Kauli za Trump zaendelea kutikisa dunia

Dar es Salaam. Wakati Rais wa Marekani, Donald Trump, akikiri wazi kuwa moja ya sababu zilizochochea operesheni ya kijeshi dhidi ya Venezuela ni mafuta, kiongozi huyo, ameendelea kutamani operesheni za kijeshi katika nchi zingine zikiwamo Colombia na Greenland.

Trump, ameendelea kuzua mjadala wa kimataifa baada ya kudokeza uwezekano wa kuendeleza sera ya upanuzi wa ushawishi wa Marekani katika ulimwengu wa Magharibi, kufuatia operesheni ya kijeshi iliyosababisha kukamatwa kwa aliyekuwa Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro.

Ameipa sera hiyo jina la “Don-roe Doctrine,” akirejea na kuibadilisha falsafa ya kihistoria ya Monroe Doctrine ya karne ya 19.

Monroe Doctrine (1823), ilianzishwa kama mwito wa kulinda ulimwengu wa Magharibi dhidi ya upenyaji wa Ulaya na kudumisha heshima ya ushawishi wa Marekani, bila kujihusisha na siasa za ndani za Ulaya.

Don‑roe Doctrine (2026): Ni jina linalotumika kuonyesha mwelekeo wa sera mpya inayoelekezwa na Trump, ikijikita zaidi katika udhibiti, ushawishi wa kiuchumi na kijeshi misukosuko ya kisiasa katika kanda.

Chini ya sera hiyo, Rais huyo ameongeza hofu zaidi baada ya kudai kuwa Marekani inaitaka Greenland kwa misingi ya usalama wa taifa, huku akitoa kauli kali zinazoashiria uwezekano wa kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya Serikali ya Colombia, pia akiituhumu kushindwa kudhibiti biashara ya dawa za kulevya.

Kauli hizo zimezidisha wasiwasi kuhusu mustakabali wa uhusiano wa Marekani na mataifa kadhaa, yakiwemo Iran, Cuba, akinuia kuchukua Mfereji wa Panama, kisiwa cha Greenland na hata kutaka kuigeuza Canada jimbo la 51 la Marekani, akidai hatua hizo ni muhimu kwa usalama wa taifa lake.

Akizungumza mwishoni mwa wiki, Trump alisema chini ya utawala wake, “utawala wa Marekani katika ulimwengu wa Magharibi hautahojiwa tena,” kauli iliyochukuliwa na wachambuzi kama ishara ya sera kali ya kuingilia masuala ya mataifa mengine.

Miongoni mwa maeneo yanayozua mjadala mkubwa ni Greenland, eneo lenye uhuru chini ya Denmark.

Trump amesema mara kadhaa kuwa kisiwa hicho ni muhimu kwa usalama wa taifa la Marekani, akidai uwepo wa Russia na China katika eneo hilo unatishia masilahi ya Marekani.

Hata hivyo, viongozi wa Denmark na Greenland wamesisitiza kuwa eneo hilo “haliuzwi” na mustakabali wake utaamuliwa na wakazi wake.

Katika Mashariki ya Kati, Trump ameionya Iran kwa kutumia nguvu dhidi ya waandamanaji wanaopinga hali mbaya ya kiuchumi, akisema Marekani iko tayari “kuchukua hatua kali” iwapo mauaji yataendelea.

Onyo hilo linakuja miezi michache baada ya Marekani kushambulia vituo muhimu vya nyuklia vya Iran katika juhudi za kudhoofisha mpango wake wa nyuklia.

Kwa upande wa Caribbean, Trump amesema Cuba “iko karibu kuporomoka,” akidai kuwa kupoteza msaada wa mafuta kutoka Venezuela kumeiathiri vibaya kiuchumi.

Kuhusu hilo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, ameongeza kuwa uongozi wa Cuba unapaswa kuwa na wasiwasi, kutokana na uhusiano wake wa karibu na utawala wa Maduro.

Colombia pia imejikuta katika orodha ya mataifa yanayolengwa na kauli za Trump.

Amemtuhumu Rais Gustavo Petro kwa kushindwa kudhibiti uzalishaji na biashara ya dawa za kulevya, akidokeza uwezekano wa hatua za kijeshi, madai ambayo Serikali ya Colombia imeyapinga.

Ingawa Trump amewahi kuitaja Canada kama “jimboni la 51,” kwa sasa mgogoro mkubwa umejikita kwenye ushuru mkubwa wa kibiashara ambao Marekani imeweka dhidi ya bidhaa za Canada.

Aidha, Rais huyo amewahi kudai kuwa Marekani inapaswa kurejesha udhibiti wa Mfereji wa Panama, madai yaliyokataliwa na Serikali ya Panama.

Hata hivyo, kauli hizo za Trump zimekabiliwa na upinzani kutoka Ulaya, ambapo viongozi wakuu wa bara hilo, wakiongozwa na Denmark, Ufaransa, Ujerumani na Uingereza, wametoa tamko la pamoja wakisisitiza kuwa usalama wa Greenland lazima uheshimu mamlaka ya nchi husika na matakwa ya wananchi wake.

Viongozi hao wamesisitiza kuwa Greenland ni sehemu ya Denmark na mwanachama wa Umoja wa Kujihami wa Nchi za Magharibi (NATO), hivyo haiwezi kuchukuliwa kwa nguvu.

Waziri Mkuu wa Denmark, Mette Frederiksen, ameonya kuwa jaribio lolote la uvamizi wa Greenland lingetishia mustakabali wa NATO, huku serikali ya Greenland ikiomba mkutano wa dharura na Marekani kujadili kauli hizo.

Kauli za Trump zimeendelea kuzua wasiwasi kuhusu mwelekeo wa diplomasia na usalama wa kimataifa.

Kauli ya Rais wa mpito wa Venezuela Delcy Rodríguez, kwamba nchi yake iko tayari kushirikiana na Marekani katika ajenda ya maendeleo ya pamoja kwa kuzingatia sheria za kimataifa, imeelezwa ni kupunguza mvutano na taifa hilo kubwa.

Mvutano huo uliongezeka zaidi baada ya Rais Trump kutangaza kuwa Marekani imefikia makubaliano ya kupata kati ya mapipa milioni 30 hadi milioni 50 ya mafuta kutoka Venezuela, akidai mapato yake yatasimamiwa na Ikulu ya Marekani kwa manufaa ya mataifa yote mawili.

Kwa mujibu wa takwimu za soko, mafuta hayo yanaweza kuwa na thamani ya hadi Dola 2 bilioni za Marekani.

Trump amekiri wazi kuwa moja ya sababu za operesheni ya kijeshi ilikuwa ni kufungua upya fursa za kiuchumi katika taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta.

Alisema pia kuwa Marekani itashirikiana na makampuni makubwa ya mafuta kama Exxon, Chevron na ConocoPhillips katika kujenga upya miundombinu ya nishati ya Venezuela, ingawa alikiri kuwa walipa kodi wa Marekani huenda wakabeba sehemu ya gharama.

Venezuela ni taifa lenye hifadhi kubwa ya mafuta duniani, likimiliki takriban mapipa bilioni 303 ya mafuta yaliyothibitishwa, sawa na karibu asilimia 17 ya hifadhi yote ya mafuta duniani, zaidi hata ya Saudi Arabia.

Hifadhi hizi kubwa, zilizoko hasa katika ukanda wa Orinoco, zinajumuisha aina ya mafuta ghafi na mafuta ghafi mazito ambayo ni ghali zaidi kuyachimba na yanahitaji miundombinu maalumu ya kuchakata kabla ya kusafirishwa au kutumika kimataifa.

Pamoja na utajiri huo wa rasilimali, uzalishaji wa mafuta wa Venezuela umeendelea kushuka kwa miaka mingi.

Hadi miaka ya 1970, nchi hiyo ilikuwa ikizalisha karibu mapipa milioni 3.5 kila siku, sawa na zaidi ya asilimia saba ya uzalishaji wa dunia.

Hata hivyo, uzalishaji sasa umepungua kwa kiasi kikubwa, ukiripotiwa chini ya mapipa milioni moja kwa siku, sawa na chini ya asilimia moja ya uzalishaji wa dunia.

Kupungua kwa uzalishaji kunachangiwa na mchanganyiko wa sababu zikiwamo usimamizi mbovu, ukosefu wa uwekezaji, miundombinu mibovu na vikwazo vya kimataifa, ikiwemo vikwazo vya Marekani na nchi nyingine.

Changamoto hizi zimefanya Venezuela, licha ya kuwa na hifadhi kubwa zaidi ya mafuta duniani, kusuasua katika uzalishaji na ushawishi wa soko la mafuta.

Nchi hiyo, ambayo ni mwanachama mwanzilishi wa OPEC, sasa haichangii kwa uzalishaji kwa kiwango kinacholingana na utajiri wake wa rasilimali, na imeshuka nafasi yake katika orodha ya wazalishaji wakuu duniani.

Mji mkuu wa Venezuela, Caracas, umeingia katika hali ya hofu baada ya kuibuka kwa makundi ya waendesha pikipiki wenye silaha nzito, wanaojulikana kama colectivos, wanaofanya doria katika mitaa mbalimbali ya jiji hilo wakiwasaka watu wanaodaiwa kumuunga mkono Rais wa Marekani, Donald Trump.

Hali hiyo imekuja sambamba na tangazo la Serikali la kutangaza hali ya hatari ya siku 90, likiwa na agizo la kuvitaka vyombo vya usalama kuanza mara moja msako wa kitaifa na kukamata watu wote wanaodaiwa kuunga mkono au kuchochea kile kinachoelezwa kama shambulio la kijeshi la Marekani dhidi ya Venezuela.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya kimataifa, hatua hiyo tayari imesababisha kukamatwa kwa waandishi wa habari 14, wakiwemo 11 raia wa kigeni, huku wengine wakiripotiwa kutoweka bila kujulikana walipo.

Makundi ya colectivos yanaripotiwa kusimamisha magari na kuanzisha vituo visivyo rasmi vya ukaguzi katika maeneo mbalimbali ya Caracas, wakikagua simu za raia kwa lengo la kubaini ujumbe au maudhui yanayoashiria kumuunga mkono Trump au Marekani.

Doria hizo zimeongeza hofu miongoni mwa wananchi, ambao baadhi yao wanasema wanaogopa kukamatwa au kuteswa kwa misingi ya mitazamo yao ya kisiasa, hali inayozidi kuzorotesha mazingira ya haki za binadamu nchini humo.