Mitandao ya kijamii ilivyogeuka uwanja wa ukatili

Dar es Salaam. Mitandao ya kijamii iliyokuwa ikisifika kuwa nyenzo yenye nguvu ya kuunganisha watu, kujieleza na kufungua fursa za kiuchumi, sasa inazidi kubadilika na kuwa uwanja wa uhasama kwa Watanzania wengi.

Majukwaa ya kidijitali yaliyokuwa yakiahidi ujumuishaji, sauti kwa wote na ushiriki mpana, yamegeuka kuwa uwanja mpya wa unyanyasaji, matusi na unyonyaji, hali inayowaathiri zaidi watoto, vijana na wanawake.

Baadhi ya watu wanasema kwa sasa, mitandao ya kijamii si chombo tena cha mawasiliano au biashara pekee, bali na uhalifu pia.

Watumiaji wengi kwa sasa wanasema mitandao ya kijamii si jukwaa la kutoa maoni, kushiriki picha, kutangaza fursa, biashara au kuchapisha maudhui ya kitaalamu pekee, bali inabeba hatari kubwa ya unyanyasaji wa kijinsia.

Wapo wanaosimulia kushambuliwa kwenye sehemu za maoni, kurushiwa matusi, kutumiwa lugha ya wazi ya kingono au kukumbwa na mashambulizi ya mtandaoni yaliyopangwa kwa makusudi.

Baadhi ya watu wanasema vitendo hivyo huanzia kwenye maneno ya kejeli na kuishia kwenye vitisho, kulazimishwa au hofu ya kudhuriwa.

Matokeo ya hali hiyo sasa inawafanya watumiaji wengi kulazimika kuzima sehemu za maoni, kufuta machapisho na kufunga akaunti au kujiondoa kabisa kwenye ushiriki mtandaoni.

Kwa maoni ya baadhi ya waathirika, ukimya umeonekana kuwa ndiyo njia pekee ya kujilinda dhidi ya ukatili unaozidi kushamiri katika mazingira ya kidijitali.

Hata hivyo, baadhi ya wataalamu wanasema hali hiyo inaambatana na ongezeko kubwa la upatikanaji wa intaneti nchini.

Inaelezwa hadi mwanzoni mwa 2025, Tanzania ilikuwa na takribani na watumiaji milioni 6.75 wa mitandao ya kijamii, huku asilimia 19 ikiwa ni watu wazima.

Lakini inaelezwa hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huo, idadi ilipanda hadi takribani milioni 7.95 ya watumiaji ikiwa ni ishara ya kasi ya wananchi kukumbatia teknolojia ya kidijitali.

Facebook inaendelea kuongoza kwa matumizi ikifuatiwa na Instagram na YouTube, huku TikTok ikipata umaarufu mkubwa miongoni mwa vijana.

Hata hivyo, sambamba na upanuzi huo, upande wa giza wa mwingiliano wa mtandaoni umejitokeza wazi.

Kinachoanza kama matusi ya maneno, mara nyingi hubadilika kuwa vitisho, unyanyasaji wa kingono hasa kwa watoto na ukatili wa kijinsia unaofanikishwa na teknolojia.

Wataalamu wanaonya kuwa kasi, upeo na hali ya kutokujulikana inayotolewa na mitandao ya kijamii huzidisha madhara, kuruhusu unyanyasaji kusambaa kwa haraka huku waathirika wakishindwa kujinasua.

Uchunguzi wa Gazeti la The Citizen uliofanywa mwaka uliopita unaonesha tabia hiyo iliongezeka kwa kiwango kikubwa wakati wa uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba, 2025 na imeendelea kushamiri hata baada ya uchaguzi. Wachambuzi wanasema majukwaa ya kidijitali mara nyingi huakisi na hata kukuza mvutano wa kijamii, mapambano ya madaraka na ukosefu wa usawa uliopo tayari katika jamii.

Ushahidi wa ukubwa wa tatizo ni wa kutia hofu. Ripoti ya Disrupting Harm ya mwaka 2022 inakadiria kuwa, asilimia nne ya watumiaji wa intaneti wenye umri kati ya miaka 12 na 17 sawa na takribani watoto 200,000 walikumbwa na unyanyasaji wa kingono mtandaoni ndani ya mwaka mmoja.

Matukio haya yalihusisha vitisho, kulazimishwa kushiriki picha za ngono na usambazaji wa maudhui ya faragha bila ridhaa yao.

Wanawake nao wameathirika kwa kiwango kikubwa. Ripoti ya Plan International ya mwaka 2020 nayo ilibainisha zaidi ya asilimia 19 ya wanawake walipunguza au kuacha kabisa kutumia mitandao ya kijamii kutokana na unyanyasaji.

Wanawake wanaojihusisha na maisha ya umma, wakiwamo waandishi wa habari, wanaharakati na wanasiasa, mara nyingi hulengwa kwa mashambulizi ya makusudi yanayolenga kuwatisha na kuwanyamazisha kupitia mitandao hiyo y kidigitali.

Kwa mujibu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), ripoti ya mwaka 2023 ilionesha ongezeko la kesi za unyanyasaji wa kidijitali, hasa kwa wanawake wanaoshiriki masuala ya kisiasa.

Aidha, tathmini ya haki za kidijitali ya mwaka 2024 ilibaini zaidi ya asilimia 53 ya matukio yaliyorekodiwa yalihusisha mashambulizi ya mtandaoni, vitisho na ufuatiliaji.

Wataalamu wanasema unyanyasaji wa mtandaoni hauwezi kutenganishwa na uhalisia wa maisha ya mtu.

Mwanazuoni, Alfani Mduge wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT) anasema mitandao ya kijamii ni mwendelezo wa jamii yenyewe. Anasema shinikizo la kiuchumi, ukosefu wa ajira na ushindani wa kutambulika, hasa miongoni mwa vijana, huongeza pia uwezekano wa tabia za ukatili kujitokeza mitandaoni.

Kwa upande wa afya ya akili, wanasaikolojia wanaonya kuwa madhara ya unyanyasaji wa mtandaoni yanaweza kuwa makubwa kuliko ukatili wa kimwili.

Padri na Mwanasaikolojia, Leons Maziku wa Jimbo Kuu la Tabora anasema waathirika hupitia msongo wa mawazo wa muda mrefu, wasiwasi, kujidharau na hata mawazo ya kujiua, hali inayowaathiri zaidi watoto na vijana.

Teknolojia nayo imeongeza changamoto. Mtaalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Michael Mollel anasema matumizi ya akili bandia yameanza kuwezesha utengenezaji wa picha, sauti na sura bandia, jambo linalozidisha ugumu wa kuwabaini wahalifu na kulinda waathirika.

Kwa upande wa sheria, wanasheria wanakiri kuwepo kwa maboresho kadhaa, lakini wanasema utekelezaji wake bado ni dhaifu kutokana na hofu, unyanyapaa na uelewa mdogo wa umma kuhusu haki na njia za kuripoti matukio.

Hata hivyo, Serikali imeshachukua hatua mbalimbali za kukabiliana na hali hiyo, ikiwamo kuimarisha sera, sheria na kampeni za uhamasishaji.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima amesisitiza dhamira ya Serikali katika kuwalinda watoto na wanawake mtandaoni kupitia Mkakati wa Taifa wa Usalama wa Mtandao pamoja na utekelezaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.

Lakini wataalamu wanasisitiza kuwa suluhu ya kudumu itahitaji ushirikiano wa pamoja kati ya Serikali, kampuni za teknolojia, jamii na watu binafsi.

Kwa kuwa kadiri Tanzania inavyozidi kuingia katika ulimwengu wa kidijitali, changamoto kubwa inakuwa kuhakikisha mitandao ya kijamii inabaki kuwa jukwaa la fursa, ubunifu na mazungumzo yenye heshima, badala ya kuwa chanzo cha hofu, maumivu na ukimya.