BEKI na nahodha wa Mtibwa Sugar, Oscar Masai amemtaja straika wa Yanga, Prince Dube kuwa ni hatari kwa kuwashughulisha mabeki uwanjani, akiufananisha uchezaji wake na staa wa zamani wa Simba, Emmanuel Okwi.
Dube ambaye amekuwa akifanya vizuri akiwa na kikosi cha Yanga alikuwa na kikosi cha timu yake ya Taifa ya Zimbabwe kwenye michuano ya AFCON 2025 ambako alifanikiwa kufunga bao moja inayoendelea nchini Morocco.
Staa huyo hapa nchini alianzia soka lake kwenye kikosi cha Azam ambapo baadaye aliondoka na kujiunga na Yanga ambako amekuwa akionyesha kiwango bora uwanjani.
Akizungumza na Mwanaspoti Masai amesema ingawa Dube anakosakosa mabao, lakini anapatikana maeneo mengi ya uwanjani na anaweza akawakusanya zaidi ya watu watatu kumkaba, hilo linawapa nafasi wachezaji wenzake kuwa huru na mpira.
“Umewahi kujiuliza kwa nini jina la Okwi lilikuwa linatajwa kwa ukubwa na kuogopwa na mabeki lakini hakuwa mshambuliaji anayechukua kiatu cha ufungaji bora zaidi ya msimu wa 2017/18 alipoibuka kinara wa mabao 20, sababu ni namna alivyokuwa anapatikana kila eneo la uwanja,” amesema Masai.
“Pia kwa nini Meddie Kagere wa Simba aliibuka mfungaji bora misimu miwili mfululizo 2018/19 mabao 23, 2019/20 mabao 22 aina ya uchezaji wake ulikuwa wa kukaa eneo la kufunga kama ilivyokuwa kwa Amisi Tambwe wakipata mipira wakiwa maeneo hayo lazima wafunge.
“ Dube anaonekana sehemu nyingi uwanjani na angekuwa ana uwezo wa kufunga mabao kwa umbali mrefu kama ilivyo kwa Feisal Salum ‘Fei Toto’ basi angekuwa ana idadi ya mabao mengi kila msimu, hivyo kwa upande wangu straika bora katika ligi hii kwa sasa ni Dube.”
Mbali na Masai, kipa wa Coastal Union, Wilbol Maseke amesema:”Kwa upande wangu Dube ni mshambuliaji hatari ninayemkubali nikiwa golini akiwepo uwanjani ni kati ya watu ambao nakuwa nao makini.”
