KOCHA Mkuu wa Azam FC, Florent Ibenge ameonekana mwenye furaha zaidi baada ya kushuhudia kiungo wa timu hiyo, Adolf Mtasingwa, akirejea rasmi uwanjani baada ya kukaa nje ya uwanja kwa takribani miezi kumi kutokana na majeraha ya kifundo cha mguu.
Mtasingwa anayecheza nafasi ya kiungo mkabaji, mara ya mwisho kuonekana uwanjani ilikuwa Februari 15, 2025 katika mechi ya Ligi Kuu Bara ambayo Azam ilishinda mabao 2-0 dhidi ya Mashujaa.
Juzi Jumatatu katika mechi ya kuhitimisha hatua ya makundi katika Kombe la Mapinduzi ambapo Azam ilishinda 2-1 dhidi ya URA kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja, kiungo huyo aliingia dakika ya 77 kuchukua nafasi ya Himid Mao.
Akizungumzia kurejea kwa Mtasingwa, Ibenge amesema: “Kwanza nina furaha kubwa kuona amerejea kwa sababu ni muda mrefu hakucheza, ukiangalia katika timu yetu yeye ni miongoni mwa wachezaji viongozi.
“Katika timu unapokuwa na wachezaji wachanga lazima wakubwa wawepo kuwaongoza katika njia nzuri. Yeye na Himid wamekuwa wakiwaongoza wenzao vizuri, hivyo kurejea kwake ni jambo zuri na inaongeza kitu kuelekea mechi yetu ya CAF dhidi ya Nairobi United ambayo tunahitaji kushinda.”
Januari 25, 2026 na Februari 1, 2026, Azam itacheza dhidi ya Nairobi United katika mechi za kundi B kwenye Kombe la Shirikisho Afrika ikianzia ugenini nchini Kenya, kisha New Amaan Complex, Unguja. Timu zote hazina pointi baada ya kupoteza mechi mbili za kwanza.
Kurejea kwa Mtasingwa kunaongeza wigo mpana eneo la kiungo cha kati ndani ya Azam kukiwa na ushindani zaidi kutokana na uwepo wa viungo wengine akiwamo Himid Mao, Sadio Kanoute, Yahya Zayd na James Akaminko hali inayompa jeuri Ibenge ya nani amtumie kutokana na mipango ya mechi husika.
