Pedro agusa mkataba wa winga Yanga

BAADA ya winga wa Yanga, Denis Nkane kwenda TRA United kwa mkopo, kocha wa kikosi hicho, Pedro Goncalves ameufungua mkataba wa mzawa huyo akitaka kuangalia kiwango chake zaidi.

Iko hivi. Nkane ambaye ameichezea Yanga kwa misimu minne mfululizo alitolewa kwa mkopo hivi karibuni akiwa amesaliwa na miezi sita ili kumalizana na klabu hiyo.

Licha ya kuondoka kwake Yanga, Pedro ametaka mkataba wa Nkane uwe wa tofauti ili apate muda wa kumsoma zaidi akiwa TRA baada ya ugumu wa namba ambao alikuwa akiupitia ndani ya kikosi chake.

Nkane alicheza dhidi ya Yanga katika mechi ya kufungia makundi ya Kombe la Mapinduzi 2026 na TRA kulala kwa bao 1-0 lililofungwa na Celestin Ecua, na mechi hiyo ilitumiwa na kocha huyo kumsoma kwa karibu zaidi.

Taarifa za ndani zilizolifikia Mwanaspoti zinadai: “Pedro amekubali kuufungua mkataba wa mkopo wa Nkane, kwamba atakapokutana na Yanga ataruhusiwa kucheza ili amuone kiwango chake, Hiyo ni tofauti na mikataba mingine ambayo inamzuia mchezaji wakati atakapokutana na timu yake hataruhusiwa kucheza.”

Hivyo Nkane kama atapenya katika hesabu za Pedro basi msimu ujao Nkane atarejea kusaini mkataba mpya Jangwani na kuitumikia tena jezi ya njano na kijani.

Mzawa huyo ana uwezo kucheza beki wa kulia, winga na kiungo mshambuliaji, ambako kote huko kulikuwa na wachezaji kama Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli na wengine na alitua Yanga akitokea Biashara United kabla ya kocha Etienne Ndayiragije kupendekeza asajiliwe TRA ili amfanyie kazi kwa ngwe ya Ligi Kuu Bara.