KONA YA MALOTO: Trump, Maduro, dawa za kulevya, mafuta ya Venezuela

Narcosobrinos ni maneno yaliyotumiwa na vyombo vya habari kutambulisha sakata la wapwa wa aliyekuwa Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro na mkewe, Cilia Flores, waliokamatwa na kilogramu 800 za cocaine Novemba 10, 2015.

Wapwa hao wa Rais Maduro, wanaitwa Efrain Antonio Campo Flores na Francisco Flores de Freitas. Walikamatwa na maofisa wa kikosi cha ujasusi cha kupambana na dawa za kulevya cha Marekani (DEA), walipokuwa Port-au-Prince, Haiti, wakijaribu kuingiza mzigo huo wa cocaine Marekani.

Novemba 18, 2016, wapwa hao wa Rais Maduro walikutwa na hatia. Maelezo yaliyotolewa mahakamani ni kuwa wapwa hao walikuwa wametumwa tu, kwamba wahusika ni Rais Maduro na mkewe Cilia ambaye wakati huo alikuwa Naibu Rais wa Bunge la Venezuela.

Ilielezwa kuwa fedha zitokanazo na mzigo huo wa cocaine zilikuwa kwa ajili ya kuisaidia familia ya Rais Maduro kuendelea kubaki madarakani. Ikaongezwa kuwa familia ya Rais Maduro inaongoza mtandao mpana wa unga ambao imeurithi na kuuendeleza kutoka kwa mtangulizi wake, Hugo Chavez.

Mhariri wa Washington Post, Jackson Diehl, alipata kuandika habari kuhusu mtandao mpana wa dawa za kulevya kwenye Serikali za Amerika Kusini, akasema kuwa Chavez na timu yake ya Serikali ya Mapinduzi ya Bolivarian, walikuwa wanaongoza genge hatari la wauza unga.

Kwa mujibu wa Diehl, mtandao wa Bolivarian, ulianza kutengeneza fedha nyingi miaka 1980 kutokana na dawa za kulevya, walipoanza harakati za kuchukua madaraka nchini Venezuela, na kwamba fedha nyingi walizopata ziliwezesha Chavez kushinda urais mwaka 1998.

Ilibainishwa kuwa mtandao huo ulioasisiwa na Chavez una nguvu kuliko genge lolote la unga katika Bara la Amerika Kusini kwa sababu lenyewe linamiliki Serikali. Hata baada ya Chavez kufariki dunia, mrithi wake, Maduro alikuwa akiendeleza ‘libeneke’. Hizo ni tuhuma tu!

Januari 3, 2026, ikiwa ni miaka 10, mwezi mmoja na siku 24 tangu wapwa wa Rais Maduro walipokamatwa, arobaini nayo ikatimia. Wanajeshi wa Marekani, kikosi cha Delta, walivamia Ikulu ya Venezuela, Miraflores Palace, Caracas, na kuwatwaa Maduro na Cilia, kisha kuwasafirisha hadi New York.

Januari 5, 2026, Maduro na Cilia, walifikishwa Mahakama ya Manhattan, New York, na kusomewa mashitaka mbalimbali ya usafirishaji wa dawa za kulevya, mbele ya Jaji Alvin Hellerstein. Maduro na Cilia walikana mashitaka yote. Wataendelea kukaa mahabusu Marekani, wakingoja hatima yao.

Mafuta na dawa za kulevya

Kwa muda mrefu, Maduro amekuwa akikana kuhusika na biashara ya dawa za kulevya. Isipokuwa, tuhuma hizo ni fitina za Marekani dhidi ya Serikali anayoiongoza. Huo ni utetezi wa Marekani.

Muda mfupi baada ya Maduro kunyakuliwa, Rais wa Marekani, Donald Trump, alitoa wito kwa kampuni za Marekani kukaa mkao wa kula. Alizitaka kampuni hizo kujiandaa kuwekeza mabilioni ya dola kwenye miradi ya mafuta Venezuela.

Bila kuchelewa, Shirika la Utangazaji wa Habar za Biashara Marekani (CNBC), lilifanya uchambuzi unaoeleza kuwa kuondolewa kwa Maduro madarakani na mabadiliko ya uongozi Venezuela ni fursa ya ukuaji kwa kampuni za mafuta za Marekani.

Uchambuzi wa CNBC, ulilenga kuanzia kampuni za Exxon Mobil na ConocoPhillips, ambazo mali zake zilitaifishwa na Serikali ya Venezuela chini ya Chavez, mwaka 2007 hadi Chevron, ambayo ni kampuni pekee ya mafuta ya Kimarekani inayoendelea na kazi ndani ya Jamhuri ya Bolivarian.

CNBC wameeleza kuwa ni wakati wa Exxon Mobil na ConocoPhillips, kurejeshewa mali zao na kuwekeza zaidi kwenye biashara ya mafuta Venezuela. Vilevile, wameainisha fursa za Chevron kukua na kupaa kibiashara kutokana na mazingira yaliyopo.

Inatosha kukusogeza kwenye mjadala kwamba Marekani kwa amri ya Trump, wametumia nguvu nyingi kuingia Venezuela, hususan ndani ya jiji la Caracas, wakaiteka Miraflores Palace, wakakata umeme jiji zima, wakaua watu makumi na kujeruhi, kisha kumtwaa Maduro kwa kisingizio kuwa anasafirisha dawa za kulevya kuingia Marekani.

Baada ya kumkamata Maduro, pamoja na mashitaka yanayoendelea dhidi yake na mkewe, lakini mjadala mkubwa siyo tena dawa za kulevya ambazo ndizo zilizotafutiwa uhalali wa uvamizi, hivi sasa kinachotazamwa zaidi ni utajiri wa Venezuela. Tambua kwamba Venezuela ndiyo nchi inayoongoza ulimwenguni kwa hifadhi kubwa ya mafuta ghafi.

Asilimia 18.17 ya mafuta yote ulimwenguni yanapatikana Venezuela. Kwa utajiri wa mafuta, Venezuela ina hifadhi ya mapipa takriban bilioni 300, ikifuatiwa na Saudi Arabia yenye asilimia 16.15 (mapipa bilioni 266). Hifadhi ya mafuta ya Iran na Iraq ukiyaweka pamoja, ndiyo unaweza kuifikia Venezuela.

Tamko la Trump kwamba Marekani itaiongoza Venezuela na kuweka sawa miundombinu ya mafuta. Wito wa kampuni za Marekani kuwekeza katika biashara ya mafuta Venezuela. Mpaka hapo jibu unalo. Je, nguvu kubwa iliyotumika kumnyakua Maduro, ni dawa za kulevya au utajiri wa mafuta Venezuela?

Dawa za kulevya na Marekani

Tangu Januari 2025, Trump alipokula kiapo kuiongoza Marekani kwa muhula wa pili, alimfanya Maduro kuwa shabaha yake. Kwanza aliongeza dau kwa yeyote ambaye angetoa taarifa ambazo zingewezesha Maduro kupatikana.

Trump alimlaumu Maduro kwa kusababisha ongezeko la wahamiaji Marekani. Pasipo kutoa uthibitisho, Trump alisema kuwa Maduro alikuwa akiwaachilia wafungwa wa Venezuela na kuwaelekeza kuhamia Marekani.

Kuhusu dawa za kulevya, ni kweli, Marekani ni taifa linaloathirika zaidi na biashara ya dawa za kulevya. Marekani imekuwa soko kuu la magenge ya wauza unga wa Amerika Kusini. Colombia ndiyo nchi inayoongoza kwa uzalishaji wa cocaine ulimwenguni, na sehemu kubwa ya dawa hizo huingizwa Marekani.

Colombia ni jirani zaidi na Marekani. Nchi hizo zinapakana. Venezuela ipo mbali kidogo. Swali linafuata, ikiwa vita inahusu dawa za kulevya, kwa nini Marekani isiivamie Colombia na kubadili utawala kwa sababu unashindwa kudhibiti magenge ya wauza dawa za kulevya? Colombia hifadhi yake ya mafuta ni mapipa bilioni mbili. Unakwenda kwenye bilioni mbili badala ya bilioni 300?