Kuna jambo linanilazimisha kumkumbuka bwana aliyekwenda kung’oa jino baada ya kuhisi maumivu makali.
Lakini baada ya kuliondoa jino alilolihisi, akaendelea kupata maumivu kwenye meno mengine. Alirudi kumlalamikia tabibu wake, kwamba inawezekana amekosea tiba na kung’oa jino lisilo bovu.
Tabibu alijaribu tena na tena bila mafanikio, hatimaye akayaondoa meno yote. Wakati jamaa akiwa amebaki kibogoyo, ndipo tabibu alipogundua tatizo halikuwa meno, bali ufizi!
Hivi karibuni Tanzania imepitia wakati mgumu sana baada ya vurugu zilizotokea baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Pande tofauti zilishukiana kuhamasisha au kuanzisha sakata hilo lililogharimu maisha ya watu, lakini hakuna upande uliokubali kuhusika. Wananchi walivitupia lawama vyombo vya usalama vilivyokuwa upande wa Serikali, lakini navyo vilirudisha lawama hizo kwa wananchi.
Baada ya mvutano uliotingisha misingi ya umoja wa Kitaifa, lilikuja wazo na hatimaye muundo wa Tume ya Maridhiano. Tume iliundwa na kupewa kazi ya kusikiliza kada tofauti zikiwemo vyama vya siasa, taasisi za kiimani, makundi maalum, serikali na wananchi kwa ujumla ili kugundua tatizo halisi. Lengo ni kuwaweka pamoja kama Taifa ili kujadili mustakabali wao. Wananchi wengi walipata imani kuwa huenda tatizo likafikia kikomo na lisingejirudia.
Lakini maridhiano yanakuwepo iwapo wanaotofautiana watakaa pamoja. Namaanisha kwanza kila mmoja amjue aliyetofautiana naye, na wayaanike mbele yao yote yanaowakwaza.
Hapa sina uhakika wa kiini kilichoamsha vurugu za wakati ule kwa sababu kulikuwa na sura tofauti katika tukio; maandamano, wizi, uharibifu wa mali, matusi na kadhalika. Huwezi kuona dhima moja katika mchangamano kama ule.
Kwa hili naiona kazi ya Tume kuwa si ndogo. Ni kubwa zaidi ya inavyoonekana kwa macho au kusomwa kwenye makaratasi. Kwa mtazamo mwepesi Tume inaweza kushughulika na madhila yaliyoibuka siku hiyo tu ikadhani imemaliza kazi. Ni kama kuzipatanisha mamlaka za Israeli na Palestina kwa kuziwekea mipaka. Kumbe inawezekana kabisa kuwa tatizo lao ni zaidi ya mipaka, lakini hakuna anayelisema bayana.
Yapo matatizo ambayo hata wanaoyashiriki hawajui vyanzo vyake. Kwa mfano vijana waliosamehewa baada ya kujiingiza kwenye vurugu bila kutambua.
Ndivyo tunaona jinsi jitihada za kiulimwengu zinavyoshindwa kusuluhisha mgogoro wa Mashariki ya Kati kwa kutoelewa kinachosuluhishwa ni kitu gani.
Wengine wanadhani tatizo ni udini na wengine siasa. Lakini wengine wanaofarakana huko ni wa itikadi zinazofanana.
Moja ya sifa kubwa ya Watanzania ni amani na upendo. Huwa hawana visasi vya mioyoni, na ndio sababu wakabuni usemi wa ‘Yaliyopita si ndwele.’ Huu ni utamaduni wa kusahau machungu yanayopita na kujifariji kwa mazuri yajayo. Wameshakumbana na matatizo mengi wakayapitisha kama ndoto, wakaganga yaliyofuata na maisha yakaendelea. Hivyo ni vigumu sana kugundua viini vya matatizo yao. Naweza kuwafananisha Watanzania na watu wenye kinga thabiti kwenye miili yao. Hapo zamani tuliwashuhudia baadhi ya wazee waliojikinga na kujitibu kwa miti shamba.
Hawakuwa na haja ya kufanya vipimo na kuondoa matatizo yao, wao walipoumwa ugonjwa fulani walikwenda kuchimba mizizi na kujitibu. Lakini tiba ilipokataa na wakapelekwa Hospitali, walifia huko kwani vipimo vilishindwa kugundua viini vya maradhi.
Kwa maono ya baadhi ya watu, wanasiasa wanaweza kubebeshwa mzigo wa lawama kwa kile kilichotokea. Lakini jamii kubwa ya Watanzania haichukulii siasa kama jambo la kuwatofautisha. Huweza kushabikia vyama kama wanavyoshabikia michezo.
Si ajabu familia moja ikawa na baba aliye kiongozi wa Simba, mama shabiki wa Yanga na watoto wanaokula huku na huku. Kwa Simba wananunuliwa viatu lakini kwa Yanga wanakula pilau.
Tume iende mbali zaidi baada ya kupokea taarifa za walengwa. Ichimbue hadi ione mzee aliyekuwa akijitibu na miti shamba alikuwa na historia ya ugonjwa gani. Kama nilivyosema, Watanzania wana tamaduni zao za “yaliyopita si ndwele” na “kufunika makombe”. Inawezekana kabisa kuwa miongoni mwao wapo walioficha maumivu yao kwa ndwele, wakarithishana wao kwa wao. Iwe au isiwe hivyo, nashauri moja ya njia za kurudisha imani ya wananchi kwa Serikali, na Serikali kwa wananchi. Ni Serikali kutekeleza ahadi ilizotoa wakati wa kampeni. Viongozi waliopo madarakani walitoa ahadi ambazo bila shaka ndizo zilizowafungulia milango ya ushindi. Ahadi hizi zikitimizwa zitakuwa tiba ya maumivu ya jumla. Isisahaulike kuwa mgonjwa mmoja katika jamii anaweza kuifanya jamii nzima iwe mashakani.
Mwalimu Nyerere aliona kuwa pamoja na Tanzania kujipatia uhuru wake, bado haingekuwa salama hadi pale mataifa yote yaliyoizunguka yatakapokuwa huru.
Aliona jinsi maadui zake ambavyo wangetumia njia ya mkato kumfikia. Vivyo hivyo, ni hatari kubwa watu wenye madukuduku yao wanavyochangamana kwenye jamii. Hata kama kinachomkwaza ni kitu kidogo sana, lakini athari yake ni kubwa sana.
Hivyo kutimiza ahadi hasa kwa wakati inaweza kuwa sawa na dawa ya kuondoa sumu mwilini.
Kwa sasa hatuna sababu ya kunyosheana vidole kama vile utamaduni wetu unavyotuongoza.
