Dar es Salaam. Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imetoa onyo kwa watu wanaojihusisha na kazi za kihabari bila kuwa na ithibati halali, ikibainisha kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kukiuka Sheria ya Huduma za Habari.
Katika taarifa yake iliyotolewa leo, Jumatano Januari 7, 2026, JAB imesema katika utekelezaji wa majukumu yake ya kisheria imebaini kuwepo kwa watu wasio na sifa za kitaaluma na kisheria wanaotekeleza majukumu ya kihabari baada ya kukamilika kwa uchaguzi mkuu.
Bodi imeeleza imekuwa ikikumbusha mara kwa mara kuwa uandishi wa habari ni taaluma rasmi inayosimamiwa kwa misingi ya kisheria, maadili na weledi wa kitaaluma, na kwamba mtu yeyote anayejihusisha na kazi za kihabari bila ithibati anavunja masharti ya Kifungu cha 19 cha Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229 (Toleo la 2023).
“Kwa mujibu wa Kifungu cha 17(1)(a) cha Sheria ya Huduma ya Habari pamoja na Tangazo la Serikali Na. 18 la Februari 3, 2017, ithibati inahitajika kwa wahariri, waandishi wa habari, waandishi huru (freelancers), wapiga picha, wazalishaji wa vipindi na watangazaji wa redio na televisheni wanaofanya kazi katika vyombo vya habari,” imesema taarifa hiyo.
Kutokana na hali hiyo, JAB imetoa onyo kwa watu wote wanaofanya kazi za kihabari bila kuwa na ithibati kuacha mara moja, ikieleza kuwa kuendelea kufanya hivyo ni kosa kwa mujibu wa Kifungu cha 50(2)(b) cha Sheria ya Huduma za Habari.
Aidha, bodi hiyo inayosimamia waandishi wa habari nchini imesisitiza kuwa itachukua hatua stahiki za kisheria dhidi ya mtu au taasisi yoyote itakayobainika kuajiri au kuruhusu utekelezaji wa kazi za kihabari bila kuzingatia taratibu na masharti ya kisheria.
Vilevile, JAB imeutaarifu umma na wadau wa sekta ya habari kuwa katika kipindi cha hivi karibuni itaendesha ukaguzi maalumu katika vyombo vya habari na maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kujiridhisha kuwa wanaotekeleza majukumu ya kihabari wanakidhi vigezo vilivyowekwa kisheria.
Bodi hiyo imekumbusha kuwa utoaji wa ithibati kwa waandishi wa habari si kikwazo cha uhuru wa habari, bali ni nyenzo muhimu ya kulinda heshima na hadhi ya taaluma ya uandishi wa habari, kuongezea uaminifu wa taarifa zinazozalishwa na kusambazwa kwa umma, pamoja na kuwapambanua waandishi waliothibitishwa kisheria.
Taarifa hiyo iliyosaniwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Patrick Kipangula, imetoa wito kwa wote wenye nia ya kufanya kazi za kihabari kuhakikisha wanapata ithibati kwa mujibu wa sheria, wanazingatia maadili na weledi wa juu wa taaluma, na kutumia kalamu, sauti na majukwaa yao kwa kuwahudumia wananchi kwa kutoa taarifa sahihi, kukuza uwajibikaji na kuchangia maendeleo endelevu ya Taifa.
