalama na kidiplomasia, huku muda wa operesheni ukiwa mdogo au mrefu, lakini athari zake zikibaki kuwa za kudumu katika historia ya dunia.
Januari 3, 2026, Marekani ilihitimisha mpango wa muda mrefu wa kumwondoa madarakani Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro kutokana na uhusiano mbaya ambao amekuwa nao na Marekani inayomtuhumu kujihusisha na uhalifu ikiwamo uingizaji wa dawa za kulevya.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), kwa miezi kadhaa, majasusi wa Marekani walikuwa wakifuatilia kwa karibu kila hatua ya Rais Maduro kabla ya kutekeleza mkakati huo wa kumtia nguvuni.
Kikosi kidogo, kikihusisha chanzo kimoja ndani ya Serikali ya Venezuela, kilikuwa kikifuatilia mahali alikolala kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 63, chakula alichokula, mavazi aliyovaa na hata, kwa mujibu wa maofisa wa juu wa kijeshi na hata “wanyama wake wa kufugwa”.
Hatimaye, mwanzoni mwa Desemba, operesheni iliyopewa jina la Operation Absolute Resolve ilikamilishwa.
Mpango huo ulikuwa matokeo ya miezi kadhaa ya mipango ya kina na mazoezi, yaliyohusisha hata wanajeshi wa kikosi maalumu cha Marekani kujenga mfano kamili wa nyumba salama ya Maduro jijini Caracas ili kufanya majaribio ya njia za kuingia.
Mpango huo uliokuwa ni uvamizi wa kijeshi wa Marekani katika Amerika ya Kusini ambao haujawahi kushuhudiwa tangu enzi za Vita Baridi ulihifadhiwa kwa usiri mkubwa.
Bunge la Marekani (Congress) halikufahamishwa wala kushirikishwa kabla. Baada ya kila kitu kukamilika, kilichobaki kwa viongozi wa kijeshi kilikuwa ni kusubiri mazingira mwafaka ya kuanza operesheni.
Walilenga kuongeza mshangao kwa kiwango cha juu, maofisa walisema Jumamosi. Kulikuwa na jaribio la awali siku nne kabla Rais wa Marekani, Donald Trump, kuidhinisha mpango huo, lakini waliamua kusubiri hali bora ya hewa na kupungua kwa mawingu.
“Katika wiki zilizopita hadi Krismasi na Mwaka Mpya, wanaume na wanajeshi wa Marekani walikuwa tayari, wakisubiri kwa subira masharti sahihi yatimie na rais atoe amri ya kuchukua hatua,” alisema Jenerali Dan Caine, ofisa wa juu zaidi wa kijeshi nchini humo, katika mkutano na waandishi wa habari Jumamosi asubuhi.
Amri ya kuanza operesheni ilitolewa saa 4:46 usiku kwa saa za Mashariki mwa Marekani, Ijumaa (saa 03:46 GMT Jumamosi).
“Tulikuwa tumejiandaa kuifanya siku nne zilizopita, siku tatu, siku mbili zilizopita, lakini ghafla mazingira yakawa sawa. Tukasema: nendeni,” alisema Trump katika mahojiano na Fox & Friends, Jumamosi, saa chache baada ya uvamizi huo wa usiku.
“Alituambia na tunathamini hilo…bahati njema na mwendo mwema,” alisema Jenerali Caine. Amri ya Trump ilitolewa muda mfupi kabla ya saa 6 usiku mjini Caracas, hali iliyowawezesha wanajeshi kufanya operesheni kwa kutumia giza.
Kilichofuata kilikuwa ni operesheni ya saa mbili na dakika 20 kupitia anga, nchi kavu na baharini, iliyowashangaza wengi Marekani na duniani kote.
Kwa ukubwa na usahihi wake, operesheni hiyo ilikuwa nadra kushuhudiwa, na ilikosolewa mara moja na baadhi ya mataifa ya eneo hilo.
Aliyekuwa rais wa Venezuela, Nicolás Maduro, na mkewe Cilia Flores wakiwa chini ya ulinzi baada ya kushushwa kwenye helikopta kituo cha Manhattan, Marekan huku wakisindikizwa na maofisa usalama wakati wa kufikishwa katika Mahakama ya Shirikisho ya Manhattan, jana Januari 5, 2026. Picha na Mtandao
Rais wa Brazil, Luiz Inácio Lula da Silva, alisema kukamatwa kwa nguvu kwa kiongozi wa Venezuela kuliweka “mfano mwingine hatari sana kwa jumuiya ya kimataifa”.
Trump hakufuatilia operesheni hiyo kutoka chumba cha dharura cha Ikulu ya White House. Badala yake, alikuwa katika klabu yake ya MaraLago, Florida, akiwa na washauri wake, akitazama tukio hilo mubashara akifuatana na Mkurugenzi wa CIA, John Ratcliffe na Waziri wa Mambo ya Nje, Marco Rubio.
“Kilikuwa kitu cha ajabu kuona,” alisema Trump. “Nilikuwa naangalia kana kwamba ni kipindi cha televisheni. Na kama ungeona kasi, nguvu… ilikuwa kazi ya kushangaza. Ni kazi ya kushangaza wamefanya watu hawa.”
Katika miezi ya karibuni, maelfu ya wanajeshi wa Marekani wamepelekwa eneo hilo, wakijiunga na manowari ya kubeba ndege za kivita na meli nyingi za kivita katika mkusanyiko mkubwa wa kijeshi ambao haujashuhudiwa kwa miongo kadhaa.
Trump amekuwa akimtuhumu Maduro kwa biashara ya dawa za kulevya na ugaidi wa mihadarati.
Dalili za awali za Operation Absolute Resolve zilianza angani. Zaidi ya ndege 150 ikiwamo mabomu, ndege za kivita na za upelelezi zilitumika katika operesheni hiyo, kwa mujibu wa maofisa wa Marekani.
Milipuko mikubwa ilisikika mjini Caracas takriban saa 08:00 usiku kwa saa za huko huku moshi mzito ukionekana kupaa angani. Wakazi walisema ndege na helikopta zilikuwa zikizunguka juu ya jiji.
Baadaye, video zilizosambaa mitandaoni zilionyesha ndege nyingi angani na athari za milipuko. BBC Verify imethibitisha maeneo matano yaliyolengwa, yakiwamo Kambi ya Jeshi la Anga ya Generalissimo Francisco de Miranda (La Carlota) na Bandari ya La Guaira.
Baadhi ya mashambulizi yalilenga mifumo ya ulinzi wa anga na malengo mengine ya kijeshi. Trump pia alidai kuwa Marekani ilizima umeme mjini Caracas kabla ya operesheni kuanza. “Kulikuwa na giza na kulikuwa na maangamizi,” alisema.
Wakati mashambulizi yakiendelea, vikosi vya Marekani viliingia mjini, vikiwamo wanachama wa kikosi maalumu cha Delta Force. Walikuwa na silaha nzito na vifaa maalumu vya kuvunja milango ya chuma ya nyumba salama ya Maduro.
Kwa mujibu wa Jenerali Caine, wanajeshi walifika katika makazi ya Maduro muda mfupi baada ya mashambulizi kuanza. Trump alisema eneo hilo lilikuwa kama ngome ya kijeshi na kwamba walipokaribia, walikabiliwa na upinzani.
Hatimaye, wanajeshi walifanikiwa kumkamata Maduro pamoja na mkewe, Cilia Flores. Rubio alianza kuwataarifu wabunge wakati operesheni ikiendelea, jambo lililozua hasira kwa baadhi ya wabunge wa Marekani.
Waziri wa Ulinzi wa Venezuela alisema wanajeshi na raia kadhaa waliuawa katika operesheni hiyo. Hata hivyo, Marekani ilisema hakuna mwanajeshi wake aliyefariki duniani.
Ifikapo saa 04:20 asubuhi Jumamosi kwa saa za huko, helikopta ziliondoka Venezuela zikiwa zimembeba Maduro na mkewe chini ya ulinzi wa Wizara ya Sheria ya Marekani, wakielekea New York kukabiliana na mashtaka ya jinai.
Takribani saa moja baadaye, Trump alitangaza rasmi kukamatwa kwa Maduro. “Maduro na mkewe hivi karibuni watakabiliwa na nguvu kamili ya mkondo wa haki wa Marekani,” alisema.
Maandalizi ya operesheni hiyo yalikuwa yakiendelea kwa miezi kadhaa huku kuwasili kwa manowari ya kubeba ndege za kivita za Marekani ijulikanayo kama USS Gerald R. Ford, Novemba mwaka jana, likiwa hatua muhimu.
Kwa mujibu wa The Conversation, hatua hiyo iliipa Marekani uwezo wa kufanya mashambulizi mengi dhidi ya malengo ya nchi kavu, na kuiongezea nguvu ya silaha za kijeshi iliyokuwa tayari imewekwa katika eneo la Caribbean.
Rais wa mpito wa Venezuela, Delcy Rodríguez (wa tatu kusho) akiwa katika kikao cha ndani na maofisa waandamizi wa nchi hiyo leo Jumatatu Januari 5, 2025. Picha na Mtandao
Manowari hiyo iliungana na kikosi cha kijeshi cha Iwo Jima Amphibious Ready Group, kilichojumuisha meli ya kubeba helikopta na meli mbili za kutua wanajeshi.
Aidha, waharibifu (destroyers) sita na meli mbili kubwa za kivita (cruisers) ziliwekwa katika eneo hilo, zikiwa na uwezo wa kurusha mamia ya makombora kwa ajili ya kushambulia ardhini na kujilinda dhidi ya mashambulizi ya angani.
Pia, kulikuwepo meli maalumu ya kuongozea operesheni za vikosi maalumu.
Idhini ya Rais Trump kwa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) kufanya operesheni za siri nchini Venezuela inaelezwa kuwa ilikuwa sababu nyingine muhimu.
Inaaminika kuwa watu waliokuwa ndani ya Venezuela walichukua nafasi muhimu sana, si tu katika kukusanya taarifa za kijasusi, bali pia kushirikiana na maofisa muhimu ndani ya jeshi na serikali ya Maduro, ili kuhakikisha hatua fulani zinafanyika au hazifanyiki katika nyakati mahsusi wakati wa operesheni ya Januari 3.
Kwa mipango na maandalizi hayo yote kuwa yamekamilika kufikia Desemba, inaaminika jeshi la Marekani lilikuwa tayari kutekeleza operesheni hiyo, lakini lililazimika kusubiri mazingira yanayofaa ili kuongeza uwezekano wa mafanikio.
Kwa ujumla, kuna mambo matatu muhimu yaliyofanikisha operesheni hiyo kwa wakati mwafaka: upatikanaji wa taarifa sahihi za kijasusi, uwepo wa ushirikiano wa kuaminika ndani ya nchi lengwa, na mazingira mazuri ya kiufundi na kijeshi.
Rais wa mpito wa Venezuela, Delcy Rodríguez. Picha na Mtandao
Taarifa za kijasusi zilikuwa nguzo kuu. Trump alikiri Oktoba kwamba alikuwa ameidhinisha CIA kufanya operesheni za siri nchini Venezuela, na kufikia mwisho wa mwaka, wachambuzi walikuwa wamekusanya taarifa muhimu zilizohitajika ili operesheni hiyo ifanikiwe.
Taarifa hizo zilipaswa kujumuisha kujua kwa uhakika mahali Rais Maduro angekuwa wakati wa operesheni na hali iliyomzunguka.
Katika miezi iliyopita, kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari, jumuiya ya kijasusi ilikuwa na mawakala waliokuwa ndani ya Venezuela, wakifanya mazungumzo na watu ndani ya jeshi, uongozi wa Chavista na wengine waliokuwa na taarifa nyeti au waliokuwa na nafasi ya kushawishi mwenendo wa matukio.
Hiyo ilihusisha, kwa mfano, kuzima mifumo fulani, kuzuia vikosi vya kijeshi kuchukua hatua, au kuhakikisha maofisa fulani hawapo kazini katika wakati muhimu.
Ripoti ya The New York Times inaeleza kuwa Marekani ilikuwa na chanzo cha karibu sana na Maduro, kilichotoa taarifa za maisha yake ya kila siku, hadi kufahamu chakula alichokula.
Kwa upande wa mazingira ya kiufundi, hali ya hewa ilikuwa muhimu. Hakukuwa na nafasi ya dhoruba, upepo mkali au mawingu mazito ambayo yangeweka ndege za Marekani hatarini zilipokuwa zikiruka katika njia hatarishi za chini kupitia milima inayotenganisha Fort Tiuna kambi ya kijeshi mjini Caracas ambako Maduro alikamatwa na ukanda wa pwani.
