Musoma. Zaidi ya mabinti 200 wamenusurika kukeketwa wilayani Tarime, Mkoa wa Mara baada ya kuokolewa na kituo cha Nyumba Salama kilichopo Butiama mkoani humo.
Mabinti hao wamenusurika kufanyiwa vitendo hivyo katika msimu wa ukeketaji uliofanyika mwaka 2025, ukihusisha ukoo wa Wairegi ambao ni miongoni mwa koo 13 za kabila la Wakurya.
Takwimu hizo zimetolewa mjini Musoma jana Jumanne Januari 6, 2026 na Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Rhobi Samuel alipokuwa akichangia mada kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri (RCC) mkoani Mara kuhusu vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto mkoani humo.
Rhobi amesema licha ya mabinti hao kuokolewa wapo mabinti wengine wengi ambao idadi yao haijapatikana, ambao wameketetwa katika msimu huo.
“Ukeketaji umefanyika sana mwaka jana na mbali na mabinti pia wapo wanawake wawili waliokamatwa na kulazimishwa kukektewa bila ridhaa yao,” amesema.
“Mwaka jana wamekeketa ukoo mmoja peke yake, ambao ni Wairegi na hao wameamua kukeketa katika mwaka ambao haugawanyiki kwa mbili, wakiamini wakiwafanyia mabinti zao ukeketaji kwa pamoja na koo zingine 12, hawa wa kwao wanakufa sana,” amesema.
Amesema kutokana na ukeketaji uliofanyika mwaka jana zipo dalili za ukeketaji kufanyika kwa kiwango kikubwa zaidi mwaka huu, ukihusisha koo zingine 12 ambazo hufanya hivyo kwa mwaka unaogawanyika kwa mbili.
Hivyo ametoa wito kwa hatua za haraka kuchukuliwa ili kuwanusuru mabinti kufanyiwa ukatili huo.
Mbunge wa Tarime Vijijini (CCM), Mwita Waitara amesema suala la ukeketaji linahusisha imani na mila na limekuwa likifanyika kwa miaka mingi, hivyo ni vigumu kulimaliza ndani ya muda mfupi.
“Ukeketaji umeanza kufanyika miaka ya 1800 hadi sasa, ni tatizo ambalo huwezi kulimaliza ndani ya muda mfupi, nashauri elimu iendelee kutolewa kwa kulenga wahusika wenyewe na taratibu mambo yatabadilika,” amesema.
Kwa upande wake, Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mara, Neema Ibamba amesema jitihada mbalimbali zimefanywa na wadau kwa kushirikiana na Serikali katika kutokomeza vitendo hivyo, lakini cha kushangaza vimekuwa vikiendelea.
“Tumeshirikisha makundi mbalimbali katika jamii hadi mangariba tumewaweka kwenye vikundi na kuwapatia mikopo isiyokuwa na riba, ili waweze kuwa na shughuli rasmi za kujipatia kipato lakini masuala haya ya ukeketaji bado yanaendelea,” amesema.
Kufuatia haki hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mara (RCC), Kanali Evans Mtambi ameagiza kufanyika kwa midahalo, makongamano na mijadala katika jamii ili kujenga uelewa wa pamoja juu ya madhara ya ukatili.
Amesema midahalo hiyo itakayokuwa endelevu ianze kufanyika mapema kabla ya Januari 30 mwaka huu ikiwa ni njia mojawapo ya kuzuia ukeketaji baadaye mwaka huu.
“Pia naagiza suala la madhara ya ukeketaji kuwa ajenda ya kudumu katika vikao vyote vya kiserikali katika jamii zinazofanya vitendo hivi kiongozi yeyote wa kiserikali atakapokuwa kwenye mikutano au vikao kwa ngazi yoyote azungumzie suala hilo,” amesema Kanali Mtambi.
Amesema kwa hali ilivyo, suala la elimu kuhusu madhara ya ukeketaji ni moja ya silaha muhimu katika kupambana na vitendo hivyo na kwamba elimu hiyo inatakiwa kutolewa kuanzia ngazi ya chini bila kuchoka.
“Mila zilizopitwa na wakati bado ni kikwazo, njia kuu na nzuri ya kuzishughulikia ni elimu, tusiogope kusema nao ni jukumu letu kufanya hivyo, tutoe elimu mara kwa mara na hakika wataelewa na kuacha,” amesema Kanali Mtambi.
