Dar es Salaam. Chama cha National League for Democracy (NLD), kimefanya kikao maalumu cha tathimini ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025, kwa lengo la kutathmini mwenendo wa uchaguzi huo na somo kwa mustakhabali wa chama hicho mbeleni.
Kikao hicho kimefanyika ikiwa ni mkakati wa kufanya mchanganuo wa mafanikio yaliyopatikana pamoja na changamoto zilizojitokeza katika maeneo mbalimbali nchini na kujadili namna chama hicho kinavyojipanga katika siasa zake.
Katika kikao hicho kilichofanyika leo Jumatano Januari 7, 2026, jijini Dar es Salaam, viongozi wa chama hicho wamekutana na waliokuwa wagombea wa nafasi mbalimbali, wakiwamo wa ubunge na udiwani kwa ajili ya kujadili kwa kina matokeo ya uchaguzi na kujifunza kutokana na uzoefu uliopatikana wakati wa mchakato wa uchaguzi huo.
Akizungumza na Mwananchi baada ya kikao hicho, Katibu Mkuu wa chama hicho, Doyo Hassan Doyo, ametoa rai kwa waliokuwa wagombea wa nafasi za uongozi katika uchaguzi huo kwa chama hicho kutokata tamaa wala kufa moyo kutokana na matokeo ya uchaguzi.
Amesema changamoto zilizojitokeza ni sehemu ya mchakato wa kidemokrasia, badala ya kuwa mzigo na kuwarudisha nyuma wanasiasa zinapaswa kuwa darasa la kujifunza na kuchukua hatuan mpya katika chaguzi zijazo.
“Nitoe rai kwa wagombea wote tulioshiriki katika uchaguzi huo kwa chama chetu nikiwamo mimi mwenyewe niliyegombea urais wa Tanzania, tusikate tamaa kutokana na matokeo mabaya yaliyotokea katika uchaguzi huo bali tujifunze kutokana na changamoto hizo uili awamu zijazo tuwe bora zaidi,” amesema akisisitiza dhambi kubwa katika mapambano ni kukata tamaa.
Doyo pia ametoa shukrani za chama hicho kwa wananchi waliokiunga mkono chama hicho katika uchaguzi akisema chama hicho kinajipanga kwa mikakati mipya ili kuhakikisha kina kuwa chama kikubwa na kuongeza ushindani katika chaguzi zijazo.
“Naomba niwashukuru wananchi kwa namna walivyokiunga mkono chama chetu katika kipindi chote cha kampeni za uchaguzi mkuu, kuanzia mwanzo wake hadi zilipohitimishwa rasmi Oktoba 27, 2025, sapoti hiyo ni ishara ya imani ya wananchi kwa chama chetu,” amesema.
Mbali na chama kuweka mikakati yake mipya ili kukabiliana na mazingira ya kisiasa yaliyopo nchini, Doyo ameweka nia kuwa chama hicho kipo katika maandalizi ya kusimamisha mgombea wa kugombea ubunge wa Peramiho mkoani Ruvuma, mara tu Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) itakapotangaza rasmi taratibu za uchaguzi huo.
Jimbo la Peramiho lipo wazi tangu aliyekuwa mbunge wake, Jenister Muhagama alipofariki dunia, Desemba 11, 2025 kinachosubiriwa kwa sasa ni hatua za tume kuweka wazi taratibu za kujaza nafasi hiyo kwa vyama vya siasa kusimamia makada wao kugombea.
Akielezea mazingira ya uchaguzi huo, aliyekuwa mgombea wa ubunge wa Segerea jijini Dar es Salaam, kwa chama hicho, Sabra Anthony amesema, chama hicho kimebainisha kuwepo kwa changamoto mbalimbali zilizokumba mchakato wa kidemokrasia zikiwamo za masuala ya kiutawala, mazingira ya kampeni pamoja na uelewa wa wananchi kuhusu sera na ilani za vyama.
“Tumeweza kujadili mambo mengi kuhusiana na uchaguzi huo ambao ulikumbwa na changamoto kadhaa za kiutawala zilkiathiri mchakato wa kidemokrasia na ushindani, tunakwenda kuzifanyia kazi na kurudi na nguvu mpya katika chaguzi zinazokuja,” amesema.
Akitoa mwelekeo wa chama hicho kufuatia hatua hiyo, aliyekuwa mgombea wa ubunge wa Babati Mjini mkoani Manyara, wa chama hicho, Paschal Ngumuo amesema chama hicho kinaendelea kuchukua hatua za kuimarisha mikakati yake ya kisiasa ili kuongeza ushindani na ufanisi katika chaguzi zijazo.
